Pages

Pages

Wednesday, October 31, 2012

KASHFA YA TUHUMA ZA RUSHWA ZAIKUMBA YAIKUMBA SOKO JIPYA LA NMC


 Kashfa ya tuhuma za rushwa yaibuka katika soko jipya la NMC baada wafanyabiashara wadogowadogo (machinga) kulalamikia ugawaji wa kinyemela kwa baadhi ya maeneo kwa watu ambao siyo wamachinga wa katikati ya jiji kama ilivyokuwa lengo la kuhamishwa kwao.





Wakizungumza na waandishi wa habari sokoni hapo kwa hasira, baadhi ya wafanyabiashara hao waliokosa maeneo ya kuuzia na matokeo yake kuuza nje ya soko huku wakifukuzwa mara kwa mara na mgambo wa jiji, walisema kuwa ndani ya soko kuna baadhi ya maeneo yameshikwa na watu wasio wamachinga.





“Kama mnavyoona ndugu waandishi, ndani ya soko kuna baadhi ya maeneo yako wazi (hayatumiki) lakini sio kama hayana watu, kuna watu lakini siyo wamachinga bali wametoka mbali na kushika maeneo ndani ya soko huku wahusika tunauza nje baada ya kukosa maeneo huko ndani ya soko” alisema mmoja wao Scola Clement, na kuongeza


“Pia ugawaji wa meneo haya kulitawaliwa sana na rushwa kwani katika ugawaji wa maeneo ukiwa na mkono mfupi( usipotoa hela) hutapewa eneo bali utazungushwa hadi utaamua mwenyewe kutoa hela upate eneo baada ya kushuhudia mwenzako aliyetoa hela amepewa eneo haraka, mbali na hilo pia katika kugawa maeneo haya siyo yote yalikuwa wazi bali kuna baadhi yalikwisha gawiwa kabla hata ya tangazo rasmi kutoka”





Aliongeza kwa kusema kuwa “baada ya tangazo kutoka tulipoenda kushika maeneo baadhi ya maeneo tuliambiwa yamekwisha chukuliwa wakati ndio siku ya kwanza tena alfajiri, matokeo yake leo hii yale maeneo tuliyokuwa tunaambiwa yamekwisha chukuliwa leo wahusika ambao ni wafanyabiashara wakubwa mijini na wengine ni wa masoko mengine wanatuuzia yale maeneo kwa shilingi laki tatu(300,000) kama siyo walipewa maeneo haya kwa rushwa ni nini” alihoji.





Mfanya biashara mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mussa Hamis alizidi kusisitiza kuwa rushwa ilitawala katika ugawaji wa maeneo hayo “mimi kama mimi naamini rushwa ilitawala sana kwani mbali na baadhi ya maeneo kupewa watu ambao siyo wahusika na leo kuja kutuuzia, pia kuna baadhi ya watu wamepewa maeneo makubwa ya mabanda mawili na zaidi, wengine madogo ya banda moja huku wengine wakipewa eneo lisilotosha hata kibanda 1”





Mussa alisema kuwa pamoja na halmashauri ya jiji kusikia kilio chao cha kupatiwa eneo la kufanyia biashara na kupewa eneo hilo lakini bado wako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko hasa katika msimu huu wanaotarajia mvua, nah ii ni kutokana na soko hilo kutokuwa na huduma muhimu za kijamii na miundombinu huku wakiambulia kuahidiwa bila utekelezaji.





Aliongeza kuwa soko hilo jipya ni sawa na voda fasta kwani halikuwa na maandalizi yoyote kimiundombinu ikiwemo dampo kwa ajili ya taka zinazozalishwa sokoni hapo, choo, maji safi, pia hadi sasa hakuna ulinzi wa mali zao na wateja wao, ambapo pia alilalamikia swala la lango kuwa moja linalotagemewa kwa kutoka na kuingia sokoni hapo ambapo huhatarisha maisha ya wafanyabiashara hao pindi janga likitokea.





Akijibu tuhuma hizo afisa habari wa halmashauri ya jiji la Arusha, Ntagenjwa Hoseah alikanusha vikali ugawaji wa maeneo katika soko hilo kuhusishwa na maswala ya rushwa ambapo katika swala la miundombinu alisema kuwa halmashauri iko katika maboresho ya miundombinu ya soko hilo huku akisema kuwa kwa sasa wafanyabiashara hao wanatumia choo cha soko la krokon lililoko pembezoni mwa soko hilo jipya la NMC.







No comments:

Post a Comment