MWANAMKE
mmoja mkazi wa Kimandolu jijini Arusha, Suzy Mrema (40) anayeishi na
virusi vya Ukimwi amedai kutengwa na ndugu zake, ikiwa ni pamoja na
kunyimwa urithi wa mali za marehemu baba yao kwa madai ya kuwa yeye ni
marehemu mtarajiwa.
Akizungumza
na gazeti hili, Suzy, mtoto wa kwanza kuzaliwa kwa marehemu Mzee Thomas
Mrema aliyeacha wake watatu, watoto 21 na mali zikiwemo nyumba kadhaa,
amekiri kuishi na virusi vya Ukimwi kwa muda mrefu.
Alisema
kwamba anasikitishwa na kitendo cha wadogo zake kumtenga na kugoma
kumgawia sehemu ya mali za marehemu baba yake, kwani tangu afariki dunia
miaka 10 iliyopita ndugu zake hao wamemtimua nyumbani, wakidai hana
faida yoyote katika familia yao na muda wowote anaweza kufa kutokana na
maradhi yanayomsibu.
“Kaka
yangu, mimi ni mwathirika wa Ukimwi na hata dawa ninazotumia hizi hapa
(anaonesha makopo matatu) ila hawa wadogo zangu wamekuwa wakininyanyapaa
kwa muda mrefu na kuniita marehemu mtarajiwa,” alisema na kuongeza;
“Hivi
sasa unavyoniona sina kazi maalumu ya kufanya nimekuwa nikibangaiza kwa
kuuza mboga na kufua nguo za watu majumbani ambao hunilipa ujira
kidogo, baba yangu ameacha mali nyingi sana ila wamejigawia wenyewe na
kunitenga mimi kwa kuwa ni mwathirika.”
Alisema
baba yake kabla ya kufariki alikuwa anaishi na wake watatu, akiwemo
mama yake mzazi ambaye yupo hai, alisema upande wa mama yake walizaliwa
watoto 10 na watoto watatu walifariki dunia na kubakia saba.
Alisema
wake wawili wa baba yake pia walifariki dunia na kuacha jumla ya watoto
14 na kati yao watoto wanne walifariki na kubaki 10 ambao hadi sasa
bado wapo hai, huku watoto wa kiume wakikataa kumgawia mali hizo na
kukataa hata kuuzwa kwa mali hizo ili wagawane fedha.
Alisisitiza
kuwa licha ya kulifikisha suala hilo katika ngazi mbalimbali, ikiwemo
ofisi ya mtendaji wa kata, kituo cha sheria na haki za binadamu na Mkuu
wa Wilaya ya Arusha, Raymond Mushi ambaye kwa sasa amehamishiwa Dar es
Salaam, hakupata ufumbuzi wa suala hilo.
Mwanamke
huyo ameiomba serikali, taasisi mbalimbali na mashirika yanayojihusisha
na haki ya mwanamke na mtoto, kumsaidia ili aweze kupata haki yake.
Kwa
upande wa mama yake mzazi, Rose Thomas Mrema alikiri kunyanyapaliwa kwa
mwanawe huyo na kusisitiza kuwa watoto wake wa kiume wakiwemo wa wake
wengine ndio wanashiriki kutumia ubabe kudhulumu wenzao na kujigawia
mali hizo wenyewe.
Alipoulizwa
kaka mkubwa wa Suzy, Severine Mrema alikiri wanandugu kutompa mgawo
dada yao, huku akisisitiza kuwa, kigezo si ugonjwa wake, bali ni kwa
sababu ameshaolewa na anaendesha maisha yake akiwa nje ya familia hiyo.
Kaka
huyo wa pili kuzaliwa katika familia ya Mrema, akizungumza kwa njia ya
simu kutoka Tanga anakoishi na kufanya biashara, alisema; “Kwa mila za
kiafrika, hawezi kupata mgawo wa mali kwa sababu ana mji wake.
Na
si yeye pekee, wako wengine kama watano, lakini kwa kuwa amekwenda
kudai haki katika vyombo vya sheria, tusubiri. Kama akifanikiwa atakuwa
amewasaidia na wengine.” Mali zinazodaiwa kuachwa na marehemu ni pamoja
na mashamba makubwa, nyumba karibu kumi, matrekta na biashara nyingine
mbalimbali.
na libeneke blog
No comments:
Post a Comment