Pages

Pages

Wednesday, April 30, 2014

TLP kutimua viongozi wake watatu wa wilaya

Na Bertha Mollel- Arusha

Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) Mkoani Arusha, kimewatimua viongozi wake watatu wa ngazi ya wilaya kwa madai ya kuvunja katiba ya chama pia  kushindwa kutekeleza majukumu yao badala yake wamekuwa wakiharibu hali ya hewa kila kukicha sambamba na kuwagonganisha viongozi wa mkoa wa chama hicho.

Timua timua hiyo imefanyika mapema jana kwenye mkutano mkuu wa kamati ya utendaji wa mkoa, ambapo waliwajadili viongozi hao wa wilaya akiwemo mwenyekiti wa TLP wilaya ya Arusha mjini na kuonekena kutokustahili kuendelea kuwa viongozi wa chama hicho badala yake warudi kama wananchama wa kawaida.
Viongozi hao walioenguliwa uongozi wa TLP wilaya ya Arusha mjini pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa TLP Michael Kivuyo ambae pia ni diwani wa kata ya Sokon One,  Salma Jumanne aliyekuwa katibu sambamba na Festo Kimaro aliyekuwa katibu mwenezi wa TLP wilaya.
Hata hivyo mkutano huo ulitumia fursa hiyo kuwachagua viongozi wa mda watakaokaimu nafasi hizo ambapo kwa upande wa nafasi ya mwenyekiti, itashikiliwa na Deo Mwakishi, na nafasi ya katibu itashikiliwa na Kinanzaro Mwanga huku nafasi ya Katibu mwenezi ikiwakilishwa na Deogratius Peter Silayo.

Wajumbe hao walisema kuwa wameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na viongozi hao kuwa sehemu ya kusababisha migogoro katika chama hicho sambamba na kudidimiza chama kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo hata kusimamisha wagombea kwenye nafasi mbalimbali za serikali zinapotangazwa hali ambayo inadhoofisha chama hicho.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho Deo Mwakishi alisema kuwa miongoni mwa matatizo yanayosababishwa na viongozi hao ni pamoja na kugonganisha viongozi wa juu wa chama hicho na viongozi wa mkoa ikiwemo ubadhirifu wa fedha za kodi ya pango la ofisi iliyopitia kwa aliyekuwa mwenyekiti wa wilaya Michael Kivuyo na kumpatia katibu wake Salma.
Alisema kuwa fedha za kulipia kodi ya pango walijichanga zaidi ya shilingi laki sita na kuongezewa na mwenyekiti wa chama hicho taifa mh,  Eliatonga Mrema lakini fedha hizo zilipowadia zilipotea katika mazingira ya kutatanisha mikononi mwa viongozi hao wa wilaya hali iliyopelekea kufungiwa ofisi na sasa hawana ofisi ya mkoa wala ya wilaya kutokana na kudaiwa kodi.
“mbali na hayo katiba ya chama imekuwa ikivunjwa hasa baada ya kumsingizia mwenyekiti wa mkoa Leonard Makanzo kuwa ameiba fedha za chama zaidi ya shilingi milioni 5 lakini wakashindwa kuthibitisha fedha hizo chanzo chake badala yake wanawashawishi wajumbe wa halmashauri kuu ya mkoa kumkataa mwenyekiti walipoaibika zaidi ni juhudi zao zilipogonga mwamba wakaamua kumwita mwenyekiti na kumtangazia kuwa wamemfukuza uongozi na wamemteua Deo Humay kama mwenyekiti wa mda hiyo sheria imetoka wapi”
Akizungumzia mkutano huo kwa waandishi wa habari mwenyekiti wa TLP mkoa wa Arusha Leonard Makanzo alisema kuwa mkutano huo pamoja na kujadili maswala na chama lakini pia kimewajadil viongozi wake wa wilaya na wajumbe kubaini chanzo cha migogoro ni wao hivyo wakawaondoa na kuwachagua wengine wa mda.
“Itakumbukwa kuwa hata hao tuliowaondoa akiwemo mwenyekiti wa wilaya Kivuyo hakuwahi kuchaguliwa bali walipewa nafasi hizo kwa mda kutokana na viongozi waliokuwepo kuhama chama aukukiuka katiba hivyo hata hao tuliowaweka kwa mda wameshindwa kuwakilisha nafasi zao kwa kutekeleza majukumu yao badala yake wamekuwa wakituharibia tu hali ya hewa lakini leo imefikia mwisho”
“Lakini mimi niseme tu kwamba hawa viongozi tuliowaondoa leo watabaki kama wanachama wa kawaida na wanaruhusiwa kugombea nafasi zozote za uongozi wa serikali na chama pindi nafasi zikitangazwa” alisema Makanzo.
Kuhusu swala la kutimuliwa ofisi kutokana na kudaiwa kodi na sasa wako wanarandaranda mtaani kwa kukosa mahala pa kuhudumia wanachama wao, mwenyekiti huyo alisema kuwa “ kwa sasa tunatafuta ofisi nyingine tutakayoweza kumudu gharama za kulipia hivyo baada ya tu ya mda mfupi tutakuwa na ofisi mpya tena nzuri zaidi”
Alitumia nafasi hiyo kuwataka wanachama wa TLP kuwa na imani na chama hicho kwani kinafanya mabadiliko hayo kuboresha chama hasa kwa kuwapata viongozi wazalendo watakaokisaidia chama kufika mbali ikiwemo kushika nafasi mbalimbali za uongozi kuwahudumia.
Kwa upande wake aliyekuwa mwenyekiti wa Chama hicho wilaya alipoongea na waandishi wa habari alisema kuwa yeye hana ugomvi na mtu kugombania cheo,
“Mimi sina taarifa halisi ya sababu ya wao kuniondoa oungozi lakini kama wameona ni sawa sina ugomvi nao bali nataka tu kujua sababu kiundani basi.

No comments:

Post a Comment