Pages

Pages

Tuesday, February 2, 2016

Riba kubwa na ukosefu wa elim ya biashara inafilisi wakopaji

Arusha . Riba kubwa inayotozwa kwenye taasisi za fedha pamoja na ukosefu wa elimu ya biashara ya kuwawezesha wananchi kuwekeza fedha wanazokopa kwenye miradi ya uzalishaji mali imeelezwa kama chanzo cha kufilisi wakopaji na kufaidisha taasisi hizo.

Akizungumza mkoani Arusha kwenye mkutano mkuu wa kitaifa wa 26 wa wanachama chama cha ushirika wa Akiba na mikopo cha Tumaini SACCOS, mwenyekiti Neema Fredrick amesema kuwa asilimia kubwa ya matajiri duniani waliofanikiwa ni kutokana na mikopo lakini kwa sasa watu wengi wamekuwa wakifilisiwa na mikopo kutokana na kukopa fedha na kuwekeza kwenye miradi isiyozalisha.

“Matajiri wengi duniani wamefanikiwa kutokana na mikopo na kukopa kwa malengo ya kuzalisha, lakini kuna watu wengi pia wamelizwa na mikopo kwa kufilisiwa hata kile kidogo walichokuwa nacho kabla ya kukopa, na sababu kubwa mbali na riba kubwa inayotozwa kwenye taasisi za fedha kuwa chanzo lakini pia kukopa na kwenda kuwekeza kwenye mradi usiozalisha ni kikwazo hivyo ili kuepukana na hili tuepuke kukopa fedha bila kuwa na mradi wa uhakika siyo kukopa kwa anasa au kununua vitu vya kwenda na wakati”

Neema alisema kuwa kutokana na hilo, walianzisha SACCOS hiyo ya tumaini yenye miaka 24 sasa ambayo katika chama chao wameweza kuwa na fedha kiasi cha bilioni 4.4 kutokana na wanachama 787 ambayo lengo kubwa ni kuweka na kukopeshana wanachama kwa riba ndogo lakini baada ya kugundua wengi wanashindwa kulipa mikopo yao ambayo wanadai zaidi ya milioni 150 wameamua kutoka elim ya biashara sambamba na kuendelea kufuatilia madeni yao.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Arusha, msajili wa vyama vya ushirika mkoa ambae alikuwa mgeni rasmi, Nerei Kyara alisema kuwa uwepo wa vyama hivyo vya kuweka na kukopa kumesaidia kwa asilimia kubwa kupunguza malalamiko pamoja na kesi nyingi za mikopo sambamba na kusaidia wananchi kujiongezea kipato kutokana na kubuni miradi mbali mbali ya kufanya na kupunguza hata ukosefu wa ajira hasa wale wanaowekeza kwenye miradi mikubwa kama viwanda kwani haujiri pia.

“Kwa Arusha pekee tuna zaidi ya vyama 400 na kila chama kina wananchi wetu ambao wengi wako kwenye ajira rasmi na wengine hawako kwenye ajira lakini kutokana na hivi vyama wanaweza kujiendeshea maisha yao bila kuwa tegemezi kutokana na kukopeshana wanachokusanya hivyo kupunguza hata mzigo kwa serikali kuwa na idadi kubwa ya watu tegemezi hivyo kwa sasa watu wazingatie elim ya biashara ili kuweza kunufaika na vyama hivi badala ya kuviua”

“Zaidi ya yote niwatake muache kukopa kwa kuangalia mkumbo au wanawake kununua vitenge na wengine kununua magari kwani mwisho wa siku haitakusaidia zaidi itakufilisi hivyo jitahidini kukopa na kuwekeza kwenye miradi itakayowapa faida na kuwezesha kurejesha mkopo husika kwenye vyama hivi huku mkiachana na taasisi zinazotoza riba kubwa ili kukuza uchumi wenu binafsi na taifa kwa ujumla”

Kwa upande wake mmoja wa wanachama Journey Mwampalile amesema kuwa kwenye chama chao hadi sasa wanaweza kukopa kuanzia milioni moja hadi milioni 40 kwa mwanachama mmoja kwa kurejesha kwa asilimia ndogo ambapo kwa upande wake amefanikiwa kuanzisha miradi mbali ya ufugaji wa mifugo kama kuku, na maduka ya jumla mjini ambayo familia yake inaishi vizuri kwa kusomesha watoto na kujenga nyumba nzuri na kuondokana na kupanga chumba.

