Pages

Pages

Sunday, September 29, 2013

CHADEMA, CUF, NSSR WATINGA KWA MSAJILI WA VYAMA KUPINGA RAIS KIKWETE KUSAINI MUSWADA WA MAREKEBISHO YA KATIBA MPYA.



MUUNGANO wa vyama vya siasa vya upinzani nchini, jana ulitinga ofisi za Msajili wa Vyama, Jaji Godfrey Mutungi, kwa nia ya kueleza dhamira yao ya kupinga Rais Jakaya Kikwete kuusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Vyama hivyo vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, vinavyounda ushirikiano wa kisiasa wa kupinga Rais kusaini muswada huo, vilimfafanulia Msajili huyo kilichotokea bungeni hivi karibuni, kwa wabunge wa upinzani nje ya ukumbi wa Bunge, wakati wale wa CCM wakipitisha muswada huo pamoja na marekebisho yake.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viunga vya viwanja vya Ofisi ya Msajili, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa ushirikiano huo, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema moja ya mapendekezo waliyompatia Msajili ni kutaka maridhiano ya kikatiba, hivyo Rais Jakaya Kikwete asisaini sheria hiyo.

“Tumefanya mazungumzo na Msajili, tulifika kumsabahi na kumweleza yaliyojiri bungeni kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, mchakato ulianzia tume mpaka kura ya maoni ya katiba… Zanzibar haikushirikishwa, Serikali ilipeleka vipengele 6,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alisema Oktoba 10 mwaka huu, ni siku ya kitaifa ya kupinga kusainiwa kwa Sheria hiyo na kwamba maandamano yatakayofanyika yatakuwa ya amani.

“Oktoba 10, wananchi wajiandae kukutana katika viwanja vya Jangwani, ni siku ya kitaifa, taratibu zote zitaelezwa, maandamano, mikutano na shughuli zote zitakuwa za amani. Hatusubiri Jeshi la Polisi kuzuia, Jeshi la Polisi linapokea taarifa na zitafuatwa kadiri iwezavyo,” alisema Profesa Lipumba.

Akizungumza kwa niaba ya Chadema Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alisema ushirika wao utatumia njia za kidemokrasia kushinikiza Rais asisaini Sheria hiyo.

“Tutatumia njia za kidiplomasia kupinga na kuwaandaa wananchi kwa kutumia njia hizo, kwani jambo hili limekuja kwa muda muafaka kutokana na kauli zilizotolewa na viongozi wa masuala hayo, Jaji Joseph Warioba na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema kauli ya Jaji Warioba juu ya kuwepo kwa kasoro katika kipengele kinachomhusisha pamoja na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inasadifu uhalisia wa mapungufu yaliyomo kwenye sheria hiyo, na kumtaka kwenda mbali zaidi kwa kuainisha vipengele visivyokidhi upatikanaji wa Katiba mpya.

Alisema makundi mbalimbali pamoja na wananchi wa Zanzibar hawakushirikishwa wakati Kamati ya Bunge ya Sheria ikikusanya maoni.

Pia alisema kauli iliyotolewa hivi karibuni na Waziri Chikawe kuwa Katiba haipatikani Kibanda Mti wala Jangwani ni ulevi wa madaraka na wala haitarudisha nyuma juhudi za Muungano huo kwa maslahi ya wananchi.

Pia alisema Waziri Chikawe amewahi kukiri kuwa kuna vifungu vya katiba ambavyo havikushirikisha Wazanzibari na kwamba kigezo hicho kilipaswa kutumika kwa Waziri huyo kumshauri Rais Kikwete asisaini.

Hata hivyo, Jaji Mutungi hakuweza kupatikana kuzungumzia mwafaka uliopatikana na kama mapendekezo hayo ameyapokea, badala yake msemaji wake, Happiness Muyombo, alisema Msajili huyo ana kikao kirefu, hivyo atazungumza na vyombo vya habari wakati mwingine.

Vyama hivyo viliamua kuungana kwa pamoja kupinga kusainiwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 pamoja na kutangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.

