Na Nicodemus Jonas
TIMU
ya Simba imeonesha jeuri ya fedha na kuuhakikishia umma kuwa haitaki
mzaha msimu ujao, baada ya kumwaga kitita cha Sh milioni 42 kumnyakua
straika wa Mbeya City, Saady Kipanga.
Habari za kina kutoka kwa rafiki wa nyota huyo zinadai kuwa, Simba
imempatia kitita cha Sh milioni 30 ‘keshi’, kama njia ya kumshawishi
pamoja na kumuahidi mshahara wa Sh milioni moja kwa mwezi.
Mshahara
huo unamfanya Kipanga kukunja kibindoni Sh milioni 12 kwa mwaka, hesabu
inayoleta jumla ya Sh milioni 42 ukijumlisha fedha za ushawishi.
Mbali na hiyo, Simba tayari wanahaha kumtafutia nyumba kwani ni moja
ya masharti aliyowahi kuwapa viongozi wa Simba kama wanahitaji huduma
yake.
Lakini licha ya yote, bado nyota huyo wa zamani wa Rhino Rangers ya
Tabora, hajasaini rasmi mkataba, ingawa wamemalizana kila kitu.
“Jamaa ameishamalizana na Simba kwa kila kitu. Amepewa milioni
thelathini keshi na wamemwambia atakuwa akilipwa kiasi cha Sh milioni
moja kwa mwezi.
“Hata jamaa mwenyewe anasema asingeweza kuacha bahati hiyo. Zaidi ya
yote, kwa sasa Simba wanahaha kumtafutia nyumba ya kuishi maana aliwahi
kuwambia kuwa lazima ahakikishiwe malazi,” alisema mtoa taarifa wetu.
Simba imekuwa kwenye rada za kumnasa Kipanga tangu kumalizika kwa
ligi kuu msimu uliokwisha ambapo alikodiwa hadi ndege kutoka Mbeya kuja
Dar kwa ajili ya kuonana na Simba kuzungumzia suala la usajili wake.
No comments:
Post a Comment