SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWA WATANZANIA,
TAREHE 31 DESEMBA, 2013.
Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Niruhusuni nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa
kutujalia uzima mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo ya kuuaga mwaka
2013 na kuukaribisha mwaka 2014. Wapo ndugu, jamaa na marafiki zetu
wengi ambao hawakupata bahati tuliyoipata sisi kwa vile wametangulia
mbele ya haki. Tuendelee kumwomba Mola wetu awape mapumziko mema na
azilaze roho zao mahali pema peponi. Ameen.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza
mwaka 2013 nchi yetu ikiwa salama na tulivu. Mipaka iko salama na ile
hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo kwa nyakati fulani mwaka huu sasa haipo
tena. Uhusiano wetu na majirani ni mzuri na tutaendelea kufanya kila
tuwezalo kuhakikisha kuwa hali inaendelea kuwa hivyo au hata kuwa bora
zaidi mwaka 2014 na daima dumu.
Hali ya usalama wa ndani ya nchi
nayo ni nzuri. Hali ya wasiwasi tuliyokuwa nayo mwaka wa jana na
mwanzoni mwa mwaka huu kuhusu uhusiano baina ya Wakristo na Waislamu
haipo. Ni matumaini yangu kuwa haitajirudia tena. Pepo mbaya amepita
tuombe atokomee kabisa.
Ndugu zangu;
Watanzania wenzangu;
Napenda
kurudia kuwasihi kuwa tuchague kuendelea kuishi pamoja kwa upendo,
umoja, kuvumiliana na kushirikiana. Tuepuke kugeuza tofauti zetu za
kisiasa, kidini, rangi, kabila au maeneo tutokayo kuwa chanzo cha uadui
na mifarakano. Kwa sasa tuna mwelekeo mzuri nawaomba tuudumishe. "Mjenga
nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni mwananchi". Tuchague kuijenga nchi
yetu badala ya kuibomoa. Tusiwasikilize watu hasidi wanaochochea uadui
na mifarakano miongoni mwetu. Watatuvurugia nchi yetu nzuri.(P.T)
Uhalifu
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 vyombo vya dola vikishirikiana na wananchi viliendelea
kupambana na vitendo vya uhalifu. Mafanikio ya kutia moyo yameendelea
kupatikana ingawaje bado kuna kazi kubwa ya kuendelea kufanya mwaka 2014
na miaka ijayo.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Kati ya
Januari na Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo 3 za cocaine na kilo
89,293 za bangi zimekamatwa na watuhumiwa 1,631 wametiwa mbaroni.
Tatizo la biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na mapambano
yanazidi kuwa makali. Mafanikio yanaendelea kupatikana ingawaje bado
tuna kazi kubwa na ngumu ya kufanya mbele yetu. Ni makusudio yetu
kuongeza maradufu nguvu ya kupambana dhidi ya uhalifu huu.
Tupo
hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalum cha Kupambana
na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia tutaitazama upya
sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa za kulevya ili
kuifanya iwe na meno makali zaidi. Vilevile, tutaongeza uwekezaji katika
vituo vya tiba na kuwarekebisha watu wanaotumia dawa za kulevya.
Mafanikio yanayopatikana Muhimbili na Mwananyamala yanatupa moyo wa
kufanya zaidi.
Ujambazi
Ndugu wananchi;
Jeshi la Polisi
limeendelea kupambana na ujambazi wa kutumia silaha na mafanikio
yameendelea kupatikana. Matukio ya ujambazi yemepungua mwaka 2013
ukilinganisha na mwaka 2012. Takwimu zifuatazo zinathibitisha ukweli
huo. Mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa yalikuwa 6,872 na kwa
mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409. Mwezi Julai mwaka huu, niliamua
kulihusisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika kupambana na
ujambazi wa kutumia silaha na utekaji wa magari katika Mikoa ya Geita,
Kagera na Kigoma. Katika Mikoa hiyo tatizo la ujambazi lilikuwa
limefikia kiasi cha kulazimisha watu kusindikizwa na Polisi kutoka Ngara
kwenda Karagwe, Biharamulo kwenda Muleba na kutoka Nyakanazi hadi
Kakonko. Hali hii haikubaliki na hatuwezi kuiacha iendelee.
Ndugu Wananchi;
Uamuzi
wangu huo ndiyo ulioanzisha Operesheni Kimbunga ambayo imekuwa na
mafanikio ya kutia moyo. Hali ya usalama katika Mikoa hiyo inaelekea
kuimarika ingawaje ni mapema mno kusema tatizo limedhibitiwa. Silaha
nyepesi na nzito zipatazo 650 zikiwemo za kijeshi na za kiraia pamoja na
mabomu ya kutupwa kwa mkono 11 zilikamatwa kwenye operesheni hiyo.
Aidha, watu 31,203 waliokuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria walirudi
makwao. Kati yao, watu 21,758 walirudi kwa hiari na 9,445 walirudishwa
wakati wa Operesheni.
Ndugu Wananchi;
Nimepata minong'ono kuwa
baadhi ya watu walioondoka wanarudi kinyemela. Napenda kuwatahadharisha
kuwa wasifanye hivyo. Wanajisumbua bure. Hawatadumu. Ushauri wangu kwao
ni kuwa kama wanapenda kuishi Tanzania wafuate njia halali za kufanya
hivyo.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu
tuliongeza nguvu katika kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji
haramu wa rasilimali za misitu. Hili ni tatizo la siku nyingi lakini
katika miaka ya hivi karibuni limekuwa kubwa mno na kuwazidi nguvu
Askari wa Wanyamapori na Maafisa Misitu.
Kwa nia ya kuwaongezea
nguvu, mwaka 2010 niliagiza Jeshi la Polisi lisaidie Idara ya
Wanyamapori na Idara ya Misitu katika kupambana na uhalifu huo.
Operesheni kadhaa ziliendeshwa maeneo mbalimbali nchini na mafanikio ya
kutia moyo yalipatikana. Lakini, kwa kutambua ukubwa wa tatizo na hasa
kwa upande wa aina ya silaha na mbinu zinazotumiwa na majangili niliamua
kuhusisha vyombo vingine vya usalama likiwemo Jeshi la Ulinzi. Nia ni
kuongeza nguvu ya mapambano. Ndipo ilipoanzishwa "OPERESHENI TOKOMEZA".