DADA WA FREEMAN MBOWE, GRACE MBOWE AFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA GARI BARABARA KUU YA KABUKU TANGA.

  Grace Mbowe mwanamama aliyehama chama cha Chadema na kuhamia CCM wilayani Hai amefariki dunia katika ajali mbaya ya dari iliyotokea Kab
uku mkoani Tanga mapema asbuhi ya jana Septemba 29/ mwaka huu. 

Gerce ni dada wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freema Mbowe. Tutaendelea kuwajulisha juu ya tukio hilo, mwenyezi mungu ampumuzishe kwa amani.
chanzo: jumamtanda

Saturday, September 28, 2013

SERIKALI INAZIDI KUWANYIMA WANANCHI KUPATA HABARI, NI BAADA YA KUIFUNGIA MWANAHALISI SASA KUYAFUNGIA MAGAZETI YA MWANANCHI NA MTANZANIA KWA MDA


 
 
.

Gazeti la MWANANCHI limefungiwa kutochapishwa kwa siku kumi na nne (14) kuanzia 27 Septemba, 2013. Adhabu hii imetangazwa kwa Tangazo la Serikali (Government Notice ) Namba 333 la tarehe 27 septemba,2013.

Gazeti la MWANANCHI limepewa adhabu hiyo kutokana na hivi karibuni kuchapisha habari zenye mwelekeo wa uchochezi na uvunjifu wa amani, mfano tarehe 17 Julai, 2013 katika toleo Namba 4774 ilichapisha habari isemayo “MISHAHARA MIPYA SERIKALINI 2013” kwa kuchapisha waraka uliozuiliwa kwa matumizi ya vyombo vya habari waraka huo ulikuwa wa Siri haukupaswa kuchapishwa Magazetini.

Aidha, katika toleo la Jumamosi, tarehe 17 Agosti,2013 lilichapisha habari yenye kichwa kisemacho “WAISLAM WASALI CHINI YA ULINZI MKALI” habari hiyo ilikolezwa na picha ya mbwa mkali mwenye hasira.

Habari na picha hiyo ilitoa tafsiri ya kuwa Jeshi la Polisi lilipeleka Mbwa katika maeneo ya ibada ya waumini wa dini ya kiislam. Jambo ambalo halikuwa la ukweli. 

Jeshi la Polisi katika doria siku hiyo halikupeleka mbwa katika maeneo ya Misikiti.

Serikali na jeshi la Polisi linaheshimu na kuzingatia maadili ya dini ya Kiislamu na kwa hiyo Jeshi lake haliwezi kupitisha au kuingiza mbwa katika maeneo ya ibada.

Hivyo basi, kwa gazeti hili kuchapisha habari iliyokolezwa na picha ya mbwa ni uchochezi wa kulichonganisha Jeshi la Polisi na waumini wa dini ya kiislam mbwa ni najisi hapaswi kuingia katika maeneo ya ibada. 

Gazeti la MTANZANIA limefungiwa kutochapishwa kwa siku tisini (90) kuanzia tarehe 27 Septemba, 2013 kwa kuchapisha habari zenye uchochezi.

Gazeti hili limeonywa mara nyingi lirekebishe mtindo wake wa uandishi wa kichochezi na lizingatie maadili na Sheria na Kanuni za fani ya Habari.

Pamoja na kuonywa gazeti hili halikuonyesha kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Magazeti, mfano ;katika toleo na 7262 la 20 Machi,2013 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “URAIS WA DAMU”,tarehe 12 Juni,2013,toleo Namba 7344 lilichapisha makala isemayo “MAPINDUZI HAYAEPUKIKI”. 

Aidha, siku ya Jumatano,tarehe 18 Septemba,2013 katika toleo Namba 73414 ukurasa wa mbele lilichapisha Kichwa cha habari kisemacho “SERIKALI YANUKA DAMU” taarifa hiyo ilikolezwa na picha zilizo unganishwa kwa ustadi mkubwa kwa kutumia kompyuta kutapakaza rangi nyekundu mithili ya damu nyingi kumwagika.

