Pages

Pages

Thursday, May 30, 2013

SABABU YA KIFO CHA MWANAMUZIKI ALBERT MANGWEA AFRIKA YA KUSINI HIKI HAPA.

Albert Mangwair PerformingALBERT MANGWEA AKIWAJIBIKA ENZI ZA UHAI WAKE KWA MASHABIKI WAKE.MWILI WA MAREHEM ALBERT MANGW EA AFRIKA YA KUSINI.

DAR ES SALAAM. 
WAKATI mazishi ya mwanamuziki marehemu Albert Mangwea(28) maarufu kama `Ngwair’ yakitarajiwa kufanyika mjini Morogoro, maeneo ya Kihonda baada ya mwili kuwasili nchini, hospitali iliyomfanyia vipimo imethibitisha kuwa pombe na dawa za kulevya kupita kiasi ndivyo vilivyomuua.
Mwili wa mwanamuziki huyo, ambaye alitamba kwenye miaka ya 2000 na wimbo wa `Mikasi’, unatazamiwa kuletwa kesho nchini na kuagwa Jumamosi kabla ya kusafirishwa kwenda kwao Kihonda, Morogoro kwa mazishi.
Kwa mujibu wa taarifa Mangwea alifariki dunia juzi kwenye Hospitali ya St Hellen, iliyopo Johannesburg, Afrika Kusini alikokuwa amekwenda kwa shughuli za muziki.
Kifo chake
Ripoti iliyochapwa na mitandao mbalimbali ya ndani na nje ya nchi inasema marehemu alifikwa na umauti baada ya kulewa kupindukia, kibaya zaidi alikuwa hajala.
Siku ya kifo chake, Mangwea alianguka nyumbani kwa rafiki zake akiwa katika hali hiyo ya kulewa sana.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya kufikishwa hospitalini, Mangwea aligundulika kulewa mara tano ya kipimo cha kilevi kilichopitishwa na serikali ya Afrika ya Kusini, ambacho ni 416mg za pombe kwenye kila milimita 100(kwa mlevi anayeendesha chombo cha moto).
Pia marehemu alikutwa na upungufu wa hewa ya oksijeni kwenye seli na tishu za mwili wake.
Ripoti hiyo ilibainisha kuwa Mangwea, maarufu Ngwair, alikuwa na tatizo la kutokula chakula vizuri kabla ya kifo chake na pia kukosa muda wa kupumzika.
Sampuli zilizopatikana mwilini mwake zinaonyesha mkusanyiko wa dawa za kulevya mbalimbali zikiwemo heroine, cocaine chafu na bangi ya gramu 0.08 ambavyo vilikutwa kwenye damu yake.
Kifo chake kilitokana na mshtuko wa moyo na kushindwa kupumua, hali iliyosababisha mapigo ya moyo wake kusimama kwa sekunde chache, na kusababisha kifo chake.
Mwili wa Ngwair ulionekana kana kwamba alitokwa na damu nyingi puani baada ya kuonyeshwa kwa Watanzania wengi jana jioni Johannesburg, Afrika Kusini.

WAHASIBU NCHINI KUFUNDISHWA MBINU ZA KUDHIBITI FEDHA HARAMU

Na Bertha Ismail  - Arusha


Wahasibu nchini watapatiwa mafunzo ya namna ya kutambua na kuzuia
fedha haramu maarufu kama fedha bandia  ili kudhibiti  tatizo hilo
ambalo limekuwa  likisababisha hasara kubwa katika sekta mbali mbali
nchini.

Mafunzo hayo yatatolewa na kitengo cha udhibiti wa fedha haramu
(financial  inteligency ) ambacho kiutawala  kiko chini ya wizara ya
fedha  ila kikazi wanajitegemea na kufanya kazi na wizara zote.

Akizungumza katika semina ya Wahasibu na Wakaguzi wa hesabu  za
serikali iliyokuwa ikijadili  kuhusu soko la mitaji na kutathmini
taarifa za kimahesabu ,maadili ya wahasibu iliyofanyika jijini
hapa.Pius  Maneno ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji  wa bodi ya taifa ya
uhasibu na ukaguzi wa mahesabu (NBA)  amesema kuwa semina hiyo
inalenga kutoa mafunzo ya namna ya kutambua fedha haramu na kuzizuia
ikiwa ni mada mojawapo itakayowasilishwa .

“Wahasibu na wakaguzi wa Mahesabu ya serikali watajifunza  mbinu mbali
mbali za kutambua fedha haramu na kuzizuia ,mafunzo hayo yatatolewa na
kitengo cha udhibiti wa fedha haramu ambacho kipo chini ya wizara ya
fedha kiutawala ila kiutendaji kinajitegemea na kufanya kazi na wizara
zote kwa kuwa tatizo la fedha haramu haliko katika wizara moja tu liko
katika wizara na sekta mbali mbali” Pius Maneno

Pius Maneno amesema kuwa  mbali na hayo  semina hiyo itajadili
ushiriki wa soko la hisa ,maboresho ya soko la mitaji  na fursa mbali
mbali na pia kutazama changamoto za namna gani Watanzania watawezeshwa
 katika soko la mitaji ili liwe kitovu cha uchumi katika maendeleo ya
taifa.

Kwa upande wake Mgeni rasmi aliyefungua semina hiyo Sonford Jacob
Shayo ambaye ni katibu tawala wa wilaya ya Arusha amesema kuwa
ushirikiano wa Ofisi ya Bodi ya taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa
Mahesabu(NBAA)  na Benki kuu ya Tanzania (BOT) unaweza kuleta tija na
kutatua changamoto za zinazowakabili wahasibu na na kuifanya taaluma
hiyo iweze kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma na maadili.

MKUU WA MKOA WA ARUSHA AINGIA KATIKA LAWAMA NA WANANCHI WA OLDONYOSAMBU

Na Bertha Ismail-Arusha
Wananchi wa kitongoji cha Engutukoiti kilichoko katika kijiji cha Losinoni Kata ya Oldonyo sambu wilayani Arumeru mkoani Arusha wamemlalamikia mkuu wamkoa wa Arusha kwa kupuuza madai yao ya kupatiwa hadhi ya kuwa kijij.

Aidha wananchi hao waliandamana hivi karibuni hadi kwa mkuu wa mkoa kuwasilisha madai yao ya kudai hadhi ya kuwa kijiji ambapo walisikilizwa na katibu tawala wa mkoa wa Arusha Exvery Mwanga kwa niaba ya mkuu wa mkoa ambapo aliwataka wananchi hao warudi majumbani mwao na kuwaahidi mkuu wa mkoa angeenda kuwasilikiza siku ya jumatano may 21 mwaka huu.

Aidha wananchi hao waliamua kutii amri hiyo kwa kuwa na imani na mkuu huyo, ambapo ilipofika may 21 wananchi hao walikusayika kumsubiri mkuu wa mkoa kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa mchana bila mafanikio ambapo mwenyekiti wa kitongoji cha Engutukoiti Lesikar Olobiis alijaribu kumpigia mkuu huyo na kuambiwa kuwa hana taarifa juu ya mkutano huo.

"Mimi baada ya kuona wananchi wamekusanyana hapa kutoka maeneo mbalimbali wakimsubiri mkuu wa mkoa bila mafanikio, niliamua kutafuta namba yake na kumpigia ambapo alisema kuwa yeye hana taarifa juu ya kikao hicho hivyo hawezi kuja" alisema mwenyekiti huo.

Aliongeza kuwa baada ya kujibiwa hivyo aliwaambia wananchi hao majibu aliyopewa hali iliyozua mtafaruku baina ya wananchi hao na baadhi yao kupandwa na jazba huku wakirusha maneno makali na kusema kuwa wamedhalilishwa na kudharauliwa na ofisi hiyo ya mkuu wa mkoa kwa kuahidiwa kusikilizwa jambo ambalo hawajatimiza.

mmoja wa wananchi Peter Senjore akiongea kwa jazba juu ya kutofika mkuu huyo alisema kuwawamekuwa na migogoro ya mara kwa mara kutokana na kutopewa haki yao ya kijiji lakini wakipeleka malalamiko hayo kwa viongozi husika akiwemo Mbunge wa jimbo hilo Godluck Ole Medeye  amekuwa nyuma kushughu;likia swala hilo hadi juzi kuamua kwenda kwa mkuu wa mkoa lakini matokeo yake ni kejeli na kudharauliwa.
|"Sisi wananchi wa kitongoji hichi tumekuwa kama si wananchi wa nchiii kwani kila tupatapo tatizo hakuna wa kushughulikia badala yake tumekuwa tukidharauliwa na kuonekana kama si kkitu, mfano mzuri ni juzi tulidai haki yetu hadi tukachoka bila msaaada na kuamua kulifikisha kwa mkuu wa mkoa tukidhani labda viongozi wetu hawafikishi matokeo yake ni kuwekwa hapa kama watoto wadogo haina shida Mungu atatutetea na kulipa, alisema mzee mmoja wa makam.

Mwananchi mwingine ni Selina Mohamed ambae kwa upande wake alilalamikia juu ya shughuli zake za kila siku alizoziacha ikiwemo kilimo, ufugaji na hata wengine kutokwenda kujitafutia riziri katika masoko kwa ajili ya kumsubiri mkuu huyo kuja kuwasilkiza na kutokomeza kero yao kubwa ya kupewa hadhi ya kuwa kijiji huku akisema kuwa baadhi ya watu wengine wametoka sehem za mbali lakini wameambulia kejeli za kudharauliwa.

Awali may 16 mwaka huu wananchi hao waliandamana hadi ofisi ya mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo kudai hadhi ya kupewa kijiji kwa madai ya kunyaswa na vitongoji vya jirani kwa kuwanyima huduma za kijamii kutokana na kitongoji hicho kupewa eneo kubwa na kufanikiwa kumiliki sehem ya malisho ya mifugo.

Katika maandamano hayo walipokelewa na katibu tawala wa mkoa Bwana Mwanga na kuwasilikiza huku akipokea makabrasha ya madai yao na kuwataka kurudi majumbani mwao kwani amekwishalifikisha na kuahidi kuwa mkuu kuyo angeenda kuwasilikiza tarehe 21 may hali ambayo imekuwa ndivyo sivyo kwa wananchi hao baaada ya kuambiwa na mkuu wa mkoa kuwa hana Taarifa hizo.