Ndugu Wananchi;
Kazi
nzuri imefanyika chini ya Operesheni hiyo. Mafanikio ya kuleta
matumaini yameweza kupatikana. Mitandao ya ujangili imeweza kutambulika
na wahusika wake kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo inahusisha watu
wa aina mbalimbali. Wamo raia wa kawaida, wapo watu maarufu, wapo
watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za
Wanyamapori na Misitu. Watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za
kijeshi 18, za kiraia1,579 na shehena kubwa za meno ya ndovu na nyara
nyingine navyo vilikamatwa.Watu kadhaa tayari wameshafikishwa
mahakamani.
Ndugu Wananchi;
Wahenga wamesema "kwenye wengi pana
mengi". Katika utekelezaji wa Operesheni hii kumekuwepo na taarifa za
kufanyika makosa kinyume na malengo na madhumuni ya Operesheni.
Niliagiza baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza, zoezi lisitishwe kwa
muda ili uchunguzi ufanyike, kasoro zitambuliwe na waliofanya makosa
wachukuliwe hatua zipasazo. Wakati kazi hiyo inafanyika suala hilo
lilijadiliwa Bungeni na Kamati Teule kuundwa. Matokeo yake sote
tunayajua. Mawaziri wanne wamewajibika kisiasa.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kuwapa pole Mawaziri wetu hao kwa matatizo
yaliyowakuta. Nawapongeza kwa uamuzi wa kukubali kuwajibika kwa makosa
yaliyofanywa na maofisa wa chini yao. Wameonesha ukomavu wa kisiasa na
kiuongozi wa hali ya juu na moyo wa uzalendo.
Kama mlivyosikia
nitaunda Kamisheni ya Uchunguzi itakayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu.
Uchunguzi wa kina utafanywa kuhusu kadhia yote hiyo. Makosa
yaliyofanyika yataainishwa na waliofanya kutambuliwa ili wachukuliwe
hatua zipasazo kwa mujibu wa sheria na kwa mujibu wa kanuni za utumishi
wa umma.
Ndugu Wananchi;
Ni muhimu kufanya hivi ili haki itendeke
ipasavyo. Mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa umma kubebwa na
viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya moja kwa moja,
siyo sahihi. Lazima kila mtu abebe mzigo wake inavyostahili. Ni
matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni kunapotokea matatizo ya
namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa waliohusika na kutenda
makosa wawajibishwe. Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani
huwaacha waharibifu waendelee na kazi isivyostahili. Mtindo huu
utawafanya watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa. Hata hivyo,
pale kwenye ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza
kuchukua hatua za kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi
huyo awajibike.
Ndugu Wananchi;
Tunakamilisha matayarisho ya
kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo
kwani tusipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.
Hali ni mbaya sana kwa upande wa uwindaji wa ndovu. Nilipolihutubia
Bunge tarehe 7 Novemba, 2013, nilieleza kuwa tutafanya sensa ya ndovu
katika Pori la Hifadhi la Selous. Sensa hiyo imekamilika lakini taarifa
yake inatisha. Kuna ndovu 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa109,419.
Tusipoendelea na Operesheni hii baada ya miaka michache ijayo hakutakuwa
na ndovu hata mmoja. Halikadhalika, zoezi la kuondoa mifugo katika
mapori ya hifadhi ya taifa litaendelea. Katika awamu ya pili ya
Operesheni hii, washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika
katika awamu ya kwanza.
Mchakato wa Kuunda Katiba
Ndugu wananchi;
Tumefika
mahala pazuri katika mchakato wetu wa kutayarisha Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jana Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa
Jaji Joseph Warioba, alitukabidhi Rasimu ya Pili ya Katiba, mimi na Rais
wa Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein. Kama nilivyosema jana
kinachofuata sasa ni kuitangaza Rasimu hiyo katika Gazeti la Serikali
kwa kila mtu na hasa Wajumbe wa Bunge la Katiba, kuiona na kuisoma.
Baada ya hapo kitafuata kitendo cha kuifikisha Rasimu kwenye Bunge
Maalum la Katiba kwa ajili ya kujadiliwa na hatimaye kupatikana Rasimu
ya Mwisho itakayofikishwa kwa wananchi kupigiwa kura.
Ndugu Wananchi;
Mchakato
wa kupata Wajumbe 201 watakaoungana na Wabunge na Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi kuunda Bunge Maalum la Katiba umeanza. Ni matarajio yetu
kuwa katika wiki ya tatu ya Januari, 2014, uteuzi utakamilika. Siku 21
baada ya hapo Bunge la Katiba litaanza. Hii ni kwa nia ya kuwapa nafasi
Wajumbe hao kusoma Rasimu ya Katiba. Baada ya Bunge la Katiba kumaliza
kazi yake, utaanza mchakato wa Kura ya Maoni itakayopigwa na wananchi
ndani ya siku 74 baada ya Rasimu ya Katiba kupitishwa na Bunge Maalum na
kukabidhiwa kwa Rais.
Iwapo Rasimu itakubaliwa na wananchi hapo
tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina
maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato
mwingine utakapoanzishwa na Katiba mpya kupatikana. Ni matumaini yangu
na, ni maombi yangu na rai yangu kuwa Rasimu hiyo itakubalika ili nchi
yetu isonge mbele.
Pongezi
Ndugu Wananchi;
Niruhusuni nitoe
pongezi zangu za dhati kwa Mwenyekiti na Wajumbe wote wa Tume kwa kazi
kubwa na nzuri waliyoifanya. Najua haikuwa kazi rahisi hata kidogo
lakini wameweza. Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi kwa ushiriki
wao mzuri uliowezesha zoezi la mabadiliko ya Katiba kufikia hatua
tuliyofikia sasa.
Ndugu Wananchi;
Ni matumaini yangu na ndiyo
matumaini ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
wataijadili Rasimu ya Katiba kwa makini na kufanya kila wawezalo
kuiwezesha nchi yetu kupata Katiba nzuri itakayoimarisha na kudumisha
Muungano wetu. Katiba itakayoendeleza umoja, upendo, udugu, mshikamano
na ushirikiano miongoni mwa wananchi wa Tanzania. Katiba
itakayoihakikishia nchi yetu amani, utulivu na ustawi wa kiuchumi na
kijamii.
Ni imani yangu na ya Watanzania wote kuwa Wajumbe wa Bunge
la Katiba wataweka mbele maslahi mapana ya taifa na watu wake. Wasiweke
mbele maslahi yao binafsi au ya vikundi vyao vya kisiasa au kijamii.