“Hata kama ukiwa na elim ya biashara lakini kukopa kwenye taasisi za fedha ni ngumu kukua kwa haraka kutokana na riba kubwa wanayotoa lakini uanzishwaji wa hivi vikundi vya SACCOS vinasaidia sana kutokana na mtu kukopa fedha aliyowekeza na baadae kukopa lakini pia mwisho wa siku kuna faida kutokana na vikundi hivyo ambayo wanachama hugawana kutokana na miradi ya chama tofauti na taasisi hizi faida ni za mmiliki wa taasisi pekee hivyo niombe watu wajiunge kwenye hivi vikundi wanufaike zaidi kwa kukuza uchumi kuliko kutegemea serikali kila kukicha kwa ajira”

Kwa mujibu wa Neema amesema kuwa kutokana na wanachama wao wengi kutokana na mashirika na world Vision na vision fund baadhi yao wanakaribia kufikia kustaafu hivyo kwa sasa wanafanya mpango wa wanachama wao kupata elim ya maisha baada ya kustaafu ambapo pia watawasaidia mitaji ya kuendeleza maisha yao.

Mwisho…………………

JAJI MKUU OTHUMAN CHANDE ATOA SIKU SABA KWA MAHAKIMU 508 WATOE MAELEZO KWANINI WASIFUNGULIWE MASHITAKA KWA KUFANYA KAZI CHINI YA KIWANGO

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam leo mchana , kuhusu utendaji wa mahakimu wa mahakama za hakimu mkazi, mahakama za wilaya na mahakama za mwanzo ambapo alitoa siku saba kwa mahakimu 508 watoe maelezo kwani ni wasifunguliwe mashitaka ya nidhamu na kuwajibishwa kwa kufanya kazi chini ya kiwango. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omari Mallungu na kulia ni Jaji Kiongozi wa Tanzania, Shaban Omari Lila. Jaji Chande alitoa kauli hiyo kwenye maonyesho ya wiki ya Sheria yanayoendelea viwanja vya Mnazi Mmoja. 
  Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, akikaribishwa kutembea mabanda mbalimbali kwenye maonesho hayo.
 Mkurugenzi Msaidizi Ukaguzi na  Maadili Mahakama ya Tanzania, Warsha Ng'humbu (kushoto), akimuelekeza jambo Balbina Mrosso (kulia), kutoka Babati mkoani Manyara aliyetembelea banda la Idara ya Malalamiko kuomba msaada wa kisheria katika maonyesho hayo.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande, akisoma moja ya daftari katika banda la Idara ya Malalamiko kwenye maonyesho hayo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Malalamiko Mahakama ya Tanzania, Happiness Ndesamburo.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Othuman Chande (kulia), akielekezwa jambo katika banda la Divisheni ya Biashara katika maonesho hayo. 

JAJI Mkuu wa Tanzania Othuman Chande ametoa siku saba kwa mahakimu 508  watoe maelezo ni kwanini wasifunguliwe mashtaka ya nidhamu na kuwajibishwa, baada ya kufanya kazi chini ya kiwango.

Jaji Chande ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Viwanja vya Mnanzi Mmoja jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Wiki ya Sheria.

Alisema kiwango cha kesi kwa kila Hakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ni 250, ambapo Mahakimu Wakazi 121 kwenye mahakama hizo wameamua kesi chini ya 100 mwaka jana.

Alibainisha kuwa kiwango cha kwa kila Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni 260, ambapo mahakimu Wakazi na Mahakimu  wa Mahakama za Mwanzo 387 wameamua kesi chini ya 100 mwaka jana.

