Jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu 30 wakazi wa Wilaya
ya Muleba kwa tuhuma za vurugu na uharibifu wa mali uliotokea wilayani
humo, ikiwemo kuvunja chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya
Kaigara na kuchoma nyumba moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, aliwaambia
waandishi wa habari jana kuwa chanzo cha uharibifu huo ni kifo cha Asera
Triphone (16) kilichotokea Juni 12, mwaka huu katika Hospitali ya Mount
Meru mkoani Arusha.
Alisema kuwa baada ya kufariki kwa mtoto huyo, mwajiri wake,
Valentina Maxmilian, alichukua jukumu la kusafirisha mwili wa marehemu
kwenda kwa wazazi wake wilayani Muleba kwa ajili ya mazishi.
Alisema wakati mwili unafikishwa nyumbani kwa baba wa marehemu,
Triphone Joseph, alikuwa na taarifa kuwa mwanae ameuawa kwa mateso,
ikiwa ni pamoja na kuondolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili, zikiwemo
sehemu za siri.
Alisema wazazi hao walitoa taarifa kituo cha polisi wakiomba mwili wa
marehemu upelekwe kituo cha afya cha Kaigara kwa ajili ya uchunguzi wa
kidaktari ombi lililopingwa na polisi ambao walitaka mwili huo
ukafanyiwe uchunguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.
Alisema kutokana na msimamo wa polisi, kundi la wananchi
lilihamasishwa na kuamua kubeba jeneza la marehemu kutoka Kijiji cha
Bukono na kulipeleka Muleba kisha kulitelekeza barabarani, lakini mwili
huo ulichukuliwa ukahifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha
kituo cha Kaigara ili kusubiri utaratibu wa kufanya uchunguzi.
Kwa mujibu wa kamanda, wazazi wa mtoto bado walikuwa wakishinikiza
uchunguzi wa kidaktari ufanyike kubaini chanzo cha kifo cha binti yao.
Alisema kabla ya utafiti huo kufanyika, wananchi wakaamua kuvunja
mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho ambapo polisi
waliingilia kati na kutumia nguvu kuwadhibiti.
Alisema wazazi wa marehemu walikubali kuchukua mwili wa mtoto wao kwa
ajili ya taratibu za mazishi huko kijijini kwao Bukono na kuwa tayari
wameshazika.
Aliongeza kuwa ilipofika usiku saa mbili, uhamasishaji uliendelea,
likatoka kundi la watu na kwenda nyumbani kwa Veronica Maxmilian, mama
wa mwajiri wa marehemu katika Kijiji cha Buyango, na kuchoma moto nyumba
mbili.
Alisema hatua za kisheria zimechukuliwa kwa kuwakamata waliohusika na
uvunjaji wa kituo cha afya, kutelekeza maiti barabarani na uchomaji wa
nyumba mbili za familia ya mwajiri wa msichana huyo.
Alisema watu 30 wanashikiliwa kwa lengo la kuwahoji ili kuwabaini
vinara wa vurugu hizo na kuwa ukamataji huo ulifanyika baada ya kupata
taarifa mbalimbali zilizolifikia jeshi hilo.
Hata hivyo, alisema mwajiri wa marehemu anashikiliwa na jeshi hilo
kwa ajili ya upelelezi wa kina ambao utafanyika hapa Kagera na mkoani
Arusha pamoja na jirani wanaomzunguka.
No comments:
Post a Comment