Wakifanya vinginevyo kuna hatari ya kupata Katiba isiyokidhi haja na
itakuwa hasara kubwa kwa taifa letu na kwao pia.
Uchumi
Ndugu wananchi;
Katika
mwaka tunaoumaliza leo, Tanzania iliendelea kupata mafanikio katika
nyanja mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Jambo la
kufurahisha ni kuwa mafanikio hayo yamepatikana licha ya kuwepo
changamoto kadhaa hapa nchini na hali ya uchumi wa dunia kuwa bado
haijatengemaa vya kutosha.
Pato la taifa limekua kwa asilimia 7.1
ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana. Tunategemea kuwa mwaka 2014
pato la taifa litakua kwa asilimia 7.3. Mfumuko wa bei umeshuka
kutokaasilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi asilimia 6.2, Novemba 2013.
Lengo letu ni kufikiaasilimia 5 mwezi Juni, 2014.
Ndugu Wananchi;
Hadi
Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye
thamani ya dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na dola
milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012. Kushuka kwa bei za
kahawa, pamba, katani, chai, karafuu na dhahabu ndiko kulisababisha
kupungua kwa mapato yetu ya fedha za kigeni. Hali hii inatukumbusha
umuhimu na uharaka wa kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani mazao na
bidhaa zetu tunazouza nje. Jambo hili tutalipa msukumo maalum mwaka 2014
na kuendelea.
Pamoja na kushuka kidogo kwa mapato ya mauzo yetu ya
nje akiba yetu ya fedha za kigeni iliendelea kuwa nzuri. Hadi Novemba
30, 2013 akiba yetu ilikuwa dola za Marekani 4,538 milioni. Hata hivyo,
akiba hiyo inatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje wa miezi 4.4 ni chini ya
lengo letu la miezi 4.5. Sina wasiwasi kuwa mwaka 2014 tutaliziba pengo
hilo.
Ndugu Wananachi;
Sekta zilizochangia sana katika kasi ya
ukuaji wa uchumi mwaka 2013 ni pamoja na mawasiliano asilimia 20.6,
huduma ya fedha asilimia 13.2, uzalishaji viwandani asilimia 8.2,madini
asilimia 7.8, ujenzi asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na uchukuzi
asilimia 7.1. Bado kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo ilikuwa ndogo kwani
ilikuwa asilimia 4.3.
Pamoja na hayo, kilimo kinaendelea kutoa
mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Tanzania na watu wake. Kilimo
kinachangia asilimia 24.7 ya pato la taifa na asilimia 10.7 ya mapato ya
fedha za kigeni. Kilimo kimeiwezesha nchi yetu kujitosheleza kwa
chakula na kuvipatia viwanda malighafi. Kwa upande wa mazao ya chakula,
kwa mfano, mwaka huu uzalishaji ulikuwa tani 14,383,845. Ukilinganisha
na mahitaji yetu ya chakula ya tani12,149,120 hivyo tunajitosheleza na
kuwa na ziada kidogo. Ziada hii ni kidogo mno hivyo inatulazimu mwaka
ujao tuongeze maradufu juhudi na uwekezaji katika kutekeleza shabaha na
malengo ya kilimo.
Ndugu Wananchi;
Kwa ajili ya uzalishaji wa
chakula kuwa mzuri, mwaka huu Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
wameweza kununua tani 233,689.8 za nafaka hadi kufikia Desemba 27, 2013
kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa miaka ya nyuma. Mwaka 2012 wakati kama
huu Wakala ilikuwa na kiasi cha tani 93,047.8 tu na kutulazimisha
kutafuta chakula nje ya nchi. Kwa ajili hiyo tulilazimika kuruhusu
wafanyabiashara kuagiza mahindi, mchele na sukari kutoka nje kwa nafuu
ya kodi. Uamuzi huo umesaidia nchi kuwa na chakula cha kutosha na kuuzwa
kwa bei nafuu kwa walaji.
Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu, na
ndiyo hasa dhamira yetu, kwamba mwaka 2014 tutapata mafanikio makubwa
zaidi kwa upande wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Naamini tutaweza
kwa vile tumejipanga vizuri. Tunayo miradi ya kimkakati iliyoainishwa
vizuri katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na chini ya Utaratibu
wa Matokeo Makubwa Sasa. Miradi hiyo kama itatekelezwa kama ilivyopangwa
uchumi utakua kwa kasi kubwa zaidi, ajira nyingi zitapatikana na huduma
za kiuchumi na kijamii zitaboreka sana.
Bahati nzuri tumeweka
utaratibu mpya na mzuri wa kufuatilia utekelezaji wa mipango, miradi na
shughuli za Serikali. Katika Ofisi ya Rais kumeanzishwa Ofisi maalum ya
ufuatiliaji ijulikanayo kama Presidential Delivery Bureau. Na, kila
Wizara ina kitengo cha namna hiyo kijulikanacho kama Ministerial
Delivery Unit. Kwa ajili hiyo utekelezaji wa miradi ya kimkakati na
shughuli za Serikali utakuwa mzuri zaidi.
Mazingira ya Uwekezaji
Ndugu Wananchi;
Ni
makusudio yetu kuwa kuanzia sasa tutaihusisha sekta binafsi kwa nguvu
zaidi katika utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo. Nimeagiza
Presidential Delivery Bureauishughulikie suala la uboreshaji wa
mazingira ya uwekezaji nchini. Sifa ya nchi yetu kuhusu mazingira ya
uwekezaji siyo nzuri. Kwa mujibu wa tathmini inayofanywa kila mwaka na
Benki ya Dunia, mwaka 2007 nchi yetu ilikuwa kati ya nchi 10 bora
duniani kwa kufanya mageuzi makubwa ya kupunguza gharama za kufanya
biashara. Mwaka huo tulikuwa nchi ya 142 kati ya nchi 175. Mwaka 2008
tukapanda na kuwa wa 130 kati ya nchi 176, mwaka 2012 tulikuwa wa 134
kati ya nchi 185 na sasa ni wa 145 kati ya nchi 185. Hali hii si nzuri
hata kidogo kwa uchumi unaokusudiwa kujengwa kwa kutegemea uwekezaji wa
sekta binafsi. Tunategemea PDB itatupa ushauri mzuri wa nini kifanyike
kurekebisha mambo.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa miradi ya Big
Result Now (BRN) katika kilimo, umeme, reli, barabara, bandari, maji,
elimu na kuongeza mapato ya Serikali umeanza kwa kasi inayoleta
matumaini. Kama upande wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali utakwenda
inavyotarajiwa tutegemee mambo mengi mazuri kufanyika kuanzia mwaka 2014
mpaka 2016.