Pia ikumbukwe kuwa madai ya wananchi hawa kudai hadhi ya kuwa kijiji limekuwa la mda mrefu hali iliyosababisha migogoro ya hapa na pale baina ya kitongoji hicho na vingine vya jirani kwa ajili ya kugombe eneo hilo la malisho lililoko katika kitongoji cha Engutukoit na kusababisha watu wawili kupoteza maisha na maelfu ya mifugo kupotea huku kaya nyingi pia zikikosa mahala pa kuishi.


Baada ya mgogoro huo kupamba moto viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo mkuu wa mkoa wa Arusha alikwenda katika kata hiyo na kuzungumza na wananchi hao na kuahidi kufuatilia mpaka huo na kutatua tatizo hilo.
 
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Arusha Magesa Mulongo alipowasiliana na blog hii ya BERTHA BLOG juu ya madai hayo alisema kuwa yeye hana taarifa juu ya mkutano wala madai hayo hivyo aliyewaahidi amewatapeli tu na kuwataka waandishi na wananchi hao wakamuulize aliyesema maneno hayo.

kero ya maji Mlali mkoani Morogoro yaondolewa


Na Juma Mtanda, Morogoro

MKUU wa wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka amezindua mradi wa maji na usafi wa mazingira kwa shule za msingi Mlali na Vitonga wenye thamani ya Sh72.7milioni ukiwemo wa uvunaji wa maji ya mvua katika kata ya Mlali mkoani Morogoro. 
Mradi huo umetekelezwa na shirika la Environmetal Conservation, Water Sanitation and Aids Control Organization (EWACO) kwa ufadhili wa shirika la WaterCan na wananchi wa vijiji vya Mlali na Vitonga. 

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Mlali na Vitonga, Mtaka alisema kuwa shirika la EWACO limeondoa moja ya kero ya muda mrefu ya shule za msingi Mlali na Vitonga kwa kujenga miradi hiyo yenye thamani ya Sh 72.7 milioni.

Alisema kuwa ili miradi hiyo iweze kuendelea kudumu ni lazima walimu, wanafunzi na wakazi wa eneo hilo kutunza miundombinu yake ili iendelee kuleta faida kwa walengwa. 

Shirika Ewaco  linapwa kuigwa na mashirika mengine kutokana na utendaji wao kwani thamani ya fedha iliyotajwa inafafana na thamani ya miradi iliyotekelezwa. Alisema Mtaka. 

Naye Mratibu wa Shirika hilo, Stanley Shekigenda alisema kuwa shirika hilo imetekeleza miradi miwili ya uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa vyoo  katika shule za msingi Vitonga na Mlali kwa ufadhili wa shirika la WaterCan pamoja na kushirikiana na wananchi. 
Shekigenda alitolea ufafanuzi wa fedha zilizotumika kwenye miradi hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule ya msingi ya Mlali uliogharimu Sh46,6 milioni na shule ya Vitonga kiasi cha Sh26.1 milioni mbali na fedha kutoka EWACO pia wananchi wa Mlali imechangia kiasi cha Sh4.9 milioni na wale wa kijiji cha Vitonga wamechangia Sh2 milioni. 

Shekigenda alisema kuwa ujenzi wa mantaki mawili ya uvunaji wa maji ya mvua yenye ujazo wa lita 110,000 yaliyojengwa katika shule ya msingi ya Mlali na matundu 20 ya vyoo vya walimu na wanafunzi, wakati shule ya msingi Vitonga likijengwa tanki la lita 56,000 na ujenzi wa matundu 17 ya vyoo kwa walimu na wanafunzi. 
Mwisho…  

Saturday, May 25, 2013

SABABU ZABAINIKA ZA KUCHOMWA MOTO NYUMBA YA MTANGAZAJI WA TBC



Nyumba pamoja na gari la mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha Taifa TBC imechomwa moto juzi katika vurugu za Mtwara

Akizungumza katika mahojiano hayo mtangazaji huyo aliweka wazi sababu za nyumba yake kuchomwa moto kuwa ni kutokana na kazi anayoifanya mke wake.


Alisema kuwa mke wake ni polisi hivyo inawezekana ndiyo sababu kubwa iliyochangia kuvamiwa na kuchomewa nyumba yake moto pamoja na gari

Alisema kazi yake pia ni sababu ya pili iliyochangia kuvamiwa kwani vurugu za mara ya kwanza alikatazwa kuandikwa chochote juu ya vurugu hizo

Wakati huo huo jeshi la polisi limewashikiria watu 91 wanaodhaniwa kushawishi vurugu zilizotokea juzi mkoani Mtwara.

Akizungumza katika mahojiano maalumu katika kipindi kimoja wapo cha radio jijini Dar es Salaam Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mtwara alisema hali ya usalama inazidi kuimalisha ingawa bado wananchi wa mkoa huo hawajajitokeza kuendelea kufanya kazi zao za kijamii.

