Pages

Pages

Thursday, November 29, 2012

RAIS KIKWETE NA VIONGOZI WENZIE WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WAZINDUA BARABARA YA ARUSHA-NAMANGA-ATHI RIVER

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Kenya Jumatano Novemba 28, 2012 tayari kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa barabara ya Arusha-Namanga-Athi River pamoja na Mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utaozungumzia maendeleo ya miundombinu. 
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Kenya Jumatano Novemba 28, 2012 tayari kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa barabara ya Arusha-Namanga-Athi River pamoja na Mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utaozungumzia maendeleo ya miundombinu.Kulia ni Balozi wa Tanzania Nchini Kenya,Mh. Batilda – Salha Burhan.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kushoto) akiwa katika mazungumzo na Kiongozi wa Jumuiya ya Waislamu wa Ismailia Mtukufu Aga Khan (kushoto) katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi Kenya Jumatano Novemba 28, 2012.Rais Kikwete yupo nchini Kenya kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa barabara ya Arusha-Namanga-Athi River pamoja na Mkutano wa Wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utaozungumzia maendeleo ya miundombinu.Wengine Pichani ni Rais wa Kenya,Mh. Mwai Kibaki (katikati) na Rais wa Burundi,Mh. Nkurunzinzah.
Wakati wa Wimbo wa Taifa.
Baadhi ya mawaziri na makatibu wakuu wa Tanzania waliohudhuria sherehe za uzinduzi rasmi wa barabara ya Arusha – Namanga – Athi River yenye urefu wa kilometa 104.4 kwa upande wa Tanzania.
Baadhi ya Maafisa wa Jeshi la nchini Kenya wakiwa kwenye Sherehe hiyo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akihutubia kwenye sherehe za ufunguzi wa barabara ya Arusha-Namanga-Athi River
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzie wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakipata maelezo ya Barabara hiyo itakavyokuwa kutoka kwa Injinia.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipanda mti.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishiriki katika uzinduzi rasmi wa Barabara ya Arusha – Namanga – Athi River yenye urefu wa kilometa 104.4 kwa upande wa Tanzania.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzie wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakikata utepe kwa pamoja kuzindua rasmi wa Barabara ya Arusha – Namanga – Athi River yenye urefu wa kilometa 104.4 kwa upande wa Tanzania.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wenzie wa nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali waliofanikisha ujenzi wa barabara ya Arusha – Namanga – Athi River.PICHA NA IKULU

NDIKUMANA AWATEGA SIMBA SC

Ndikumana

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba SC, Suleiman Yamin Ndikumana kwa sasa ndiye anaongoza kwa kufunga mabao katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge inayoendelea mjini hapa.
Ndikumana aliyewahi pia kucheza Norway na Uturuki, jana alifunga bao la tatu katika mashindano haya, akiichezea Burundi dhidi ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars. 
Sasa anamzidi kwa bao moja, John Bocco ‘Adebayor’ wa Kilimanjafo Stars.
Jumla ya mabao 17 hadi sasa yamefungwa katika mechi 16 za makundi yote matatu, zilizopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
Bocco anafungana na mshambuliaji mwingine wa Burundi, Christopher Nduwarugira, wakati wachezaji wengine ambao hadi sasa kila mmoja amefunga bao moja ni Farid Mohamed, Yussuf Ndikumana wa Burundi, Mohamed Jabril wa Somalia kwa penalti, Geoffrey Kizito wa Uganda, Yonatal Kebede Teklemariam, Haruna NiyonzimUganda, David Ochieng, Clifton Miheso na Jean Mugiraneza.
Kwa sasa Bocco anayechezea Azam FC ya Dar es Salaam, ndiye mshambuliaji pekee kwenye kikosi cha Bara, baada ya washambuliaji wengine, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemomkrasia ya Kongo (DRC) kuzuiliwa na klabu yao.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
Suleiman Ndikumana   Burundi    3 (1 penalti)
John Bocco                  Tanzania  2
Chris Nduwarugira        Burundi   2
Yussuf Ndikumana       Burundi   1
Mohamed Jabril            Somalia   1(penalti).
Geoffrey Kizito              Uganda   1
Brian Umony                 Uganda   1
Yonatal Teklemariam     Ethiopia  1
Haruna Niyonzima         Rwanda  1
Jean Mugiraneza           Rwanda  1
David Ochieng               Kenya     1
Clifton Miheso                Kenya     1
Farid Mohamed              Sudan     1 

 .................xxx.............xxx.............xxx.................

