Pages

Pages

Tuesday, October 30, 2012

WATU TISA WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UJANGILI



Watuhumiwa wa ujangili wakiwa chini ya ulinzi na nyara walizokamatwa nazo eneo la Hifadhi ya Bonde la Yaeda Wilayani Mbulu mkoani Manyara juzi, ambapo nyara hizo zina thamani ya Sh3.2 milioni.

WATU tisa  wanaodaiwa kuwa majangili wamekamatwa na polisi, mkoani Manyara kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya short gun na  nyara za Serikali.
Wanadaiwa walikutwa na nyumbu watano na kanga watatu  wote wakiwa na thamani ya Sh3.2 milioni waliokuwa wamebebwa kwenye magari mawili.
Inadaiwa kuwa watu hao walikamatwa juzi kwenye pori la Hifadhi ya Bonde la Yaeda Chini, wilayani Mbulu  na mmoja wao alikuwa na sare  tatu  za  mavazi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).  
Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai mkoani Manyara, Benedict Msuya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa watu hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi uchunguzi wa tukio hilo utakapokamilika.

Msuya alisema watu hao walikamatwa baada ya raia wema kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mbulu (OCD), George Kyando ambaye alituma polisi waliowakamata watu hao wanaodaiwa kuwa ni majangili.
Alisema watuhumiwa ni pamoja na mkazi wa Geita mkoani Mwanza aliyekutwa na sare za JWTZ.
Mmoja niu mkazi wa  Shinyanga wakati wengine watatu ni wakazi wa Kijiji cha Dominiki mkoani Singida.
Msuya alisema kuwa watuhumiwa wengine wa tukio hilo ni  wakazi wa Mkoa wa Singida.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bunduki aina ya short gun na risasi zake tano yenye namba  Mark 1V, mapanga sita, visu vinne na tochi kubwa tatu, sufuria tano na madebe mawili ya unga wa mahindi.
Alisema pia waliyakamata magari mawili aina ya Land Rover. 
Naye,Ofisa Wanyamapori wa wilaya hiyo, Allan Shanny alisema magari hayo yalikuwa yamebeba wanyama pori waliouawa wakiwamo nyumbu watano na ndege watatu aina ya kanga wenye thamani ya Sh3.2 milioni.
Shanny alisema hali ya ujangili Bonde la Yaeda chini ni kubwa hususani kwa wanyama kama tembo wanaouawa kwa ajili ya kitoweo na pia uharibifu wa mazingira unafanywa na wawindaji haramu.

No comments:

Post a Comment