Katika habari hiyo gazeti hilo limedai bila uthibitisho kuwa Jeshi la Polisi linahusika na wahanga waliomizwa na watu wasiojulikana kwa kumwagiwa tindikali na waliyovamiwa na kujeruhiwa vibaya. 

Vile vile gazeti hilo limeishtumu serikali kuwa goigoi katika kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi. Kwa ujumla wake habari hiyo ni ya kichochezi ina lengo la kuwafanya wananchi wavichukie vyombo vya ulinzi na usalama wavione kuwa haviwasaidii. 

Kutokana na makosa yalitajwa hapo juu serikali imelifungia gazeti la Mtanzania kutochapishwa kwa muda wa siku tisini (90) kwa Tangazo la Serikali Namba 332 (Government Notice No.332) la tarehe 27 septemba,2013,. Serikali inawataka wamiliki,wahariri na wanahabari kwa ujumla kuwa makini, kuzingatia weledi, miiko na madili yataaluma uandishi wa habari. 

Serikali inawataka wamiliki na hasa wahariri kuhakisha kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoviandaa vinazingatia taaluma, kuweka mbele maslahi ya taifa letu kwa kuwa na uzalendo wa hali ya juu. 

Serikali inavionya vyombo vya habari vinavyoutumia uhuru wa habari bila wajibu kuwa haitasita kuvichukulia hatua kali ikiwemo ya kuvifungia. Serikali haitakubali kuona vyombo vya habari kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani nchini. Imetolewa na

MKURUGENZI IDARA YA HABARI WIZARA YA HABARI,VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO 28 SEPTEMBA, 2013.

NI WATU 67 WALIOTHIBITISHWA KUPIGWA RISASI NA WANAMGAMBO WA AL-SHABAAB KATIKA JUMBA LA WESTGETE MALL IKIWA NI JUMA MOJA SASA LIMEPITA.


Wakenya walimaliza siku tatu za maombolezi Ijumaa.

Imetimia juma moja kamili tangu jengo la maduka mjini Nairobi kushambuliwa na watu wengi kuuwawa.

Watu wenye silaha walivamia jengo la Westgate, magharibi mwa Nairobi, na kwa siku kadha waliendeshana mbio na vikosi vya usalama huku wakifyatua risasi na kuuwa wateja waliokuwamo kwenye maduka hayo, pamoja na watoto.

Hadi sasa inajulikana kuwa watu 67 waliuwawa.

Mamia ya watu walikuwemo kwenye jengo la biashara washambuliaji walipoanza uvamizi Jumamosi iliyopita.

Mwandishi wetu mjini Nairobi anasema moto bado unatokota sehemu ya jengo hilo.

Alama za risasi zinaonekana kwenye kuta - matokeo ya mapambano baina ya jeshi la Kenya na wapiganaji.

Zana nzito zinatumiwa kunyanyua kifusi cha saruji, na hapo ndipo itajulikana iwapo washambuliaji waliuwawa na mateka wangapi zaidi walikufa.

