MAKADA watatu wa CCM mkoani Arusha wameendelea kumng’ang’ania Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema baada ya kuwasilisha Mahakama ya Rufani maombi ya marejeo ya hukumu iliyomrudisha bungeni mbunge huyo.
Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, 2012 kutokana na kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni Lema baada ya kushinda rufaa yake aliyokata mahakamani hapo akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Makada hao wa CCM hawakuridhika na hukumu hiyo na sasa wamewasilisha maombi mahakamani hapo, wakiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya hukumu hiyo huku wakianisha hoja kadhaa za kupinga hukumu hiyo.
Katika hukumu yake, iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu, Desemba 21, 2012, Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu ya Mahakama Kuu na ikamthibitisha rasmi Lema kuwa ni mbunge halali wa Arusha Mjini.
Katika hukumu hiyo iliyoandikwa na Jaji Bernard Luanda kwa niaba ya jopo la majaji wenzake wawili waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo, Mahakama ya Rufani ilisema kuwa warufani hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi dhidi ya Lema kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi.
“Rufaa imefanikiwa na tunatengua hukumu, tuzo na amri ya Mahakama Kuu.Tunamtangaza mrufani kuwa Mbunge wa Arusha Mjini,” ilisema Mahakama ya Rufani katika hukumu yake hiyo na kuwaamuru wajibu rufaa kulipa gharama za rufaa hiyo.
Hata hivyo, makada hao katika maombi yao hayo wanaliomba jopo la majaji hao lifanye marejeo ya hukumu yake hiyo ama mahakama kupitia kwa jopo jipya la majaji isikilize upya rufaa hiyo na kutoa uamuzi wa rufaa hiyo ya Lema.
Sambamba na rufaa hiyo, pia makada hao wa CCM wanaomba rufaa yao waliyokata pia wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu Arusha (Cross Appeal), ishughulikiwe haraka.
Katika maombi hayo, makada hao kupitia kwa wakili wao Alute Mughwai wanadai kuwa sababu zilitolewa na jopo hilo la majaji kuhusiana na haki yao ya kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi inapingana na uamuzi mwingine wa mahakama hiyo.
Wanabainisha mkinzano huo kuwa ni katika aina ya sheria ambayo inapaswa kutumika, ambayo ni ya Sheria za nchi za Jumuiya ya Madola na Sheria ya Uchaguzi ya Taifa, huku wakibainisha kuwa mkinzano huo katika suala moja unaharibu hadhi ya mahakama.
Pia wanadai mahakama ilikosea iliposema kuwa hapakuwa na ushahidi katika kumbukumbu za mahakama kuonyesha kuwa wao walikuwa ni wapigakura waliojiandikisha.
Wanaongeza kuwa pia mahakama hiyo ilikosea kusema kuwa haki ya mpigakura katika kupinga matokeo ya uchaguzi yana mpaka na kwamba ni kwa jambo ambalo linahusiana na uvunjwaji wa haki zao za kupiga kura tu.
Katika rufaa yake, Lema kupitia kwa mawakili wake, aliwasilisha hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, lakini katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufaa iliibua na kutolea uamuzi hoja mpya ambayo haikuwa imetolewa na upande wowote.
No comments:
Post a Comment