Mpaka sasa hali ya ukusanyaji wa mapato ya Serikali si
mbaya. Wastani kwa mwezi unakaribia shilingi bilioni 700 kuelekea
shilingi bilioni 800. Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa miezi ya Julai
hadi Novemba yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,008.1 kipindi kama
hicho mwaka 2012 hadi shilingi bilioni 3,555.5 mwaka 2013. Hata hivyo
makusanyo ya Julai hadi Novemba, 2013 ni asilimia 88.1 ya lengo la
kukusanya shilingi bilioni 4,036.8. Lengo halijafikiwa kwa sababu ya
kuchelewa kutekelezwa kwa baadhi ya marekebisho ya mfumo wa kodi,
hususan tozo ya simcard, kodi za mishahara kutokana na kutokupandishwa
kwa kima cha chini katika sekta binafsi na ya uhawilisho wa fedha (money
transfer). Pia kuendelea kwa mvutano baina ya TRA na wafanyabiashara
kuhusu bei za mashine za kodi. Ni matumaini yangu matatizo hayo
yatashughulikiwa na kumalizwa mapema iwezekanavyo ili tuweze kupata
mafanikio makubwa zaidi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali mwaka
2014.
Elimu
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu tumeendelea
kupata mafanikio katika kupunguza tatizo la upungufu wa walimu wa shule
za msingi na sekondari. Mwaka huu tuliajiri walimu 28,666. Kwa ajili
hiyo upungufu wa walimu ni 57,755 kati yao 20,625 wa shule za msingi na
37,130 wa shule za Sekondari. Mapema mwaka ujao tutaajiri walimu wapya
36,100 kati yao 18,100 wa shule za msingi na 18,000 wa sekondari.
Kufanya hivyo kutafanya pengo lililopo liwe dogo zaidi.
Kwa upande
wa shule za sekondari, tatizo la walimu wa masomo ya sanaa tunakaribia
kulimaliza. Changamoto yetu kubwa itakuwa kwa walimu wa masomo ya
sayansi. Upungufu ni walimu 26,998 na uwezo wa vyuo vyetu ni kutoa
walimu wa sayansi 2,300 kwa mwaka. Mapema mwaka 2014 tutakutana na wadau
wa elimu nchini kujadiliana juu ya mkakati wa haraka wa kulikabili
tatizo hili. Nilipanga tufanye hivyo mwaka huu lakini mambo
yaliingiliana sana hatukuweza.
Ndugu Wananchi,
Tumeendelea
kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kujifunzia na
kufundishia. Tuliongeza fedha katika bajeti ya elimu kwa ajili ya
vitabu. Hivi sasa usambazaji wa vitabu vyenye thamani ya shilingi
bilioni 76 za bajeti ya mwaka 2012/13 unaendelea. Kwa sababu hiyo hivi
sasa upungufu wa vitabu umeshuka na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi
3. Naamini shilingi bilioni 49 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu
wa fedha kwa ajili ya vitabu itafanya mambo kuwa nafuu zaidi.
Tukiendelea kuwekeza kama tufanyavyo sasa shabaha yetu ya kila
mwanafunzi wa msingi na sekondari kuwa na kitabu chake kwa masomo yote
ifikapo 2016 itatimia.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeanza
utekelezaji wa mpango mkubwa wa kujenga nyumba za walimu. Kwa kuanzia
tumetenga shilingi milioni 500 kwa kila Halmashauri. Tumeanza na
Halmashauri 40,mwaka ujao na miaka inayofuata tutaongeza fedha
zinazotengwa na kuzifikia Halmashauri zote. Kwa upande wa ujenzi wa
maabara katika sekondari za kata napenda kuwakumbusha Wakuu wa Mikoa na
Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya na Miji, kuwa kila mmoja
ahakikishe kuwa ifikapo Novemba, 2014 malengo yanatimia. Wasisubiri
kuulizwa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Kwa kutambua umuhimu wa maji
kwa maisha ya wanadamu na uchumi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha
sekta ya maji imepewa upendeleo katika mgao wa fedha. Tutaendelea
kuongeza fedha katika bajeti mbili zinazofuata ili watu wengi zaidi
mijini na vijijini wapate maji safi na salama. Kama fedha zitapatikana
kama ilivyopangwa na utekelezaji ukasimamiwa vizuri tunatarajia kuwa
katika mwaka 2013/14 watu milioni 7.1 watapata maji. Katika mwaka ujao
wa fedha 2014/15 tumepanga kuwapatia maji watu wengine milioni 7 na
mwaka utaofuata (2015/16) tutaongeza tena huduma hiyo kwa watu milioni
1.3 na kufanya tufikie asilimia 74 ya Watanzania wanaopata maji safi na
salama ifikapo 2015/2016.
Afya
Ndugu wananchi;
Tumeendelea
kupata mafanikio katika kuendeleza upatikanaji wa huduma ya afya kwa
wananchi wa Tanzania. Zahanati, vituo vya afya na hospitali zimeendelea
kujengwa kote nchini. Aidha, hospitali za wilaya, mikoa, kanda na
Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuboreshwa. Kwa ajili hiyo
idadi ya Watanzania wanaoweza kupata huduma ya afya iliyo bora inazidi
kuongezeka. Hali kadhalika, wataalamu wa afya wa fani mbalimbali
wameongezeka na hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba imezidi
kuboreshwa. Pamoja na yote hayo bado kuna kazi kubwa ya kufanya mbele
yetu. Kufanya hayo ndiyo dhamira yetu kuu kwa mwaka 2014.
Ndugu wananchi;
Tumeendelea
kupata ushindi katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayoua watu wengi
nchini. Kwa upande wa malaria, kwa mfano, maambukizi ya ugonjwa huo kwa
watoto na mama wajawazito yamepungua kutoka asilimia 18 hadi 9.5.
Tutaendelea kugawa vyandarua kwa wajawazito na watoto kwa kutumia hati
punguzo pamoja na kusisitiza matumizi ya dawa mseto na kupulizia dawa ya
kuua mbu majumbani. Aidha, tunatarajia kupata mafanikio zaidi miaka
ijayo kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuua viluilui vya mbu
wanaoeneza malaria kitapoanza kazi.