KAZIMOTO, KAPOMBE HATARINI KUWAKOSA WASOMALI JUMAMOSI

Kazimoto
WACHEZAJI wawili wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, beki Shomary Kapombe na kiungo Mwinyi Kazimoto, walishindwa kumaliza mechi za jana, baada ya kuumia na sasa wako hatarini kuikosa mechi ya mwisho ya Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Somalia, Desemba 1.
Wachezaji hao wa klabu ya Simba, wote waliumia kipindi cha pili na kutolewa, nafasi ya Kapombe ikichukuliwa na Issa Rashid wa Mtibwa Sugar nay a Mwinyi ikichukuliwa na Shaaban Nditi wa Mtibwa pia.
Wote walitoka wakichechemea, kuashiria wamepata maumivu makali kidogo na Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark, Kim Poulsen alisema ataangalia hali zao leo na kesho.
Kim pia alisema kwamba sasa imetosha kuzungumzia suala la washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama watajiunga na timu hiyo au la.
“Kwangu sasa lazima ifikie wakati iwe inatosha, sitaki kuwazungumzia tena wachezaji hao, waulizeni TFF,”alisema Poulsen baada ya kuulizwa kama mawasiliano na klabu yao kama yanaendelea juu ya kuombea ruhusa.
Mazembe imekataa kuwaruhusu wachezaji hao kwa sababu michuano ya Challenge haimo kwenye kalenda ya FIFA.
Kutokana na kukosekana kwa washambuliaji hao, Stars sasa inabaki na mshambuliaji mmoja tu kikosini, John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, ambaye Watanzania wanatakiwa kumuombea dua asiumie ili aendelee kuibeba timu yao ya taifa.
                  .............xxx.................xxx................xxx................

JOHN BOCCO AGEUKA LULU KUJMPALA, WATU WAANZA KUFIKA BEI

John Bocco

Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
SOKA ya nguvu aliyoonyesha mshambuliaji wa Tanzania Bara, John Bocco ‘Adebayor’ katika mechi mbili za Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zimemfanya awe lulu katika mashindano haya yanayoendelea mjini hapa.
Mawakala mbalimbali waliopo mjini Kampala wameanza kuulizia uwezekano wa kumtafutia timu Ulaya mchezaji huyo wa Azam, lakini uongozi wa timu ya Bara, Kilimanjaro Stars mjini hapa umewataka wawasiliane na klabu yake, Azam FC ya Dar es Salaam moja kwa moja.
Lakini pia kuna uwezekano klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini, iliyomfanyia majaribio Agosti mwaka huu ikamfikiria tena mchezaji huyo kutokana na kiwango kikubwa alichoonyesha hadi sasa kwenye mashindano haya.
Japokuwa hakufunga bao juzi kwenye mechi na Burundi, lakini kazi aliyoifanya wengi walikubali yeye ni mshambuliaji mzuri haswa kutokana na mfumo wa sasa wa kocha wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen kumtumia peke yake mbele.  
Bocco ana mabao mawili kwa sasa, wakati mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Suleiman Yamin Ndikumana ndiye anayeongoza kwa mabao katika michuano hii.
Ndikumana aliyewahi pia kucheza Norway na Uturuki, juzi alifunga bao la tatu katika mashindano haya, akiichezea Burundi dhidi ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars. 
Jumla ya mabao 25 hadi sasa yamefungwa katika mechi 18 za makundi yote matatu, zilizopigwa kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
Bocco anafungana na mshambuliaji mwingine wa Burundi, Christopher Nduwarugira na mchezaji mwenzake wa Azam, Khamis Mcha ‘Vialli’ wakati wachezaji wengine ambao hadi sasa kila mmoja amefunga bao moja ni Farid Mohamed, Yussuf Ndikumana wa Burundi, Mohamed Jabril wa Somalia kwa penalti, Geoffrey Kizito wa Uganda, Yonatal Kebede Teklemariam, Haruna NiyonzimUganda, David Ochieng, Clifton Miheso na Jean Mugiraneza, Dadi Birori, Chiukepo Msowoya, Miciam Mhone, Patrick Masanjala, Amir Hamad Omary na Yosief Ghide.
WAFUNGAJI CECAFA TUSKER CHALLENGE 2012
Suleiman Ndikumana    Burundi    3 (1 penalti)
John Bocco                   Tanzania  2
Khamis Mcha                Zanzibar   2
Chris Nduwarugira        Burundi    2 
Yussuf Ndikumana        Burundi    1
Mohamed Jabril            Somalia    1(penalti).
Geoffrey Kizito              Uganda    1
Brian Umony                 Uganda    1
Yonatal Teklemariam    Ethiopia    1
Haruna Niyonzima        Rwanda    1
Jean Mugiraneza          Rwanda    1
Dadi Birori                    Rwanda    1
David Ochieng             Kenya       1
Clifton Miheso              Kenya       1
Farid Mohamed            Sudan      1
Chiukepo Msowoya      Malawi      1
Miciam Mhone              Malawi      1
Patrick Masanjala         Malawi      1
Amir Hamad Omary      Eritrea      1
Yosief Ghide                Eritrea       1(penalti).  

