Na Bertha Mollel --Arusha
TIMU ya AFC ya Arusha imepokea msaada wa vifaa vya michezo zikiwemo
jezi, mipira na viatu vyote vikiwa na thamani ya sh milioni 2.5 kutoka
Kampuni ya Tanzanite Forever ikiwa ni sehemu ya kuiwezesha kushiriki
ligi ya mabingwa wa mikoa itakayoanza Mei 10, mwaka huu jijini Mbeya.
Pamoja na vifaa hivyo, kampuni hiyo imebeba jukumu la kugharamia
nauli na mahitaji yote ya timu hiyo kwa muda wote itakayokuwa
ikishiriki ligi hiyo, ukiwa ni mkakati wa kuirejesha Ligi Kuu Tanzania
Bara baada ya kushuka daraja miaka minne iliyopita.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa
Tanzanite Forever, Faisal Shahbhai, alisema umefika wakati sasa kwa
wapenzi na wadau wa soka kujiunga pamoja kusapoti mpira wa Mkoa wa
Arusha na kuelekeza nguvu kubwa katika kuichangia kwa hali na mali AFC
ambayo ndiyo yenye wapenzi wengi mkoani hapa.
Shahbhai alisema kuwa, AFC inahitaji sapoti kubwa ili iweze
kushiriki ligi ya mabingwa wa mikoa na kushika nafasi ya kwanza na
kupanda Daraja la Kwanza, hatua moja kabla ya kurejea Ligi Kuu na kwa
sasa inahitaji fedha kwa ajili ya kulipa hoteli, posho za wachezaji na
chakula kipindi chote watakachokuwa Mbeya.
Aliongeza kuwa, wachezaji wa AFC wameonesha moyo wa kujituma na
kujitolea kuanzia Ligi ya Wilaya hadi Mkoa na sasa ni wakati wa wadau
na wahisani mbalimbali, kuisaidia ili iweze kuukomboa Mkoa wa Arusha
ambao hauna timu ya Ligi Kuu kwa sasa, baada ya Oljoro JKT iliyokuwa
ikishiriki ligi hiyo kwa miaka mitatu, kushuka daraja mwaka huu.
Akipokea vifaa hivyo, Katibu Mkuu wa AFC, Mike Warioba, alitoa rai
kwa wachezaji kuonyesha shukrani kwa kufanya vizuri katika ligi hiyo na
kusahau hali ngumu iliyokuwa ikiikabili na kubeba jina la timu hiyo
inayosifika na kuogopwa na timu nyingi kongwe hapa nchini.
No comments:
Post a Comment