Alisema kuwa maeneo ya Magomeni ndiyo yaliyoharibiwa na vurugu hizo ingawa vurugu hizo zilianzia sokoni

HUYU NDIYE ALIYEMWAGIWA TINDIKALI VISIWANI ZANZIBAR, DKT. SHEIN AMJULIA.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein, akimsikiliza, Sheha wa Shehia  ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohamed Saidi Kidevu,(kulia) aliyelazwa Hospitali ya Mnazi Mmoja mjini Zanzibar baada ya kumwagiwa Tindikali na Mtu asiyejuilikana huko maeneo ya Tomondo juzi wakati alipokuwa akirudi kuchota maji na kuelekea nyumbani kwake. Sheha huyo anaendelea kupatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Mnazi mmoja (wa pili kulia) ni  Kaka yake Sheha Sudu Mgeni Saidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein,akimuangalia Sheha wa Shehia  ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja,Mohamed Saidi Kidevu,(kulia) jinsi alivyoathirika na Tindikali aliyomwagiwa na Mtu asiyejuilikanwa  huko Tomondo juzi wakati alipokuwa akirudi kuchota maji na kuelekea nyumbani kwake, wakati Rais alipomtembelea kumjulia hali Sheha huyo yupo katika Hospitali ya Mnazi mmoja .Kushoto Dkt.Slim Mohamed Mgeni. Picha na Ramadhan Othman Ikulu.

UGONJWA WA KUPINDA MIGUU WATOKOMEZWA AFRIKA MASHARIKI

Na Bertha Ismail -Arusha

Katika hali ya kuhakikisha ugonjwa wa kupinda miguu unatokomezwa kabisa hapa nchini, chuo cha mafunzo kwa watu wenye ulemavu kimewapa madaktari wa mifupa mafunzo ya wiki 2 ya namna ya kutibu ugonjwa huo bila opereshen hasa kwa watoto wadogo.

Hayo yameelzwa na mratibu wa mafunzo hayo, Grace Ayoo alipokuwa akizungumza na  waandishi wa habari mapema jana kwenye mafunzo hayo yalijumuisha madaktari wa mifupa kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini, yaliyofanyikia katika chuo cha mafunzo cha watu wenye ulemavu kilichoko USA river wilayani Arumeru Mkoani Arusha.

Alisema Mpango huo unaodhaminiwa na watu kutoka ujerumani, umefanikiwa kuwanyoosha miguu watoto zaidi ya 125 waliokuwa wamepinda miguu kutoka sehem mbalimbali hapa nchini katika chuo hicho hapo huku wakitarajia kusambaza huduma hiyo katika wilaya mbalimbali mkoani Arusha na baadae hata nchi nzima.

Grace alisema kuwa pamoja na juhudi za kutokomeza ugonjwa huo kwa watanzania lakini bado serikali ya Tanzania imekuwa haiko tayari kupongeza juhudi hizo kwa kuwasapoti kwa baadhi ya vifaa vya kutolea huduma ikiwemo pamba na P.O.P wakati wanaonufaika ni watanzania na kuongeza nguvu kazi ya taifa badala yake wanaosapoti kwa nguvu zate ni wajerumani.

Amesema kuwa kwa sasa wagonjwa ni wengi wanaojitokeza kutibiwa ugonjwa wa kupinda miguu, huku Iringa ikingoza hivyo kwa sasa wanataka kufungua tawi mkonia Iringa kuwasogezea wananchi hao huduma hii tofauti na sasa wanakuja hadi Arusha kufuata huduma hiyo.

Aidha alisema kuwa hadi sasa hawajui chanzo halisi cha ugonjwa huo ambapo bado wanaendelea kufanya utafiti kubaini na kutoa wito kwa jamii  kutohusisha ugonjwa huo wa ulemavu wa kupinda miguu na imani za kishirikina kama ilivyo sasa kwani ni ugonjwa wa kurithi na kutoka kwa mzazi mmoja au wote wawili ambo pia unatibika.

Kwa upande wake mwakilishi  wa wafadhili hao kutoka ujerumani Dr. Trine Heim alisema ugonjwa huo umekuwa kwa kiasi kikubwa hapa Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania.

Akielezea sababu za wao kufadhili mpango huo, alisema kuwa ujerumani wamefanikiwa kuutokomeza ugonjwa huo kwa kiasi kikubwa hivyo kuamua kusaidia ma watu wengine wakiwemo  watanzania lengo ikiwa ni kuutokomeza ugonjwa huo hapa Afrika.

Aliongeza kuwa kwa sasa mpango huo unaenda taratibu na kushindw a kufanikiwa kwa wakati kutokana na kulemewa na idadi kubwa ya wagonjwa huku serikali ya Tanzania ikishindwa kuusapoti mpanngo huo ili ulete tija kwa watanzania wengi zaidi kwa mda mchache.
 


CHADEMA YAMNG'ANG'ANIA KATIBU MKUU WA CCM ABDULRHMAN KINANA JUU YA PEMBE ZA NDOVU.