KUNDI A LAMALIZA BIASHARA LEO TUSKER CHALLENGE

Shangwe hizi zitaendelea kwa Uganda leo?
Na Mahmoud Zubeiry, Kampala
MECHI za Kundi A, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge zinatarajiwa kufikia tamati leo kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole mjini hapa.
Wenyeji na mabingwa watetezi, Uganda The Cranes wanatarajiwa kumaliza na Sudan Kusini, mchezo ambao utaanza saa 12:00 jioni, kabla ya hapo, kuanzia saa 10:00 jioni, Kenya Harambee Stars wataonyeshana kazi na Ethiopia.
Uganda wanaongoza Kundi A kwa pointi zao sita, wakifuatiwa na Ethiopia na Kenya, ambao kila mmoja ana pointi tatu. Sudan Kusini hawana pointi hata moja.
Ikumbukwe timu mbili za juu kutoka kila kundi, A, B na C zitafuzu moja kwa moja Robo Fainali, wakati kutoka makundi yote matatu, watatafutwa washindi wa tatu bora wawili, kukamilisha idadi ya timu za kucheza Nane Bora.
Kwa sababu hiyo, pamoja na kwamba Sudan Kusini wamepoteza mechi zote mbili za mwanzo, bado wanaweza kupigana kiume japo kugombea kupenya kama miongoni mwa washindi wa tatu bora.  
Kenya na Ethiopia bila shaka patachimbika leo- kwani timu zote zimefungwa na Uganda na zote zimeifunga Sudan Kusini- sasa leo itakuwa siku ya kujua nani nafuu kati yao.
Mechi nyingine za kukamilisha hatua ya makundi ya michuano hii, zitachezwa zote kesho za Kundi B na C.
MSIMAMO KUNDI A:
                      P   W  D   L    GF GA GD Pts
Uganda          2    2    0    0    2    0    2    6
Kenya            2    1    0    1    2    1    1    3
Ethiopia         2    1    0    1    1    1    0    3
Sudan Kusini 2    0    0    2    0    3    -3  0
MSIMAMO KUNDI B:
                     P   W  D   L    GF GA GD Pts
Burundi         2    2    0    0    6    1    5    6
Tanzania       2    1    0    1    2    1    1    3
Sudan           2    1    0    1    1    2    -1  3
Somalia         2    0    0    2    1    6    -5  0
MSIMAMO KUNDI C:
                     P   W  D   L    GF GA GD Pts
Zanzibar        2    1    1    0    2    1    1    4
Rwanda         2    1    0    1    3    2    1    3
Malawi           2    1    0    1    3    4    -1  3
Eritrea           2    0    1    1    2    3    -1  1
MECHI ZILIZOSALIA:
RATIBA KUNDI B:
Desemba 1, 2012:
Sudan v Burundi             (Saa 10:00 jioni)
Somalia v Tanzania        (Saa 10:00 jioni)
RATIBA KUNDI C:
Desemba 1, 2012:
Malawi v Zanzibar          (Saa 10:00 jioni)
Eritrea v Rwanda            (Saa 10:00 jioni)
VIWANGO VYA UBORA FIFA
NCHI                 NAFASI
Uganda             86
Malawi              101
Ethiopia            102
Sudan               102
Rwanda             122
Burundi             128
Kenya                130
Tanzania           134
Zanzibar            134
Somalia             193
Eritrea               192
Sudan Kusini    200
(Viwango hivi vimetoka mwezi huu)

Wednesday, November 28, 2012

MAMIA WAMZIKA MSANII SHARO MILIONEA LEO MUHEZA MKOANI TANGA

 Mwili wa Marehemu Sharo Milionea ukiswaliwa mapema mchana huu kabla ya kupelekwa kwenye nyumba yake ya milele
Sehemu Kubwa ya Umati wa watu ulikishiriki mazishi
Rafiki mkubwa wa marehemu Sharo Milionea,Mzee Majuto akiwa ameshikwa mkono na Msanii wa filamu JB wakielekea kwenye mazishi mapema mchana huu,Muheza mkoani Tanga.Picha Kwa Hisani Ya Ahmed Michuzi

RIPOTI YA NCHI MASIKINI SANA DUNIANI MWAKA 2012 UKWELI WA MAMBO YENYEWE MPAKA TARAKIMU HUU HAPA


Nov
Ripoti ya Nchi Maskini Sana Duniani ya Mwaka 20121, yenye kichwa kidogo cha habari Kutumia Fedha Zinazotumwa na Raia Wanaoishi Nga’ambo na Weledi Wao Kujenga Uwezo wa Uzalishaji, imetolewa jana
--

Mwelekeo wa uhamiaji
-Idadi ya watu ambao wamehamia Ulaya kutoka Nchi Maskini Sana (LDCs) iliongezeka kutoka milioni 19 mwaka 2000 kufikia milioni 27 mwaka 2010. Hii ni sawa na 3.3% ya wakazi wote wa nchi hizo.
-Nchi Maskini Sana Duniani zinatoa 13% ya wahamiaji duniani kote---idadi ambayo inalingana na mgawo wa LDCs katika idadi ya wakazi wote duniani (12.1%).
-Wahamiaji wanne kati ya watano kutoka LDCs wanaishi kwenye nchi zinazoendelea (Kusini) na mmoja tu kati wa watano ndiye anaishi kwenye nchi zilizoendelea (Kaskazini).
Utumaji fedha
-Kiwango cha fedha zinazotumwa na raia waliohamia ng’ambo kwenda kwenye nchi zao kiliongezeka mara nane kati ya mwaka 1990 na 2011: Kutoka dola bilioni 3.5 kufikia dola bilioni 27. Tangu mwaka 2008 kiasi cha fedha kimeendelea kuongezeka pamoja na kuwepo na anguko la kiuchumi duniani.
-Mwaka 2011 kiasi cha fedha zilizotumwa kwenda nchini Tanzania kutoka Uingereza zilikuwa dola milioni 4.5, kutoka Canada dola milioni 3.2 na kutoka Kenya dola milioni 2.5.
-Mwaka 2011, fedha zilizotumwa kwenda LDCs zilikuwa kama mara mbili ya thamani ya uwekezaji wa moja kwa moja (FDI) katika nchi hizi (dola milioni 15), na kiwango hiki kilizidiwa tu na Misaada Rasmi Kutoka Nje, yaani ODA (dola bilioni 42 mwaka 2010), kama chanzo cha fedha kutoka nje ya nchi.
-Kiwango cha fedha zinazotumwa kutoka nje kama kingegawanywa kwa mwananchi mmoja mmoja kiliongezeka kutoka dola 10 kama kila mtu angepokea hadi dola 30 kati ya mwaka 2000 na 2010.
-Fedha zinazotumwa na raia wanaoishi nje zina umuhimu wa pekee kwa LDCs ikilinganishwa na nchi zilizo katika makundi mengine. Katika LDCs, fedha zinazotumwa na raia kutoka nje zinachangia 4.4% kwenye pato la nchi na 15% ya thamani ya bidhaa zinazouzwa nje. Kiwango hiki ni kikubwa kwa mara tatu ikilinganishwa na nchi nyingine zinazoendelea (ambazo siyo LDCs).
