Pages

Pages

Monday, May 5, 2014

UKAWA waitesa CCM


MIKUTANO miwili ya hadhara ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), iliyofanyika Unguja na Pemba visiwani Zanzibar, na ujumbe uliotolewa na viongozi wa umoja huo, umeitia kiwewe Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kimepanga kujibu mapigo.
Mbali ya kutaka kujibu mapigo, CCM pia inahaha kutumia vyombo vya dola na ofisi ya msajili kuusambaratisha umoja huo unaoonekana kuungwa mkono na wananchi wengi.
UKAWA inaundwa na vyama vinavyounga mkono rasimu ya katiba ya serikali tatu ambavyo ni Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR- Mageuzi, UDP na vyama vingine ambavyo wajumbe wake walisusia mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kutoridhishwa na namna Bunge hilo lilivyokuwa linaendeshwa.
Ujumbe unaoelezwa kuivuruga CCM kwenye mikutano hiyo ya UKAWA visiwani Pemba na Unguja, ni ule unaoeleza mkakati wa umoja huo kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais na katika ngazi nyingine za uwakilishi.
Duru za siasa zinasema kuwa tayari viongozi wa juu wa CCM wamepanga kuanza kufanya mikutano ya hadhara kujibu mapigo ya UKAWA, na pia kueleza umuhimu wa kuwa na serikali mbili na ubaya wa serikali tatu.
Habari zinasema kuwa CCM leo imepanga na tayari imeomba kibali kufanya mkutano wa hadhara visiwani Zanzibar, katika uwanja ule ule waliotumia UKAWA wa  Kiembesamaki.
Mkutano huo ambao unaelezwa kwamba utawashirikisha baadhi ya viongozi wa CCM kutoka Tanzania Bara, pamoja na mambo mengine utajibu kauli za UKAWA, hasa kuhusu serikali tatu, lakini pia kuelezea mkakati wao wa kutaka kuungana 2015.
“CCM leo wana mkutano hapa hapa Kiembesamaki walipofanyia UKAWA. Wamepanga kutoa ufafanuzi wa hoja za UKAWA ambazo kama zikiachwa, zinaweza kuleta athari kubwa kwa taifa,” alisema mmoja wa viongozi wa CCM Zanzibar.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye, alisema kuwa wamelazimika kwenda kujibu mapigo kwa madai kuwa UKAWA wameamua kupotosha umma na hawana nia njema na taifa.
Alisema UKAWA wamevunja sheria ya mabadiliko ya katiba ambayo inakataza kwenda kwa wananchi sasa wakati hakuna jambo lililokwishaamuliwa bungeni.
Duru za siasa toka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa moja ya njia hizo ni kutumia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuhoji uhalali wa UKAWA kubadilisha hoja ya mchakato wa katiba mpya na kuzungumzia harakati za kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais.
Alisisitiza kuwa watazunguka nchi nzima katika kila eneo ambalo UKAWA watapita ili kutoa ufafanuzi wa ajenda zao ambazo alidai zina nia ya kusaka madaraka.
Wakati CCM wakijipanga kwenda kujibu mapigo, upande mwingine chama hicho kinadaiwa kutumia vyombo vya dola na ofisi ya msajili kutaka kuusambaratisha umoja huo na kuzima mikutano yao Tanzania Bara.
Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, juzi alikaririwa na gazeti moja akionyesha kukerwa na jinsi UKAWA wanavyofanya mikutano ya hadhara kwa kutumia jina la umoja huo, huku wakijua fika kwamba sio chama cha siasa kilicho na usajili.
Jaji Mutungi katika taarifa hiyo, alisema mikutano ya hadhara iliyoombewa kibali Zanzibar ni ya CUF, lakini alieleza kushangazwa kwake, kwamba katika mikutano hiyo wazungumzaji walikuwa wakijitambulisha kwa jina la UKAWA na kusalimiana kwa jina la umoja huo.
Pia alihoji sababu za umoja huo kutumia UKAWA kisiasa kwa kutangaza kusimamisha mgombea mmoja wa urais mwakani badala ya kuzungumzia mchakato wa katiba na sababu zilizowatoa nje ya Bunge.
Habari zaidi zinasema kuwa kuna mpango wa vyombo vya dola kutumia kauli ya msajili kuzuia mikutano ya UKAWA Tanzania Bara kwa madai kuwa umoja huo umevunja sheria.
Habari za kiintelijensia zinasema kuwa polisi watazuia mikutano ya UKAWA kama itaombewa kibali cha umoja huo, lakini kama kibali hicho kitaombwa kupitia moja ya vyama vinavyounda UKAWA, jeshi hilo litalazimika kujiridhisha mkutano huo utakuwa wa chama husika na si vinginevyo.
Akizungumza na maelfu ya wananchi visiwani Pemba, Mwenyekiti wa UKAWA, Freeman Mbowe, alielezea nia ya umoja huo kutaka kusimamisha mgombea mmoja wa urais na katika nafasi nyingine za uwakilishi.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani Kongwe mjini Chakechake Pemba, juzi, Mbowe alisema UKAWA umeanzishwa kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya, lakini baada ya kuona faida yake, sasa wanakusudia kusimamisha mgombea mmoja kwenye uchaguzi mkuu mwakani.
“Je, wananchi wa Pemba mko tayari kuwa na mgombea mmoja kuanzia uwakilishi hadi rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?” alihoji Mbowe na kuitikiwa kwa kuungwa mkono na maelfu ya wananchi waliofurika kwenye uwanja huo.
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema nguvu ya pamoja na mshikamano walioukosa zamani, ilisababisha CCM kuwa  jeuri, hivyo hawawezi kurudia kosa hilo.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema wapinzani wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kujitenga kwani walikosa nguvu ya pamoja katika chaguzi zilizopita.

No comments:

Post a Comment