Dk Willibrod Slaa
SIKU
moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtangaza Dk
Willibrod Slaa kuwa ndiye mgombea wa urais mwaka 2015 kwa tiketi ya
chama hicho, makada wa chama hicho wamegawanyika baadhi wakimponda na
wengine kumuunga mkono.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya makada wa chama hicho walisema
mwenyekiti wao amekosea kumtangaza mgombea kabla ya wakati, huku
wanaomuunga mkono wakisema hajakosea kwa sababu hatua hiyo itasaidia
kuondoa makundi ndani ya chama hicho.
Juzi,
Mbowe akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Karatu mkoani
Arusha, alisema Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa atapewa fursa
ya kuwania tena urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, huku mwenyewe
akijiweka kando kuwania nafasi hiyo
Hata
hivyo, Dk Slaa alipoulizwa iwapo ana nia ya kuwania nafasi hiyo
alihoji: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe,? Iwapo wanachama wa
Chadema watanipendekeza nitafikiria kufanya hivyo.” Mwasisi wa chama
hicho Edwin Mtei, Wajumbe wa Kamati Kuu; Profesa Mwesiga Baregu na Dk
Kitila Mkumbo, Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Bavicha
John Heche na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walitoa maoni
yanayopingana kuhusu kauli hiyo ya Mbowe.
Wanaounga mkono
Mtei alisema anaunga mkono kauli ya Mbowe akisema kiongozi huyo hajakosea kumtangaza Dk Slaa kuwania urais mwaka 2015.
“Ninaunga
mkono Dk Slaa kuwania tena nafasi ya urais mwaka 2015. Mwenyekiti
amemtangaza baada ya kupata baraka ya vikao vya chama,” alisema Mtei.
Ingawa
Mtei hakuwa tayari kusema ni kikao gani kilichopitisha jina la Dk Slaa
kuwania nafasi hiyo, alisisitiza: “Kuna vikao vya Kamati Kuu
vimefanyika hivi karibuni, vinaweza kuwa vimefanya uamuzi huo.
Mwenyekiti hawezi kuzungumza jambo bila baraka za vikao vya chama.”
Hata
hivyo, kauli hiyo ya Mtei inapingana na ile aliyoitoa Oktoba 6, mwaka
huu baada ya Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kutangaza
kutogombea tena ubunge badala yake kusema anataka kugombea urais katika
uchaguzi wa mwaka 2015.
Mtei alisema hatua ya Zitto kutangaza kuwania urais mapema kungesababisha mzozo na mpasuko ndani ya chama hicho.
Mtei
alisema amekuwa akimshauri Zitto mara kwa mara kuhusu hatua yake hiyo
akimtaka kuwaunganisha wana Chadema na siyo kuwagawa au kuwavuruga.
“Hakuna
shida kuonyesha hisia, lakini unatengeneza mzozo mkubwa sana ukitangaza
sasa. Mimi nimeshamshauri sana Zitto, ahakikishe anakiunganisha chama
na siyo kukigawa wala kukivuruga.”
Alisema
mbunge huyo kutangaza kutogombea tena ubunge na badala yake kujipanga
kuwania urais mwaka 2015 kumekuja mapema mno na kuonya kuwa itaibua
mzozo ndani ya Chadema.
Mtei
ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Fedha na Gavana wa Benki Kuu enzi za
utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, alisema kwamba wakati mwafaka
ukiwadia, Chadema kitaamua ni nani mwenye sifa za kugombea urais huku
akisema kina utaratibu wake wa kuwapata wagombea mbalimbali wa uongozi.
Hata
hivyo, Zitto jana alikataa kuzungumzia suala hilo akisema: “Nimesikia
hata mimi kwenye vyombo vya habari ila sina cha kuzungumza kuhusu hilo.”
Mwenyekiti
wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche alisema
kauli hiyo Mbowe siyo yake binafsi, bali ni ya wananchi.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment