Pages

Pages

Tuesday, October 30, 2012

ZANZIBAR WALALAMIKIA UNYANYASAJI WA POLISI


BAADHI ya wananchi wa Zanzibar, wamelalamikia kile walichokielezea kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu, unaofanywa na polisi katika operesheni ya  kuwasaka wahalifu na watu wanaotuhumiwa kuchochea vurugu visiwani humu.
Operesheni hiyo inafuatia matukio ya  uvunjifu wa amani ulioambatana na uharibifu wa mali hasa baada madai ya kutoweka ghafla kwa Kiongozi wa Taasisi za Kiislamu, Sheikh Farid Hadi Ahmed,  Oktoba 16 mwaka huu.
Jana zaidi ya watu 50 walikutana na waandishi wa habari na kulalamikia  vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu katika operesheni ya kuwasaka watuhumiwa.
Kwa mujibu wa watu,  kijana mmoja aliyetambuliwa kuwa ni Hamad Ali Kaimu, amekufa  baada ya  kupigwa na askari wa vikosi vya usalama katika operesheni hiyo.
Miongoni mwa waliozungumza na waandishi ni, baba mzazi wa kijana huyo, Ali Kaimu mkazi wa eneo la Nyerere, ambaye alidai kuwa mtoto wake alipigwa hadi kufa akiwa mikononi mwa polisi na kwamba tukio hilo lilitokea Oktoba 27, mwaka huu.
Kaimu alisema kitendo hicho hakikubaliki na kwamba hatua lazima zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Baba huyo wa marehemu, alisema alimuona mtoto wake akiitwa na polisi wakati akienda kuchunga ng’ombe na kwamba baadaye askari walianza kumpiga kijana huyo akiwa mbele ya macho yake.
“Mwanangu aliniita baba njoo uchukue mzigo wangu na nikuonyeshe nilipomfunga ng’ombe wangu na nilipokwenda polisi na mie wakaniangushia kipigo kikali sana. Mwanangu alikuwa na Sh50,000 za kununulia godoro na alitaka kunipa lakini walikataa asinikabidhi” alisema baba huyo kwa huzuni.
Alisema kijana wake alikamatwa na siku ya Sikukuu ya Idd El Hajj na  wakati akichunga ng’ombe huko Magomeni.
Kaimu alisema siku ya pili alipigiwa simu akiitwa katika katika Kituo cha Polisi cha Madema na alipokwenda alitakiwa kwenda katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kuchukua  mwili wa mtoto wake.
“Walinipigia simu nikachukue maiti yangu na mimi nikagoma  kwa sababu wamemchukua mwanangu akiwa hai na nikawaambia munikabidhi mwanagu akiwa hai vipi watanipa mwanangu maiti,” alihoji mzee huyo.

No comments:

Post a Comment