Pages

Pages

Tuesday, February 19, 2013

LOWASSA APIGWA CHINI UVCCM

BARAZA Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), jana lilitangaza majina mapya ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, huku likiweka kando jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha baraza hilo kilichofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema nafasi ya Lowassa aliyekuwa Mwenyekiti kwa miaka 10, inachukuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi (pichani).

Shigella aliwataja wajumbe wengine walioteuliwa kuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar), Mohamed Abood, Waziri asiye na Wizara Maalumu Zanzibar, Machano Othman Said na Mbunge wa Kikwajuni Hamad Masauni.

Shigela alisema katika kuteua wajumbe hao, kikao hicho cha UVCCM kilizingatia uwezo wao katika ushawishi na kuwaunganisha vijana “bila ya kuwapo kwa makundi.” Hata hivyo, hakufafanua maana ya makundi hayo.

Kuondolewa kwa jina la Lowassa ni pigo jingine kwa mwanasiasa huyo ambaye amekuwa akitajwa kuwa miongoni mwa wanaotaka kuwania urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao. Jina lake pia halikupendekezwa miongoni mwa wagombea wa ujumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM katika uchaguzi uliofanyika wiki iliyopita.

Lowassa alikuwa ameanza kuibuka tena kisiasa kutokana na kambi yake kupata ushindi mkubwa katika mchakato wa chaguzi za ndani za chama hicho zilizowaingiza wafuasi wake wengi kwenye nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na katika jumuiya za chama hicho.

Wajumbe wengine walioachwa ni Nazir Karamagi, Dk Mary Nagu, Yusufu Ame Yusufu na Said Abuu.

Kwa upande wa Dk Nchimbi, nyota yake ya kisiasa inaonekana kung’ara kiasi cha kuanza kutajwa kuwa mmoja wa makada wa CCM wanaoweza kuteuliwa kumrithi Rais Jakaya Kikwete kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika uchaguzi huo wa Kamati Kuu ya CCM, Dk Nchimbi alichaguliwa kuwa mjumbe pamoja na wenzake sita kutoka Tanzania Bara, baada ya kupendekezwa na Rais Kikwete kuwania nafasi hiyo.

Itakumbukwa kwamba miaka 10 iliyopita, Dk Nchimbi katika kipindi chake cha pili cha Uenyekiti wa UVCCM, ndiye aliyependekeza jina la Lowassa kuwa mwenyekiti wa baraza hilo, mpango ambao ulipingwa na baadhi ya wanachama wakiongozwa na Nape Nnauye ambaye hivi sasa ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM.

Nape alifikia hatua ya kufukuzwa ndani ya jumuiya hiyo na hata alipotaka kukata rufaa alijibiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, wakati huo Yusuph Makamba kwamba asingeweza kurejeshwa katika jumuiya hiyo, hata kama angekata rufaa mbinguni.

Kikao hicho cha Baraza Kuu la UVCCM, pia kiliteua wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ambao ni Daud Njalu, Reuben Sixtus, Seki Kasuga, Amina Mkalipa na Mariamu Chaurembo ambao wanaingia kupitia Bara. Kwa upande wa Zanzibar waliopata nafasi hizo ni Shaka H Shaka, Bakari Vuai, Nadra Mohamed, Viwe Khamisi na Ali Nasoro.

chanzo :mwananchi

No comments:

Post a Comment