"Ukiondoa wale ambao wameajiriwa karibuni, wanaofanya kazi kwenye mahakama za mwanzo zisizokua na mashauri mengi au waliyokwenda masomoni kati kati ya mwaka  au likizo za ujauzito hawatahusika katika sakata la kujieleza.

"Majaji Wafawidhi nimewaagiza wachambue na kuanisha mahakimu wote walioshindwa kufikia kiwango cha kesi walizopaswa kuamua kesi 250 na kesi 260 kwa mwaka jana na kuwataka watoe maelezo ndani ya siku saba kwa nini wasichukuliwe hatua," alisema Jaji Chande

Jaji Chande alitoa muda wa kukamilika kwa mchakato huo, ambapo walizitaka idara husika ndani ya siku 21 kila kitu kiwe kimekamilika ili ijulikane ni hatua gani wanachukuliwe.

"Mahakama haikubali hakimu ambaye anabembeleza kesi. Hakimu hatakiwi kufanya hivyo anatakiwa asikilize kesi hizo naazimalize. Haiwezekani katika mahakama moja hakimu mmoja anamaliza kesi 800 mwingine anamalizia chini ya 100  hilo halitakubalika kutokana na kasi ambayo tunayo," alisema

Jaji Chande alisema mahakimu hao watapelekwa katika kamati zao kwa hatua ya kujieleza. Kazi kuu ya kamati hizo ni kupeleleza, kuchunguza na kushughulikia mashtaka yote ya nidhamu ya mahakimu.

"Mahakimu wote walioshindwa kufikia malengo ya mwaka la kesi na kushindwa kutoan sababu za kuridhisha kwa nini wameamua idadi ndogo ya kesi kuliko walivyopaswa, ambapo itashughulikiwa haraka na Kamati za Maadili za Mahyakimu kwa mujibu wa sheria na taratibu za haki," alisema

Hata hivyo, Jaji Chande alitoa pongezi kwa mahakimu ambao wamevuka kiwango, ambapo mahakimu 14 wameamua zaidi ya kesi 700 kwa mwaka jana na mahakimu wengine wamesikiliza kesi 915,789 na 778.

Alisema mkakati wao ni kuanza kesi sifuri mwaka unapoanza, kwa sababu kuna baadhi ya mahakama za mwanzo zimekuwa zikimaliza kesi na kuanza mwaka upya.


Jaji Chande alisema Januari 1, 2015 mahakama za mwanzo zilianza na kesi 34,126 na mwaka huu Januari 1 zilianza na kesi 20,431. Kiwango cha kumaliza kesi ukilinganisha na idadi ya kesi zilizosajiliwa 2015 nni zaidi ya asilimia 100. Mahakama ya Mkuranga asilimia 141, Rufiji asilimia 121 na Bukoba Mjini asilimia 224.

WAZIRI MKUU MAJALIWA AFANYA ZIARA HOSPITALI YA RUFAA MAWENZI


Mkuu wa wilaya ya Moshi,Novatus Makunga akisalimiana na Waziri mkuu  Majaliwa.

Waziri Mkuu  akislimiana na Mstahiki meya wa  Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya .
alipowasili
Waziri mkuu akitizama chumba cha kupigia  pcha za mionzi (X Ray) katika hospitali  ya rufaa  ya Mawenzi.

Waziri mkuu akiwa wodi ya watoto alipotembelea kujionea namna ambavyo  wagonjwa wanahudumiwa.
Waziri mkuu Majaliwa akizungumza jambo na mganga  mkuu wa mkoa  wa Kilimanjaro, Dkt Mtumwa  Mwako.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro akitoa taarifa ya mkoa kwa Waziri  mkuu  Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mbunge wa jimbo la Vunjo , Mhe. James Mbatia walipokutana Ikulu ndogo mjini Moshi