Ndugu Wananchi;
Mambukizi ya
UKIMWI yameshuka hadi asilimia 5.1. Inaleta faraja kuona watu wengi
wamejitokeza kupima afya zao kwa hiari. Mpaka sasa watu milioni 18
wamepima. Tunao watu 1,298,402 walioorodheshwa kwa ajili ya kupata
huduma ya tiba na kati yao 485,715wanapata dawa. Waliosalia watapata
wakati wao ukifika.
Mpaka sasa vituo 4,603 vinavyotoa huduma ya
kuzuia maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
vimeanzishwa nchini kote tangu mpango huo uzinduliwe tarehe 1 Desemba,
2012. Idadi yake inaendelea kuongezeka. Ni dhamira yetu kuendeleza
jitihada za kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa Watanzania.
Mafanikio ya kampeni hii pamoja na ile dhidi ya malaria ndiyo chachu ya
mafanikio tuliyopata katika kupunguza vifo vya watoto nchini na kufikia
lengo la Milenia mwaka huu.
Magonjwa ya Moyo
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2013 tunaoumaliza leo, tumeshuhudia mambo kadhaa mazuri
yakifanyika yanayoelezea mafanikio tunayoendelea kuyapata katika
jitihada zetu za kujenga uwezo wa tiba kwa maradhi tunayopeleka wagonjwa
nje ya nchi. Niruhusuni niyataje baadhi yake. La kwanza, ni kuanza kazi
kwa Kituo cha Tiba na Mafunzo ya Magonjwa ya Moyo katika Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili. Hiki ni kituo kikubwa na cha aina yake cha matibabu
ya maradhi ya moyo hapa nchini. Huduma za kisasa za uchunguzi na
matibabu ya maradhi ya moyo ambazo zamani zilikuwa zinapatikana nje ya
nchi sasa zinaweza kupatikana hapa hapa nchini. Kwa kuwa na vitanda 100
vya kulaza wagonjwa, Watanzania wengi wataweza kuhudumiwa na maisha yao
kuokolewa.
Ndugu Wananchi;
Katika kituo hiki watu wanaweza
kufanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo (open heart surgery), uwekaji wa
mashine ya kuongezea nguvu kwenye moyo (pacemaker), uwekaji wa vyuma
vidogo katika mishipa ya damu ya moyo ambayo imebanana (stent). Tangu
kituo kianze kazi rasmi tarehe 30 Aprili, 2013 mpaka sasa watu 347
wamefanyiwa upasuaji wa moyo na watuwatatu wamewekewa pacemaker tangu
huduma hiyo ianze Novemba, 2013. Mapema mwakani kituo kinatarajiwa
kuanza huduma ya kuweka stent.
Kituo hiki ni kipya hivyo katika
mwaka 2014 tutaendelea kukijengea uwezo wa vifaa tiba, wataalamu na
mahitaji mengine muhimu ili kulipunguzia taifa mzigo wa kupeleka
wagonjwa nchi za nje. Serikali, pia itaendeleza ushirikiano wake na
uongozi wa Hospitali ya Kanda ya Bugando kuboresha huduma ya upasuaji
mkubwa wa moyo katika hospitali hiyo. Huduma hiyo ilizinduliwa tarehe 26
Oktoba, 2013 na Makamu wa Rais Mheshimiwa Daktari Mohamed Ghalib Bilal.
Saratani
Ndugu Wananchi:
Kwa
upande wa maradhi ya saratani, Februari, 2013 jengo jipya la kulaza
wagonjwa 170lilifunguliwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Kufunguliwa kwa jengo hilo kumeongeza uwezo wa taasisi yetu hiyo kulaza
wagonjwa 290 badala ya 120 tu kabla ya hapo. Ujenzi wa jengo hili jipya
umesaidia sana watu wengi zaidi kuhudumiwa na kupunguza msongamano
mkubwa wa wagonjwa uliokuwepo.
Figo
Ndugu Wananchi:
Kuhusu
maradhi ya figo mwaka huu pia tumeshuhudia huduma ya usafishaji wa figo
zenye matatizo ikipanuliwa. Huduma hiyo imeanzishwa tena katika
Hospitali ya Kanda ya Mbeya na imeanzishwa kwa mara ya kwanza katika
Chuo cha Tiba katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Pale Mbeya tayari wagonjwa
93 wamehudumiwa mwaka huu na kuwapa matumaini mapya ya maisha yao. Kwa
pale Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa kituo kikubwa kitakachobobea kwa
magonjwa ya figo unaendelea na unategemewa kukamilika mapema mwaka 2014.
Mafunzo
Ndugu Wananchi:
Katika
mwaka 2013 tumefungua ukurasa mpya katika jitihada zetu za kuongeza
wataalamu wa afya nchini. Chuo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha
Dodoma kimefanya mahafali yake ya kwanza ambapo wanafunzi 50 wa Shahada
ya Uuguzi walihitimu. Tunatarajia kuanza kupata madaktari kuanzia mwaka
2014.
Kwa upande wa mchakato wa kujenga
makazi mapya ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili
kule Mloganzila mchakato umeanza. Ujenzi wa miundombinu ya barabara,
maji na umeme unaendelea hivi sasa. Mwaka 2014 ujenzi wa Hospitali ya
kisasa ya kufundishia yenye vitanda 650 utaanza.
Ujenzi wa Mlonganzila ukikamilika Chuo
Kikuu cha Muhimbili kitaweza kuchukua wanafunzi 15,000 wa fani zote
ukilinganisha na 3,060 wa sasa. Hatua hiyo itaongeza sana uwezo na kasi
yetu ya kupunguza uhaba wa Madaktari, Wauguzi na wataalam wengine wa
afya.
Nyumba
Ndugu Wananchi:
Katika
mwaka 2013 ujenzi wa nyumba 35 za kuishi watumishi wa afya katika mikoa
ya Mtwara (5), Rukwa (20) na Singida (10) umekamilika. Ujenzi wa nyumba
100 unaendelea. Nyumba hizo ni sehemu ya mpango wa ujenzi wa nyumba 580
zinazojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Global Fund kwa awamu
mbili.