 
KATIBU MKUU WA CCM, ABDULRAHMAN KINANA.
KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kwa mara nyingine imezidi kumbana Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ikimtaka mwendesha mashitaka wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kumfungulia mashitaka ya kutorosha pembe za ndovu katika mahakama ya Afrika Mashariki.

http://polis.parliament.go.tz/images/Pictures/1608.jpgRaya Ibrahim Khamis.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo jana kwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka 2013/2014, Raya Ibrahim Khamis kwa niaba ya msemaji mkuu Ezekiel Wenje, alitaka Tanzania iombe msaada wa Kenya yenye ubalozi wa Vietnam ili kurahisisha upatikanaji wa ushahidi badala ya kutegemea ubalozi wake ulioko China.

Raya alisema madhumuni ya kumfungulia kesi Kinana yana lengo la kuudhibiti mtandao wa majangili na wafanyabiashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa wanataka Kina
na afunguliwe kesi kutokana na meli anazosimamia mojawapo ilikamatwa na shehena za pembe za ndovu huko Vietnam mwaka 2009.

Hii ni mara ya pili kwa kambi hiyo kuibua tuhuma hizo dhidi ya Kinana ambapo kwa mara ya kwanza msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alihoji jambo hilo na kupata upinzani mkali kutoka kwa wabunge wa CCM.

Raya alisema kuwa biashara haramu ya pembe za ndovu katika ukanda wa Afrika Mashariki inakua kwa kasi jambo linalotishia kutoweka kwa wanyama ndovu ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.

Alisema kuwa taarifa katika mtandao wa habari wa “Annamiticus” (www.annamiticus.com) zinasema kwamba mwaka jana, makontena mawili kutoka Kenya na Tanzania yalikamatwa huko Hong Kong yakiwa yamebeba tani 4 (kilo 4,000) za pembe za ndovu.

“Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kontena lililotoka Tanzania lilikuwa limeandikwa “plastic scrap” ikimaanisha kuwa lilikuwa na vifaa ya plastiki, lakini baada ya kufunguliwa kulikuwa na vipande 972 vya pembe halisi za ndovu zenye uzito wa kilogramu 1,927 pamoja na kilo moja na nusu ya unga wa pembe za ndovu zilizosagwa.

“Kontena lililotoka Kenya lilikuwa limeandikwa “roscoco beans” yaani maharage aina ya roscoco, lakini lilipofunguliwa kulikuwa na vipande 237 vya pembe za ndovu sawa na kilogramu 1,884,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa hiyo, wingi wa pembe hizo za ndovu zilizokamatwa, unadhihirisha kwamba tembo 600 kwa uchache waliuawa.

Aliongeza kuwa mwezi uliopita kontena jingine limekamatwa limesheheni pembe za ndovu 113 huko China zenye thamani ya dola za Marekani 400,000 likiwa limeandikwa kwamba limebeba vipuri (spareparts) kutoka Burundi.

“Kwa kuwa Burundi haina bandari, kuna uwezekano mkubwa kwamba kontena hilo lilipitia bandari ya Tanzania, na hivyo kuna uwezekano pia kwamba pembe hizo zinatokana na tembo waliouawa Tanzania,” aliongeza.

Alisema kambi hiyo inataka kujua kama Serikali ya Tanzania imefanya mawasiliano na Burundi ili kujua ukweli kuhusu kontena lililosheheni pembe za ndovu lililokamatwa huko China.

Aliongeza kuwa kwa kuzingatia utekelezaji wa mpango mkakati wa amani na usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kubadilishana taarifa za uhalifu na usalama, ni vema serikali ikiwasiliana na wote wanaoweza kukamilisha uchunguzi husika.

Alisema kuwa kuna Watanzania walioshutumiwa na kusutwa kuhusika na mtandao huu wa biashara hii haramu ya pembe za ndovu akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Kinana.

“Kwa kuwa Serikali ya Tanzania inaonekana dhahiri kumtetea na kumlinda mtu huyu kwa kuwa ni kiongozi mkubwa wa chama tawala, kama alivyofanya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi alipokuwa anatoa mchango wake kwenye bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii Aprili 30 mwaka huu.

“Na kwa kuwa tembo wengi wa Afrika Mashariki wanazidi kupotea kila siku kutokana na biashara hii haramu ya pembe za ndovu, jambo ambalo linaikosesha Jumuiya ya Afrika Mashariki mapato yatokanayo na utalii na hivyo kuiweka hatarini sekta ya utalii ya Afrika Mashariki, watu hawa lazima washtakiwe,” alisema.

Raya pia aligusia uhuru wa habari kwa nchi wanachama huku akinukuu taarifa ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) ya Mei 20 mwaka huu ambayo ilisema kuwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameamuru kufungiwa kwa gazeti la kila siku la nchi hiyo la “The Daily Monitor”, na gazeti lingine la “Red Pepper”.

Hatua hiyo ni kutokana na kuchapisha habari iliyofichua njama za Rais Museveni za kumuandaa mtoto wake, Muhoozi Kainerugaba ambaye ni brigedia wa jeshi kuwa rais wa nchi hiyo baada ya yeye kuondoka madarakani.

Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba yake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliomba mwongozo wa kiti akitaka wapinzani wakemewe kwa kukiuka kanuni na kutaja majina ya viongozi wakuu wa nchi kwa dhihaka.