EALA yaombwa kuondoa Burundi katika uanachama wa jumuiya EAC

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza
BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), limeombwa kuiondoa nchi ya Burundi katika uanachama wa jumuiya hiyo na ile ya Umoja wa Afrika (AU) hadi hapo mgogoro wa kisiasa na kijamii utakapomalizika nchini humo.
Ombi hilo limewasilishwa mjini hapa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika, Donald Deya, alipowasilisha maombi ya mashirika sita yasiyo ya kiserikali kutoka EAC yaliyoomba kuzungumza na Bunge juu ya mgogoro wa Burundi.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Mambo ya Ndani ya Bunge na Usuluhishi wa migogoro ya EALA inayoongozwa na Mwenyekiti Abdullah Mwinyi, Deya alisema nchini Burundi bado kuna shida ya kisiasa na kuna Serikali iliyochaguliwa, lakini si halali kisheria.
Alisema pamoja na maombi ya kuondolewa kwa nchi hiyo, bado itaendelea kushiriki kwa karibu katika meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta mwafaka utakaowezesha kupatikana kwa amani na kuondoa shida zinazowakabili kwa sasa.
“Kitu cha msingi ambacho tunaliomba Bunge hili, litumie mbinu zote kuhakikisha Warundi wote wamefika mezani kwenye mazungumzo ya kutoa mwafaka wa shida yao. Na mbinu wanazoweza kutumia zipo nyingi,” alisema Deya na kuongeza:
“Sisi tunasema kwa sasa Serikali ya Burundi iwekwe ‘suspended’ (pembeni) kabisa kwenye uanachama wa Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ule wa Umoja wa Ulaya (AU),” alisema Deya.
Akiwasilisha maombi hayo ndani ya ukumbi wa Bunge uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini hapa, Deya alisema kumekuwapo na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na kijamii huku baadhi wakiogopa na kuiona nchi hiyo inaweza kuteketea na kuingia kwenye mauaji ya kimbari.
“Kwa maoni yetu ukilinganisha mazungumzo ya utatuzi wa mgogoro wa Burundi na mazungumzo yaliyosaidia kuiondoa Kenya kwenye machafuko mabaya ya kisiasa mwaka 2008, utaona tofauti kubwa kabisa,” alisema Deya.
Akifafanua kuhusu mazungumzo yaliyoinusuru Kenya kutumbikia kwenye wimbi la mauaji zaidi, alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa AU na Rais wa Ghana, John Kufor, aliiwezesha nchi hiyo kurejea kwenye amani tofauti na ilivyo kwa Burundi leo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge EALA, Mwinyi alisema kwamba maombi yaliyowasilishwa na mashirika hayo sita kupitia jopo la wanasheria wa Afrika yamesikilizwa na wajumbe wa kamati hiyo.
“Kuna mambo mengi wamependekeza, leo wajibu wetu Kamati ya Bunge ni kuyasikiliza na kutafuta ufafanuzi wa kina, ushahidi na baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyajadili na baadaye tutaandika ripoti na kuipeleka Bunge ili nalo lijadili na kutoa maazimio ya mapandekezo,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Sisi hapa hatuna dhamira ya kumtenga mtu wala kikundi au Serikali, dhamira yetu ni kusikiliza na kikubwa tunachokitafuta hapa ni suluhisho ili hatimaye tusitishe mauaji yanayotokea Burundi kwa pande mbalimbali.”