-Kuanzia mwaka 2008 hadi 2010, kiasi cha fedha kilichotumwa kutoka nga’mbo kinalingana na zaidi ya moja ya tano ya pato la taifa la nchi za Lesotho, Samoa, Haiti na Nepal.
-Tangu mwaka 2009 hadi 2011, nchi za Nepal na Haiti zilipata fedha nyingi za nje kutoka kwa raia wao walio ng’ambo kuliko zile ambazo nchi hizi zilipata kutokana na mauzo ya bidhaa nje.
-Kwa LDCs tisa, kiwango cha fedha zinazotumwa na raia wanaoishi nje kilizidi kile cha uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) na misaada rasmi kutoka nje (ODA) kati ya mwaka 2008 na 2010. Hizi ni nchi za Bangladesh, Haiti, Lesotho, Nepal, Samoa, Senegal, Sudan, Togo na Yemen. Kwenye nchi nyingine nane za kundi la LDCs, katika kipindi hicho hicho, fedha zinazotumwa na raia kutoka ng’ambo zilizidi FDI: Benin, Burundi, Comoros, Ethiopia, Gambia, Guinea-Bissau, Kiribati na Uganda.
-Theluthi mbili ya fedha zinazotumwa na raia kutoka ng’ambo kwenda kwenye LDCs zinatoka kwenye nchi zinazoendelea.
-Duniani kote, gharama ya kutuma fedha zinafikia 9% ya kiwango cha fedha kilichotumwa; kwa LDCs gharama ni kubwa zaidi kwa theluthi moja (12%).
-Kama nchi zilizo kusini kwa Jangwa la Sahara zingelipia gharama za uhamishaji fedha kwa wastani wa gharama inayolipwa duniani kote, mapato yao yangekuwa yaliongezeka kwa dola bilioni 6 mwaka 2010.
-Asilimia 66 ya fedha zilizohamishwa kwenda kwenye LDCs kati ya mwaka 2009 na 2011 ni za nchi tatu tu: Bangladesh, Nepal na Sudan.
-Matumizi ya simu za mkono kwenye LDCs ni makubwa zaidi (368 kwa kila wakazi 1,000) kuliko idadi ya akaunti za benki (171 kwa wakazi 1,000). Simu za mkono zinaweza vile vile kutumika katika kuhamisha na kupokea fedha kutoka ng’ambo.
Kuhama kwa utaalam
-Mtu mmoja kati ya kila watu watatu wenye ujuzi mkubwa (mwenye elimu ya chuo kikuu) kutoka LDCs anaishi ng’ambo. Kwenye nchi zilizoendelea kiwango ni mtu mmoja katika kila watu 25.
-LDCs sita zina raia wao wataalaum wengi zaidi wanaoishi nje ya nchi kuliko wale waliobakia nchini mwao: Haiti, Samoa, Gambia, Tuvalu na Sierra Leone.
-Theluthi mbili ya wahamiaji wenye ujuzi mkubwa kutoka LDCs wanaishi kwenye nchi zilizoendelea; theluthi moja wanaishi katika nchi zinazoendelea.
-Kiwango cha kuhama kwa watu wenye ujuzi kwenda ng’ambo ni kikubwa (20% ) kwa LDCs nyingi (30 kati ya 48).
-Wahamiaji kutoka LDCs wenye elimu ya chuo kikuu ambao wanaishi na kufanya kazi ng’ambo inafikia milioni 2.
-Idadi ya Watanzania waliohamia Uingereza kwa kumbukumbu za mwaka 2000 ni 10,535.