“Mimi sitaki kuzungumzia suala la Kinana maana hizo ni porojo wacha waendelee, lakini nazungumzia ukiukwaji wa makusudi wa kanuni na kumtaja Rais Museveni kwa mambo ambayo eti msemaji ameyasikia kwenye redio pamoja na lile la Kinana japo tumeishajibu, lakini wanaendelea kujifurahisha. Naomba ukemee jambo hili,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Lukuvi kuketi, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika naye aliomba mwongozo akitumia kanuni inayomruhusu mbunge kunukuu taarifa kwenye vyombo vya habari akisema kuwa Raya alikuwa sahihi.

Sitta amkingia kifua
Akijibu hoja hiyo wakati wa majumuisho, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliwataka CHADEMA wamuache Kinana afanye siasa na majibu watayaona mwaka 2015.

Sitta alisema CHADEMA imekuwa ikitumia nguvu kulazimisha hoja zao na inaonekana Kinana ndiye anayewakera kwa kuwa hatoki midomoni mwao.

“Kila siku Kinana…Kinana…jamani hebu acheni kumhusisha na biashara haramu ya pembe za ndovu,” alisema.

THE CIVIC UNITED FRONT- (CUF – CHAMA CHA WANANCHI) TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 24/05/2013 GHASIA ZA MTWARA.

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba
TTHE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) kimesikitishwa sana na vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na polisi tarehe 23 Mei 2013. 
Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua ume
me wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.

CUF inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim Mikongolo, na nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani vikali vitendo vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la Mikindani linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

CUF imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari wanne wa JWTZ kwa ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.
Tumepeleka salamu za pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia za marehemu. 
Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa letu.

Vilevile tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa kupigwa risasi akiwemo mama mjamzito na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole familia za marehemu na kuwaombea wote waloumia wapone haraka na waendelee na shughuli zao.

Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia hizi zilianza baada ya hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini iliyosomwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Taarifa tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia asubuhi, wakati Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa Jeshi la Polisi walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia. 
Polisi walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na kuwachukua kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za moto zilipigwa hovyo hovyo. 
Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo waliwapiga wake zao, watoto wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao wanasumbua. Binti mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. 
Katika eneo la Mkana Read, Polisi walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za raia zimechomwa moto na polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya wafanyabiashara. 
Wananchi wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia nyumba zao. Taarifa tulizopata zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada ya maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi kufika Mtwara.

Vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi Jeshi la Polisi kupiga watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara na kupora mali za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali na kuchoma vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana. Weledi ndani ya Jeshi la Polisi uko chini sana. 
Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na kupora. Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya polisi waliohusika na vitendo hivyo.
Tunatoa wito kwa asasi za haki za binadamu na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai haki zao.

Pamoja na kulaani vitendo hivi vya kihalifu na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo, Serikali itafanya makosa makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu na wananchi wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa wanasiasa wachache wanaojitafutia umaarufu. 
Narudia Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa. 
Mradi mwingine ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama malighafi kama ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki visima vya gesi ya Mnazi Bay na Msimbati. 
Kama miradi hii ingeanza kutekelezwa nina uhakika wananchi wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.

Kauli ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali itawasaka waasisi wa vurugu hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta mchawi badala ya kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa serikali ya CCM. 
Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata viongozi mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea, kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF.
Serikali ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu wasiokuwa na hatia. CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi tumejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu utekelezaji wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza. 
Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.

Mimi binafsi nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya ya Tandahimba. 
Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja na kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali. Tarehe 14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara sikukaidi nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.

Kuwakamata viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na Lindi na wa kitaifa hakutamaliza mgogoro kati ya serikali na wananchi wa Mtwara ikiwa serikali itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza. Badala yake itaongeza chuki dhidi ya serikali.

Wakati wananchi wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi wa CCM na serikali yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za kiraia kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia. 
Umma uliokata tamaa na unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza kuchukua hatua zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.

Serikali imekuwa inapotosha kwa makusudi madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi ya gesi iliyoahidi wananchi wa Mtwara. 
Badala yake wananchi wa mikoa mingine wanalishwa sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi iwanufaishe Watanzania wengine.
Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa katika gridi ya taifa utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi ya taifa. Kiwanda cha mbolea cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi nzima. Wananchi wa Mtwara hawajasema Watanzania wengine hawana haki ya kwenda Mtwara kupata ajira au kufanya shughuli za kibiashara. 
Wanaobomoa umoja na mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza, kuwadharau na kuendelea kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza sumu kwa Watanzania wengine kwa kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kushindwa kwa serikali kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.

Wananchi wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na kupeleka ombi (petition) kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni kujadili kutekelezwa kwa miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia ombi hilo kujadiliwa.

Bunge limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa nini mradi wa kufua umeme MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12 ulitengewa na kutumia shilingi 540 milioni umesitishwa.
Mpaka hivi sasa hakuna kamati ya Bunge iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake Spika amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.

Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza serikali kupitia TANESCO kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga kituo cha kufua umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa kupitia Songea. Hata hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu wala kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi. 
Wananchi wa Mtwara wanaona wanaendelea kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli za kejeli za Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara katika masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi. 
Mpaka hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba na upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya gesi wataweza kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia gesi mkoani Mtwara.