Awamu ya kwanza zinajengwa nyumba
310ambapo taasisi ya Benjamin William Mkapa Foundation ndiyo mtekelezaji
wa ujenzi huo. Napenda kutumia nafasi hii kutoa shukrani za dhati kwa
Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwa mchango wake mkubwa alioutoa
na anaoendelea kutoa kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Ujenzi wa Miundombinu
Ndugu wananchi:
Katika
mwaka 2013, tumeendelea kupata mafanikio makubwa katika kuboresha
miundombinu ya usafiri wa ardhini, majini na angani. Kasi ya ujenzi wa
barabara imeendelea kufanyika kote nchini. Kazi ya ujenzi ingekuwa nzuri
zaidi kama mtiririko wa malipo kwa Wakandarasi ungekuwa mzuri. Tatizo
hili tutalitafutia ufumbuzi mwaka 2014 ili kasi ya ujenzi wa barabara za
lami nchini iwe nzuri zaidi.
Pamoja na hayo mwaka huu kilomita
877 za barabara zimekamilika. Ujenzi wa daraja la Malagarasi nao
umekamilika kinachosubiriwa ni sherehe za uzinduzi. Ujenzi wa daraja la
Kilombero umeanza na ule wa daraja la Kigamboni unaendelea vizuri.
Tunatarajia kuwa mwakani tutaongeza
zaidi kasi ya ujenzi wa barabara zilizosalia ikiwa ni pamoja na kujenga
baadhi ya barabara kwa ubia na sekta binafsi. Kwa kasi na mwenendo
tunaoendelea nao sasa naamini ifikapo mwaka 2015 tutakuwa tumefikia
hatua ya juu sana katika shabaha yetu ya kuunganisha mikoa yote nchini
kwa barabara za lami.
Ndugu Wananchi:
Jitihada
za kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam
zimeendelea kutekelezwa. Barabara kadhaa zilipanuliwa na kazi
inaendelea. Ujenzi wa njia ya kupita mabasi yaendayo haraka umeendelea
kwa kasi ya kuridhisha. Mchakato wa ujenzi wa barabara za juu ya
nyingine katika njia panda za TAZARA na Ubungo umeshaanza. Mwaka ujao
huduma ya usafiri wa treni kusafirisha abiria Dar es Salaam itaongezwa
ili watu wengi zaidi wanufaike.
Ndugu wananchi:
Mwaka
huu, kwa upande wa reli ya kati, kazi ya kuboresha njia ya reli
imeendelea kufanyika na itaendelea mwaka 2014. Mwakani (2014) Shirika la
Reli litapokea injini mpya 13, mabehewa ya mizigo 274 na breki 34 hivyo
kuboresha sana huduma katika reli ya kati. Kuhusu ujenzi wa reli mpya
ya upana wa kimataifa ni matarajio yetu kuwa kama kila kitu kitaenda
sawa mchakato wa ujenzi utaanza katika nusu ya pili ya mwaka 2014.
Ndugu Wananchi:
Tumetoa
kipaumbele cha juu katika kuboresha huduma ya usafiri wa anga nchini.
Mwaka huu, tumeendelea na ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja vya
ndege vya Mikoa ya Kilimanjaro, Kigoma, Tabora, Mwanza, Arusha, Mtwara
na Kagera. Ni jambo la kufurahisha kuona Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Songwe ukianza kutumika. Hatimaye ndoto imetimia. Mwaka wa 2014 ujenzi
wa majengo mengine ya kuhudumia abiria, mizigo na ndege utaendelea
katika uwanja huo.
Pia ni furaha iliyoje kwamba upanuzi
wa Uwanja wa Ndege wa Mafia na ujenzi wa gati la Kilindoni
vimekamilika. Kero ya miaka mingi imepatiwa ufumbuzi. Kazi ya ujenzi wa
jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere itaanza rasmi mwaka 2014.
Nishati
Ndugu wananchi:
Dhamira
yetu ya kutaka Tanzania iwe na umeme wa uhakika na unaonufaisha watu
wengi imepata sura na mwelekeo mzuri mwaka huu 2013. Ujenzi wa bomba la
gesi kutoka Mtwara na Songosongo kuja Dar es Salaam umeanza na
utekelezaji unakwenda vizuri. Kama ujenzi wa bomba utakamilika kama
inavyotarajiwa na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme Kinyerezi utaenda
kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia lengo la
kuzalishamegawati 3,000 za umeme.
Ndugu Wananchi:
Bahati
nzuri mwaka huu, kufuatia kuongezewa fedha za bajeti, kasi ya usambazaji
umeme imekuwa nzuri. Tunaumaliza mwaka huku idadi ya Watanzania
waliounganishiwa umeme ikiwa imefikia asilimia 24 ukilinganisha na
asilimia 21 mwaka 2012 na asilimia 10 mwaka 2005. Haya si mafanikio
madogo. Kwa mwelekeo huu, kufikia lengo la asilimia 30 ya Watanzania
kupata umeme mwaka 2015 ni jambo la uhakika kabisa sasa. Tena kuna
uwezekano mkubwa wa kulivuka lengo hilo.
Ushirikiano wa Kanda
Watanzania Wenzangu:
Katika
mwaka 2013, nchi yetu imeendelea kushiriki vizuri katika shughuli za
Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC) ambazo sisi ni wanachama. Mwezi wa Agosti, 2013
tulikabidhi Uenyekiti wa chombo cha SADC kinachoshughulikia Siasa,
Ulinzi na Usalama kwa Namibia. Tulikuwa tumemaliza kipindi chetu cha
mwaka mmoja.
Katika kipindi chetu cha uongozi
tulishiriki kwa ukamilifu kutafuta suluhu kwa mizozo na migogoro ya
kisiasa na kiusalama nchini Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
na Madagascar. Tunafurahi kuona kwamba mambo katika nchi zote hizo sasa
yanakwenda vizuri.
Nchini Zimbabwe utulivu umerejea baada
ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi Julai, 2013. Nchi ya Madagascar nayo
imemaliza duru ya pili ya uchaguzi wa Rais kwa usalama. Matokeo
yanatarajiwa kutangazwa tarehe 7 Januari, 2014. Ni matumaini yetu kuwa
watu wa nchi hiyo watayapokea matokeo hayo na wataelekeza nguvu zao
katika kujenga umoja na maridhiano ili wajenge upya uchumi wa nchi yao.
Kwa upande wa Mashariki ya Kongo,
tishio kubwa la usalama kutokana na vitendo vya kundi la waasi la M23
limezimwa na Jeshi la Kongo kwa kushirikiana na Jeshi la Umoja wa
Mataifa. Kama mjuavyo Tanzania ni moja ya nchi zinazochangia maafisa na
askari wa Jeshi hilo.
