JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI
WA JAMII
UTANGULIZI
Kutokana na mgomo wa madaktari
uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi juni 2012.Wizara iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la madaktari
Tanganyika ili lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao .Idadi ya madaktari
wote waliogoma walikuwa 394, kati
yao madaktari 376 walikuwa ni madaktari
walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka hospitali za Muhimbili,
K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St.Francis - Ifakara, Dodoma, Temeke,
Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure. Aidha, Madaktari waajiriwa(Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo kutoka hospitali
ya Rufaa ya Mbeya.
Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki
kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.
Adhabu hizo zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo kali na kusimamishwa
udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile vile kuna
Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo
walifutiwa mashtaka.
MCHANGANUO WA ADHABU
- Waliofutiwa mashitaka madaktari 49
- Waliopewa onyo madaktari 223
- Waliopewa onyo kali madaktari 66
- Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
- Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria madaktari 4
- Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza madaktari 22
Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa
mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele
ya Baraza la Madaktari. Wizara pia imeridhia kuwapa Madaktari
waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya kuendelea na
mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla ya kuondolewa.
Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote waliopewa adhabu za
kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza kutumikia
adhabu zao.
HITIMISHO
Kwa taarifa hii madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa
onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha
kurejeshewa usajili na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo kwa vitendo.
Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar) wanatakiwa pia kuripoti kwa
Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa barua zao kulingana na Adhabu
walizopewa. Barua hizi zitatolewa kuanzia tarehe 2 Januari, 2013.Madaktari
wote walio katika mafunzo kwa vitendo wanatakiwa kuanza kazi katika
vituo vyao vya awali ifikapo tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda utakaoongezwa kwa
kipindi kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote waliopewa
adhabu wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo
ilivyotolewa.
Nsachris Mwamwaja
Msemaji
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
27/12/2012
No comments:
Post a Comment