Pluijm : mechi ya Prison ni kama fainali

KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans Van der Pluijm, amesema anauchukulia mchezo wao wa kesho dhidi ya Tanzania Prisons kama fainali kwani unahitaji nguvu, umakini mkubwa, kujiamini ili kutimiza mafanikio ya ushindi.
Yanga inashikilia nafasi ya kwanza katika msimamo wa ligi hiyo, huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja katika michezo 16 ambayo imecheza hadi sasa ikifanikiwa kuwa na pointi 39.
Hata hivyo, Yanga imefanikiwa kubaki nafasi hiyo baada ya Azam iliyoko nafasi ya pili ambayo ina mchezo mmoja mkononi kwa kuwa imecheza michezo 15 kuwa nje kwa ziara ya michezo ya kirafiki na ina pointi 39. Tanzania Prisons yenye pointi 27 inahitaji pointi tatu hizi ili kufikisha pointi 30 na kujiweka vizuri katika msimamo wa ligi.
Akizungumza na MTANZANIA, Pluijm alisema wanatambua si rahisi kupata ushindi katika uwanja huo wa Sokoine, ila watajitahidi kuweza kuondoka na pointi tatu katika mchezo huo.
Kikosi cha Pluijm kinakabiliwa na majeruhi ambayo yameathiri safu yake imara ya ulinzi baada ya kuumia nahodha wa timu hiyo na beki wa kati, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Haji Mwinyi na ile kadi nyekundu aliyoipata Kelvin Yondani katika mchezo dhidi ya Coastal Union wikiendi iliyopita.
Kocha huyo raia wa Uholanzi alisema pamoja na kupata pigo kwenye safu ya ulinzi kutokana na majeruhi hao, hawezi kumchezesha beki mkongwe, Cannavaro ambaye tayari ametolewa hogo (POP), kwani bado hajapona vizuri majeraha yake ya mguu, akifanya hivyo upo uwezekano wa kuendelea kumkosa katika mechi nyingine muhimu zinazofuata.
Alisema kwa sasa Cannavaro hawezi kucheza anaendelea na programu maalumu ya mazoezi ambayo ameanzia kwenye gym na baada ya kuridhika na maendeleo ya afya yake atamruhusu kujiunga na wenzake mazoezini.
Akimzungumzia beki Yondani ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo uliopita, Pluijm alikiri kuwa ni pigo kubwa ndani ya kikosi chake hasa kwa kipindi hiki ambacho wanakabiliwa na mechi ngumu mbele yao.
Alisema Yondani alitakiwa kucheza kwa utulivu na umakini wa hali ya juu kuliko kufanya jambo ambalo linaweza kuigharimu timu, hakupaswa kupaniki na changamoto alizokuwa akizipata kutokana na ushindani uliokuwepo kati yao.
“Tayari tumesahihisha makosa yetu, hivyo sifikirii kushindwa tena, pia tunatambua mzunguko huu wa pili kila mchezo kwetu ni zaidi ya fainali.
“Tunatarajia kucheza dhidi ya Prisons ya Mbeya, tayari tumeshawasili na tumeanza kufanya mazoezi asubuhi na jioni ili kujiweka tayari na mchezo, kwa sasa hatuangalii tuna pigo gani bali tunaangalia ushindi,” alisema.
Pluijm alieleza kipigo dhidi ya Coastal Union kimewafanya kuimarika zaidi, baada ya kufahamu makosa yao na kuwa tayari kuyasahihisha.
“Kila mchezo ni lazima tushinde na tutaufanya kama fainali ili kufikia lengo la kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,” alieleza Pluijm.
Hata hivyo, mchezo huo umeonekana kuwa na hisia kubwa kwa mashabiki wa Yanga, ambao wamejipanga kuhakikisha timu hiyo inaondoka na ushindi.
Akizungumzia mchezo huo, shabiki Saleh Kupaza, alisema mchezo dhidi ya Yanga na Prisons ni mgumu kwani timu zote zimekuwa zikizihitaji pointi hizo tatu katika kujiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi.
“Mchezo wa Jumatano (kesho) ni mgumu kwani kila timu inahitaji pointi hizi tatu muhimu, ukiangalia ratiba ya Prisons ni ngumu kwani wakimaliza kibarua na Yanga, wanatarajia kukutana tena na mahasimu wao Mbeya City siku ya Jumamosi,” alisema.
Yanga wamewasili Mbeya juzi jioni na kuweka kambi ndani ya Jeshi la Wananchi 44KJ, Mbalizi nje kidogo ya mji na wanatarajiwa kufanya mazoezi katika Uwanja wa Sokoine jana jioni, huku Prisons wakiendelea kujifua ndani ya Uwanja wa Shule ya Sekondari Sangu.
Prisons imelazimika kuutumia uwanja wa shule hiyo kwa muda baada ya kupisha ukarabati wa kiwanja chao kilichopo ndani ya Jeshi la Magereza.