Ndugu Wananchi:
Napenda
kutumia nafasi hii, kwa mara nyingine tena kutoa pongezi zangu za dhati
kwa wanajeshi wetu kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka waliyoifanya huko
Mashariki ya Kongo. Pia nawapongeza wanajeshi wetu walioko Darfur na
Lebanon kwa kazi yao njema waifanyayo. Wote nawaomba waendelee kudumisha
nidhamu na weledi, mambo yaliyowafanya wapewe sifa nyingi na
kuheshimiwa.
Wameiletea nchi yetu heshima kubwa.
Bahati mbaya, katika kutimiza wajibu wao huo wa kimataifa tumepoteza
vijana wetu 10, sabaDarfur na watatu Kongo. Narudia kutoa pole kwa Jeshi
letu na familia za marehemu kwa msiba mkubwa uliowakuta. Napenda
kuwahakikishia kuwa daima tutauthamini na kuuenzi mchango wao. Wanajeshi
wote tunawatakia heri na fanaka tele katika mwaka 2014.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi:
Mwaka
huu, ushiriki wetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki umepita katika
mtihani kidogo kufuatia ndugu zetu wa Uganda, Rwanda na Kenya kufanya
mambo ambayo yalijenga hisia ya kuwepo mifarakano. Pia yalileta hofu
kuwa hata uhai wa Jumuiya yenyewe ulikuwa mashakani. Katika mkutano
uliopita wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya uliofanyika tarehe 30
Novemba, 2013 mambo hayo tuliyazungumza kwa uwazi na kidugu. Tumeelewana
kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Ndugu Wananchi:
Katika
mkutano wa Kampala tuliamua mambo matatu makubwa na muhimu katika
kuendeleza agenda ya utangamano wa Afrika Mashariki. La kwanza,
tulikubaliana kuhusu Itifaki ya kuanzisha Umoja wa Fedha wa Afrika
Mashariki na kutia saini. Hii ndiyo hatua ya juu ya utangamano wa
kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tumekuwa tunashirikiana katika
kuwianisha sera za uchumi, fedha na bajeti, kwa uamuzi huu sasa
tunaelekea kwenye kuwa na sera moja ya fedha na bajeti kwa mambo hayo na
hatimaye sarafu moja. Baada ya hatua hii, inayofuata ni ile ya
utangamano wa kisiasa, yaani Shirikisho la Kisiasa. Katika mkutano wetu
wa Kampala tulikubaliana kuwa nchi wanachama ambazo hazijakamilisha
kutoa maoni yao, zifanye hivyo kisha baada ya hapo tuzungumzie jambo
hilo na kulipa mwelekeo.
Ndugu Wananchi:
Vilevile
katika kikao chetu cha Kampala, tuliridhia mpango wa utekelezaji wa
uamuzi wetu wa awali wa kuanzisha Himaya Moja ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Lengo la mfumo au utaratibu huu ni kufanikisha
utekelezaji wa malengo na madhumuni ya Umoja wa Forodha wa Afrika
Mashariki.
Utaratibu huu utarahisisha na
kuharakisha uingizaji na utoaji wa bidhaa katika bandari na mipaka ya
nchi za Afrika Mashariki. Pia, utaondoa vikwazo visivyokuwa vya kodi
katika uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kutoka nchi wanachama kwenda
nchi nyingine. Kwa jumla, Himaya Moja ya Forodha itasaidia biashara
kukua na hivyo uchumi wa nchi wanachama kukua na kuboresha ustawi wa
wananchi wa Afrika Mashariki.
Narudia kuwakumbusha wenzetu wa
Wizara ya Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha kutengeneza utaratibu
mzuri wa kuelimisha jamii kuhusu Umoja wa Fedha na Himaya Moja ya
Forodha. Nawataka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara
ya Afrika Mashariki, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Ujenzi, Wizara
ya Uchukuzi, Mamlaka ya Bandari, Mamlaka ya Mapato na Jeshi la Polisi,
kuhakikisha kuwa taratibu zote husika kuhusu Himaya Moja ya Forodha
zinakamilishwa mapema. Nia yangu na yetu sote ni kuona utekelezaji
unaanza mara moja. Hili ni jambo lenye maslahi makubwa kwa nchi yetu.
Medani za Kimataifa
Ndugu Wananchi:
Katika medani
za kimataifa, mwaka 2013 ulikuwa mzuri kwa Tanzania. Nyota ya nchi yetu
iliendelea kuangaza vizuri. Tumeendelea kuwa na uhusiano mwema na
mataifa yote duniani na hakuna nchi ambayo tuna uadui nayo. Pia tuna
uhusiano mzuri na mashirika ya kimataifa na kikanda yanayoshughulikia
masula ya siasa, fedha na maendeleo.
Vile vile, tuna uhusiano mzuri na watu
mashuhuri na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayoshughulikia
masuala ya maendeleo na ya kibinadamu.
Kwa sababu hiyo tumepata
misaada mingi ya maendeleo na ya kibinadamu iliyochangia katika
mafanikio tuliyoyapata katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii mwaka
2013.
Napenda kwa niaba yenu nitumie nafasi
hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa nchi, mashirika na watu
waliochangia katika maendeleo ya nchi yetu mwaka huu. Wakati
tukiwashukuru, napenda kuwakumbusha kuwa misaada yao bado tunaihitaji
mwaka ujao (2014) na miaka inayofuatia.
Ndugu Wananchi:
Kwa
upande wa wageni, mwaka huu ulikuwa wa baraka sana kwa Tanzania.
Tumepata heshima ya aina yake ya kutembelewa na Rais wa China,
Mheshimiwa Xi Jiping tarehe 24 – 25 Machi, 2013 na Rais wa Marekani
Mheshimiwa Barack Obama tarehe 01 - 02 Julai, 2013.
Pia tulitembelewa na Rais wa Sri Lanka
Mheshimiwa Mahinda Rajapaksa tarehe 26 – 27 Juni, 2013. Waziri Mkuu wa
Thailand, Mheshimiwa Yingluck Shinawatra tarehe 30 Julai mpaka Agosti 1,
2013 Pamoja na hao, tulipokea Wakuu wa Nchi na Serikali 19 waliokuja
kushiriki mkutano wa Smart Partnership Dialogue uliofanyika Dar es
Salaam tarehe 28 Juni, 2013.
Ndugu Wananchi:
Vilevile,
tulitembelewa na Marais Wastaafu wa Marekani, Mheshimiwa Bill Clinton
na Mheshimiwa George W. Bush. Nchi yetu inanufaika na misaada
inayotolewa na mashirika yao katika nyanja za afya na kilimo.
Napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru
wageni wetu wote hao kwa uamuzi wao wa kuja kututembelea. Wameipa nchi
yetu heshima kubwa. Ni matumaini yetu kuwa mwaka 2014 utaendelea kuwa wa
baraka kama huu tunaoumaliza leo. Pia nawashukuru sana Watanzania
wenzangu kwa kuwapokea vizuri wageni wetu. Wameondoka nchini wakiwa na
furaha kubwa na kumbukumbu nzuri kuhusu nchi yetu.
Licha ya kutembelewa, mimi na
viongozi wenzangu Wakuu wa Nchi yetu tulialikwa na kufanya ziara katika
nchi mbalimbali duniani. Pia tumeshirikishwa katika mikutano mbalimbali
ya kimataifa. Ziara hizo zimekuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu.
Ndugu Wananchi:
Katika
kikao cha Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kilichofanyia mwezi Januari,
2013 nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi za Afrika
ya kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi. Mwenyekiti wa
Kamati hiyo ndiye huwa mwakilishi na msemaji wa Bara la Afrika katika
majukwaa ya kimataifa ambapo masuala hayo yanazungumzwa au
kushughulikiwa.
Kwa ajili hiyo nilikwenda Warsaw,
Poland kuhudhuria Mkutano Mkuu wa 19 wa Mabadiliko ya Tabia Nchi
uliofanyika tarehe 11 – 22 Novemba, 2013. Katika mkutano huo
hatukufanikiwa vya kutosha. Hivi sasa matumaini yetu yapo katika mkutano
wa mwakani (2014) nchini Peru.
Iwapo tutafanikiwa tutakuwa tumejenga
msingi mzuri utakaowezesha Mkutano wa Paris mwaka 2015 kufanikiwa
kupatikana Mkataba wa Kimataifa unaozifanya nchi ziwajibike kisheria kwa
masuala yahusuyo kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Ikishindikana Peru na kama mataifa yataendelea kukaidi katika mkutano wa
Paris, hatma ya dunia yetu itakuwa mashakani kwani hali si nzuri hata
kidogo.
Ndugu Wananchi:
Mwaka huu
tunaoumaliza nchi za SADC tumepoteza mmoja wa viongozi wetu mashuhuri,
shujaa Nelson Mandela. Nilipata nafasi ya kuwawakilisha katika sala ya
kitaifa, kutoa heshima za mwisho na mazishi yake. Kule Qunu, nilipewa
nafasi ya kuzungumza ambayo niliitumia kuelezea uhusiano wetu na shujaa
Mandela, ANC na mchango wa Tanzania kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika.
Hotuba yetu ilipokelewa vizuri sana na
wenyeji kwani niliwaelezea baadhi ya mambo ambayo walikuwa hawayajui.
Watu wengi wa Afrika Kusini na duniani kwa jumla sasa wanaufahamu vizuri
mchango mkubwa wa nchi yetu kwa ukombozi wa Afrika Kusini. Tuendelee
kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema, peponi roho ya shujaa Nelson
Mandela.
Miaka 50 ya Mapinduzi na Muungano
Ndugu Wananchi:
Mwaka
ujao (2014) ni wa aina yake katika historia ya nchi yetu. Ni mwaka ambao
tunatimiza miaka 50 tangu Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari
12,1964 na miaka 50 ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika ziungane na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili
26, 1964. Ni mwaka wa kutambua na kusheherekea mafanikio tuliyoyapata.
Lakini, ni mwaka wa kuweka nadhiri ya kupata mafanikio makubwa zaidi
miaka 50 ijayo na kuendelea. Tutakiane heri katika kusheherekea siku
hizo adhimu.
Shukurani
Ndugu Wananchi:
Napenda
kuchukua nafasi hii adhimu kuwashukuru kwa dhati Makamu wa Rais,
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu,
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd.
Viongozi Wakuu wenzangu hao nawashukuru
kwa msaada mkubwa walionipa na wanaoendelea kunipa katika kuiongoza nchi
yetu mwaka 2013. Naomba tuendelee hivyo mwaka 2014 kwa maslahi ya nchi
yetu na watu wake.
Nawashukuru pia Mawaziri na
viongozi wengine wa Serikali zetu mbili kwa kazi nzuri waliyofanya ya
kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali za
Serikali. Kazi yao nzuri ndiyo iliyotupatia mafanikio tunaojivunia leo.
Naomba sote tutambue kuwa bado zipo mbele yetu kazi nyingi na changamoto
kubwa na nzito za kushughulikia katika jitihada zetu za kuwaletea
wananchi na nchi yetu maendeleo.
Tunao wajibu wa kudumisha umoja,
mshikamano, amani na utulivu wa nchi yetu. Hatuna budi kuendelea
kushirikiana na kusaidiana pamoja na kufanya kazi kwa bidii zaidi mwaka
ujao 2014 kwa niaba na kwa maslahi ya watu waliotuchagua.
Ndugu Wananchi:
Kwa namna
ya pekee nawashukuru sana Watanzania wote po pote pale walipo kwa
kuunga mkono juhudi za Serikali na kufanya kazi kwa bidii na maarifa
kujiletea maendeleo. Hali kadhalika nawapongeza kwa uelewa wenu
ulioiwezesha nchi yetu kuendelea kuwa kisiwa cha amani. Nawaomba
tuendelee na moyo huo wa kuipenda nchi yetu na kujitolea kwa ajili ya
utulivu wake na maendeleo yake na yetu sote.
Naomba pia nimalize kwa kuwashukuru
viongozi wetu wa dini wa madhehebu mbalimbali pamoja na waumini wao kwa
sala na maombi katika kipindi chote cha mwaka unaoisha leo.
Sala zao na maombi yao yametupa nguvu na
faraja katika vipindi vigumu ambavyo tumevipitia. Naomba muendelee
kuliombea taifa letu ili lipate baraka na neema ya Mwenyezi Mungu.
MWISHO.
Ndugu Wananchi;
Naomba
tuzidi kuombeana heri ili mwaka ujao uwe wa baraka na mafanikio makubwa
zaidi. Twendeni tukasherehekee mwaka mpya kwa amani na utulivu.
Nawatakia heri na fanaka tele katika mwaka mpya wa 2014.
Mungu Ibariki Tanzania,
Mungu Ibariki Afrika
chanzo: jumamtanda
No comments:
Post a Comment