chanzo: BBC

Friday, September 27, 2013

TANESCO yapoteza bil. 2/-


                                                                                       na Grace Macha, Arusha


SHIRIKA na Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) linapoteza zaidi ya sh bilioni mbili kwa mwaka kutokana na wizi wa mafuta ya transfoma na uharibifu wa miundombinu ya umeme.
Aidha, Mkoa wa Arusha unaongoza kwa matukio ya uharibifu huo, ukiwamo wizi wa nyaya za shaba za hasara ya zaidi ya sh milioni 800, ukifuatiwa na Kilimanjaro zaidi ya sh milioni 400 na Tanga.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felchesmi Mramba, alieleza hayo jana wakati akikagua kituo kidogo cha kisasa cha  kusambaza umeme kinachojengwa kwa zaidi ya sh bilioni 11.4 karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Aliwaomba wananchi kushiriki kikamilifu kuwafichua watu hao wanaolisababishia hasara taifa na kukwamisha juhudi za TANESCO.
Mramba alisema kuwa wanafikiria kukabiliana na wizi wa mafuta kwa kutumia transfoma zisizotumia mafuta, lakini wamekuwa wakikwama kufanya hivyo kutokana na gharama ya transfoma hizo kuwa ghali mara tatu ya bei ya hizi.
Alisema kuwa asilimia 20 ya umeme unapotea kabla ya kumfikia mteja ambapo tatizo hilo husababishwa na masuala ya kiufundi na yasiyo ya kiufundi.
Akizungumzia kituo hicho chenye uwezo wa kuzalisha 40 mega voltage amperes (MVA), alisema kuwa kiko kwenye hatua za mwisho kukamilika na kinatarajiwa kuzinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu na Rais Jakaya Kikwete.
Alisema kuwa kituo hicho kitasaidia kumaliza tatizo la umeme kwenye mikoa ya Arusha na sehemu za Kilimanjaro na Manyara, ambayo wakati wa jioni hukabiliwa na tatizo la kuwa na umeme mdogo.
Naye Meneja wa Arusha, Genes Kakore, alitaja maeneo yatakayonufaika na umeme huo kuwa ni Bomang’ombe, Mirerani, KIA, USA-River na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela.

SERIKALI INASHUGHULIKIA MAOMBI YA MWEKEZAJI MOLLEL KUUZIWA N.M.C

                                                                                         na Grace Macha, Arusha

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema serikali inashughulikia maombi ya mwekezaji kwenye kinu cha kusaga na kukoboa nafaka cha Arusha (NMC), Kampuni ya Monaban ya kuomba kuongezewa mkataba au kuuziwa kiwanda hicho.
Aidha, alimpa pole kwa madai aliyomweleza ya kupata usumbufu kutoka kwa watendaji wa serikali ambao walifikia kuzima mashine wakati akiwa anaendelea na usagaji wa nafaka jambo lililosababisha bidhaa hizo kuharibika.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi baada ya kutembelea kiwanda hicho na kujionea shughuli za ukoboaji na usagaji wa mahindi na ngano zilivyokuwa zikiendelea pamoja na kuona ghala la uhifadhi wa bidhaa hizo.
“Nimeona unasononeka na kuumizwa sana na uamuzi wa vinu vingine kuuzwa na hiki hakikuuzwa, uamuzi ulifikiwa baada ya kuunda bodi ya nafaka na mazao tukaona hiki na kile cha Iringa tusiviuze viendelee kusimamiwa na bodi hii.
“Nimeona umewekeza, umefunga mashine mpya, lakini ombi lake Bwana Molel, apewe kipindi kirefu zaidi au auziwe hiki kiwanda, tumeshaongea na watu wa kilimo ili watazame na sisi tutaangalia,” alisema.
Pinda aliongeza kuwa huo ndio mchango wa serikali kwenye uwekezaji, japo wakati mwingine wakiwekeza kwenye mali za umma wale wanaowekwa wasimamie wanaziua zaidi.
Alipongeza jitihada za Kampuni ya Monaban katika kukifufua kiwanda hicho sanjari na kushiriki ipasavyo katika kununua mahindi ya wakulima mpaka ngazi wa chini vijijini, ambapo ameuza mahindi tani 7,600 kwa wakala wa ghala la chakula la taifa Kanda ya Kaskazini kwa msimu huu wa kilimo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Monaban, Philip Mollel, alisema kuwa mwaka 2007 aliingia mkataba wa miaka 15 wa kufufua kinu cha ngano kilichokuwa kimekufa kwa zaidi ya miaka 10 na kukarabati kinu cha mahindi ambapo ametumia zaidi ya sh bilioni 6.2 kufanya kazi hiyo.
“Mkataba nilioingia ni wa kufufua, kukarabati, kuendesha na kuzalisha unga wa ngano na mahindi hapa NMC Arusha kwa miaka 15, ambapo baada ya kipindi hicho kampuni yetu inaweza kuingia mkataba mwingine,” alisema.
Hata hivyo alisema kuwa kampuni yake inashindwa kufanya maboresho zaidi, ikiwamo kufunga mitambo mikubwa zaidi, kuweka lami eneo la ndani ya kiwanda na kujenga uzio imara wa matofali ya saruji kuzunguka kiwanda hicho kutokana na kukosa ushirikiano kutoka serikalini.
Hali hiyo alidai inasababishwa na urasimu anaofanyiwa na Shirika Hodhi la Mitaji (CHC) ambalo hutumia waraka namba 40 wa serikali kumzuia asinunue kiwanda hicho wakati waliuza viwanda vingine kwa wafanyabiashara wenye asili ya Asia baada ya waraka huo kuwa umetolewa.
“Hivi majuzi Agosti 31, mwaka huu CHC bila kunipa taarifa huku wakijua nimewekeza walikuja kiwandani kwa lengo la kukabidhi kiwanda kwa bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko.
“Walifanya hujuma ya kuzima mashine bila taarifa wala ridhaa yangu. Mpaka sasa sijaelewa lengo lilikuwa ni nini. Uzimaji huo uliisababishia Monaban hasara kubwa sana hasa ukizingatia kuwa tani 120 za ngano na 60 za mahindi zote kwa pamoja zilikuwa tayari kwenye mfumo na mchakato wa uzalishaji hivyo nafaka hizo ziliharibika,” alisema

MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA YA KATIBA 2013 UNA KASORO !!!.

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

DAR ES SALAAM. 
WAKATI wananchi wa kada mbalimbali wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Kat
iba 2013, kwa maelezo kuwa una kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba naye amesema sheria ina upungufu.

Warioba alisema jana kwamba ni jambo la kushangaza sheria hiyo kueleza kuwa tume hiyo itavunjwa baada ya kukabidhi Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba, wakati huohuo ikieleza kuwa itahusika tena kusimamia utoaji wa elimu ya kura ya maoni.

Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.

Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: “Mwisho wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura ya maoni ?”.

Jaji Warioba pamoja na kukiri upungufu huo, alisema kurekebisha au kutokurekebisha kasoro hizo si jukumu la tume hiyo.

“Tunawaomba watafakari, waone jinsi gani tume ambayo imekwishavunjwa itakuja kutoa elimu wakati wa kura ya maoni, sheria ina ‘contradiction’ (ina mkanganyiko),” alisema.

Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM baada ya wale wa upinzani kutoka nje baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe kuamuriwa na Naibu Spika, Job Ndugai kutoka nje kutokana na kukaidi kwake amri ya kukaa chini alipokuwa akitaka kutoa hoja kabla ya mjadala wake kuanza.

Muswada huo unapingwa kwa kuwa Rais amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe 166, ambao si wabunge wala wawakilishi na Zanzibar kutokushirikishwa kikamilifu kwenye maandalizi ya muswada huo.

Hata hivyo, Warioba alisema pamoja na kasoro hizo Tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata sheria hiyo huku akisisitiza, “Wanaotunga sheria ni wengine siyo sisi, tulipoteuliwa tulikuta sheria na kuanza kazi kwa kuifuata. Imefanyiwa marekebisho sisi tunafuata.”

Alisema waliofanya mabadiliko ya sheria hiyo wana haki ya kufanya hivyo na kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba haiwezi kuzuia kutokufanyika kwa mabadiliko hayo, kwani yapo baadhi yanaihusu.

Alisema baada ya kuipata sheria hiyo: “Tulijiuliza maswali kwa sababu miswada huwa inapelekwa bungeni na Serikali ikiwemo ya Katiba. Anayeipeleka kama ni waziri ndiye anayetoa ufafanuzi pale inapohitajika.”

Alisema kulingana na sheria, tume yake ndiyo inayotakiwa kutoa ufafanuzi katika Bunge la Katiba, kama ambavyo Waziri hutoa maelezo anapowasilisha muswada bungeni. 
 
                                                                                                                 MWANANCHI