Linalonistusha na kunitisha ni kwa nini viongozi wa juu wa serikali hawataki kuwa wawazi kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha, kuwagawa wananchi na kudanganya alimuradi mradi huu utekelezwe na usihojiwe?

Gesi ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982 lakini mpaka hivi sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza utaratibu wa kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18. 
 Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake wa kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi – Netherlands Development Finance Company. 
Gharama za mradi wa kufua umeme zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225. Kampuni maalum ya kuendesha mradi huu ya Tanzania Generation Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na kuendesha mradi huu. 
Kampuni hii ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65 zingechangiwa kama hisa na kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya madini ya Barrick International.

Kampuni nyingine maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili ijenge msongo wa umeme (nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na kuunganisha umeme wa Mnazi Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu dola milioni 400. 
Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania na wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National Power Development Master Plan). 
Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco inaueleza mpango huu kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali iliukabali mradi huu baada ya kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.

Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa mwaka 2008 uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa moja ya Artumas iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia dola 0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata na ilibidi serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na ufuaji wa umeme wa MW 18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa TANGEN. 
Katika kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.

Tarehe 10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa anawahutubia Wabunge na Wananchi katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari za mtikisiko wa uchumi duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua. 
Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. 
Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na ajira. 
Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.” 
Kwa kauli ya Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla waliisikia kwani hotuba hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji la Tanzania – Radio na Televisheni na vyombo vingine vya habari. 
Miradi ya kutumia gesi ni pamoja na kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia gesi kama malighafi, aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha saruji ambacho kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi. 
Wananchi wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia mbadala ya kujikwamua ili miradi hiyo iendelee.

Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete aliwaeleza wananchi wa Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara itakayotumia gesi ya Mnazi Bay. 
Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010, ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi Bay (k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam. Mitambo ya kufua umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa itumie gesi ya Songosongo kwani bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka Dar es Salaam lingepanuliwa. 
Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas ilijiandaa kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka Songosongo – Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya kufua umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. 
Serikali iliisitisha kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa umekamilika na kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau MW 200.

Rais Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya Mashujaa tarehe 25 Julai 2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo ufuaji wa umeme wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.

Tarehe 12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye gridi hiyo. 
Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida. 
Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300 kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”

Mikoa sita ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya taifa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na kufua umeme wa MW 300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye gridi ya taifa. 
Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.”

Maelezo haya yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari vikayatangaza na wananchi wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni kuanzisha viwanda hasa ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya Mtwara. 
Mwaka wa fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi 540 milioni fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development Project. 
Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena. Badala ya mradi huu kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.

Kwa taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme wa MW 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa gharama yake ni dola milioni 684. 
Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa na mkopo wa dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China. 
Ni wazi gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye gridi ya taifa ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.

Msongo wa umeme za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa – Dodoma – Singida na Shinyanga. 
Mradi huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga umeme za kV 400 ni dola za Marekani  600,000 kwa kilomita 1. Gharama za kujenga bomba la gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa kilomita 1. 
Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni zaidi ya mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam. Isitoshe unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusambaza kwa msongo huo huo.

Ujenzi wa bomba la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha hadi Dar es Salaam. 
Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za ujazo bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.

Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 33.7 imegunduliwa katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado haujaanza. 
Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado hazijafanya uamuzi wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi nchi kavu. 
Kwa kuwa gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni za juu sana, kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu kwenye eneo lililo fupi kuliko yote. Statoil imegundua gesi nyingi eneo la Zafarani bahari kuu eneo la mkoa wa Lindi. 
Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa kuweza kuweka kituo cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa ambayo ina kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. 
Kwa hivi sasa hakuna uhakika gesi iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga bomba kubwa umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida zake kiuchumi. Jambo la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha kutekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na uwajibikaji wa kisiasa?

Wentworth Resources wamefanya upembuzi yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara. 
Kiwanda cha mbolea chenye faida kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya gesi iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay. 
Mradi wa kujenga kiwanda unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea kiwanda kitazalisha methanol yenye soko kubwa duniani.
Kiwanda kitatumia hewa ukaa (carbondioxide) na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha mazingira. Uongozi wa Wentworth Resources una uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam.

Serikali imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi yenye manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kwa taifa letu. 
Uchunguzi huru na wa kina ufanyike kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara na kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa itolewe ili Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu. 
Mkataba wa mkopo na utekelezaji wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi. Serikali iruhusu kampuni ya Wentworth resources kuendelea na mradi wa kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.

Vyama vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za wananchi wa Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa nini Mradi wa Kufua umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.

Sakata hili la gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa hatuna sera muafaka na mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa letu na Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa itakuwa balaa na laana. 
Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu zitakazohakikisha kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na utakaolinufaisha taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi. 
Wananchi wa Mtwara wanahitaji kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi ya gesi.

Friday, May 24, 2013

AMRI KIHEMBA ASAINI YANGA KWA MKATABA WA MIAKA MIWILI.




Mshambuliaji wa Simba, Amri kihemba kulia akimtoka beki wa Ruvu Shooting ambapo mchezaji huyo amesajili na mabingwa wa soka msimu wa mwaka 2012/2013 Yanga Sport Club kwa mkataba wa miaka miwili.
 WAKATI Haruna Niyonziam akiwa amesaini mkataba wa miaka miwili kuichezea Yanga, habari zilizotufikia hivi punde zinasema kiungo wa Simba, Amri Kiemba amesajiliwa na Yanga tayari kwa kuitumikia timu hiyo kwa msimu ujao.
Akizungumza na mtandao huu, mtu mmoja kutoka kamati ya usajili ya Yanga, amesema Kiem
ba amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili ili kuongoza nguvu katika safu ya usajili ya Yanga.
Mtandao huu unaahidi kuwasiliana na Kiemba muda mfupi atakapotoka mazoezini katika kambi ya Taifa Stars kujiandaa na mechi ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014.
Atakapotoka mazoezini mtandao huu utawasiliana naye kiungo huyo ili aweze kueleza ukweli juu ya usajili wake kwa Yanga.
Kiemba aliwahi kuichezea Yanga miaka ya nyuma kabla ya kutimka katika timu hiyo.

Wednesday, May 22, 2013

MONGELA AWATAKA VIJANA KUJITAMBUA


mwongela
MKUU wa wilaya ya Arusha , John Mongela amewataka vijana kujitambua na kujiamini huku wakiepukana na tabia ya kutumiwa na vyama mbalimbali vya siasa na kuishia kuwanufaisha wengine na wao kuendelea  kubakia maskini.

Aliyasema hayo jana  wakati akizungumza na vijana kutoka maeneo mbalimbali , ikiwemo vyuoni na wajasirimali wadogowadogo pamoja na viongozi  kutoka serikalini katika semina iliyofanyika mjini hapa .

Alisema kuwa, vijana wanapaswa kujitambua kuwa wana fursa mbalimbali ambazo wanapaswa kuzitambua na kuzitumia badala ya kubweteka na kukaa bila shughuli za kufanya na wengine kuishia kutumia na vyama mbalimbali vya siasa  hali inayochangia wengi wao kujiingiza katika makundi yasiyofaa.

 ‘unajua vijana wengi kutokana na kutokuwa na kazi za kufanya wameishia kutumiwa na vyama vya siasa hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kubaki kama walivyo na kuendelea kuwanufaisha vyama  hivyo, ni vizuri mjifunze kujituma na kutumia fursa zilizopo kwa kujiletea mafanikio zaidi’alisema Mongela.

Naye Mwenyekiti Mtendaji wa  chuo cha mafunzo ya uandishi wa habari na biashara (EABMTI) ,Rosemary Mwakitwange alisema kuwa, lengo la mkutano huo ni kuangalia namna ya vijana wa kitanzania wanaweza kupata fursa zilizopo hapa na kuweza kuzitumia kwa manufaa yao kwa ujumla.

Alisema kuwa, ili vijana waweze kujikwamua kiuchumi ni lazima tufike mahali sasa tuweze kuwajengea ujasiri wa kuweza kujitambua wao kwanza na hatimye kuzimbua fursa zilizopo katika maeneo yao na kuzitumia kwa manufaa yao na nchi kwa ujumla .

Alisema kuwa , chuo hicho ndio waratibu wa mradi huo hapa nchini  ambapo wamekuwa wakiandaa mikutano mbalimbali yanayohusiana na  maswala mbalimbali ya kiafya na kujamii ya vijana haswa wa kike wenye umri kati ya miaka 15 -24.

Aidha  mikutano hiyo wameshafanya  katika mikoa ya Pwani, Tanga, Iringa,Manyara,na Zanzibar ambapo hii ikiwa ni awamu ya pili  wamepanga kufanya mikutano mingine ya aina hiyo katika mikoa ya Rukwa, Kilimanjaro, Zanzibar,Mwanza,  na Ruvuma .

‘Unajua katika semina hii tunazungumzia  mradi wa ‘je tufanyeje  mradi unaodhaminiwa na shirika la USAID chini ya Sauti ya Amerika (VOA)  katika kujadili maswala mbalimbali ya vijana na fursa  za kiuchumi zilizopo miongoni mwao na kuweza kuzitumia kwa lengo la kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na hatimaye kuwawezesha kufikia malengo yao’alisema Mwakitwange.

Aidha semina hiyo imedhanimiwa na shirika la misaada la watu wa Marekani (USAID) chini ya uangalizi na uandaaji  wa Idhaa ya Kiswahili ya sauti ya Amerika (VOA).

ASKARI WANNE WA JWTZ KIKOSI CHA 41KJ WAFA AJALINI WILAYANI NACHINGWEA LINDI WAKIWA NJIANI KWENDA KUWAONGEZEA NGUVU POLISI WA MTWARA!



ASKARI WANNE WA JWTZ KIKOSI CHA 41KJ WAFA AJALINI WILAYANI NACHINGWEA LINDI WAKIWA NJIANI KWENDA KUWAONGEZEA NGUVU POLISI WA MTWARA!
chanzo;JUMAMTANDA BLOG