-Aina ya wahamiaji inafuata ukubwa wa kipato wa nchi mwenyeji. Katika nchi zilizoendelea, 35% ya wahamiaji ni wale wenye elimu ya chuo kikuu; kwenye LDCs 4% tu ya wahamiaji wana kiwango hicho cha elimu. Viwango hivi ni kwa wahamiaji kutoka nchi zote, japo viwango ni hivi hivi kwa wahamiaji kutoka nchi za kundi la LDCs.
-Theluthi moja ya wahamiaji kutoka LDCs ambao wana elimu ya chuo kikuu wanaishi Marekani.
Uwezo wa kiuchumi (Uchumi mpana)
-Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa mwaka kwa LDCs tangu kipindi cha msukosuko wa kiuchumi duniani (2009-2011) ni 4.7%, ambacho ni chini ya kiwango cha kipindi cha miaka ya ukuaji mkubwa wa kiuchumi (2003-2008), yaani 7.9%. Hii ina maana kwamba kiwango cha ukuaji wa kipato kwa mwaka kwa kila mkazi kilishuka kutoka 5.4% miaka ya ukuaji mzuri wa uchumi hadi kufikia 2.4%.
-Wastani wa ukuaji halisi wa pato la nchi katika LDCs mwaka 2011, yaani 4.2%, ulikuwa chini ya 4.9% ya mwaka 2009 wakati wa anguko la uchumi duniani.
-Kile kinachojulikana kama Gross fixed capital formation kwenye LDCs kilipanda kidogo kutoka 20.7% ya pato la jumla la taifa mwaka katika miaka ya 2005-2007 kufikia 21.6% miaka ya 2008-2010. Hata hivyo, bado kilibaki chini ya viwango vya nchi nyingine zinazoendelea, ambazo zilifikia kiwango cha 30.1%.
-LDCs zinaendelea kutegemea sana raslimali kutoka nje. Pengo la pato linalotokana na uagizaji bidhaa na uuzaji bidhaa nje lilikuwa kubwa kwa 20% ya pato la jumla la taifa katika nchi tano za kundi la LDCs mwaka 2011, wakati LDCs nyingine 13 pengo lilikuwa asilimia 10 ya pato la jumla la taifa.
-Kiwango cha utegemezi wa rasilimali kutoka nje katika kulipia uwekezaji wa ndani ya nchi kati ya mwaka 2008 na 2010 kilikuwa 15% ya pato la jumla la taifa kwa LDCs ambazo hazisafirishi mafuta nje.
-Asilimia 62 ya mauzo ya bidhaa nje kutoka LDCs 48 yalikuwa ni kutoka nchi tano tu: Angola, Bangladesh, Equatorial Guinea, Yemen na Sudan. Ukiacha Bangladesh, nchi zote hizi zinauza mafuta nje.
-Mapato ya LDC kwa mauzo ya bidhaa nje yanategemea zaidi mauzo ya bidhaa moja (mafuta), ambayo yanaingiza 46% ya jumla ya mapato yote yanayotokana na mauzo ya bidhaa nje.
-Zaidi ya nusu ya mauzo ya nje kutoka LDCs (54%) yalikuwa yanakwenda kwenye nchi zinazoendelea mwaka 2011, mwelekeo unaothibitisha umuhimu wa biashara ya kusini-kusini. China ndiyo iliyonunua bidhaa nyingi zaidi kutoka LDCs (26.4%) ikiwazidi Jumuia ya Ulaya (20.4%) na Marekani (19%).
ZIKO WAPI NCHI MASKINI SANA DUNIANI?
Umoja wa Mataifa unaziweka nchi 48 kwenye kundi la Nchi Maskini Sana Duniani (LDCs). Mgawanyo wao ni kama ifuatavyo.
Africa (33): Angola, Benin, Burkina Faso, Burundi, Central African Republic, Chad, Comoros, Jamhuri ya KIdemnokrasia ya Kongo(DRC), Djibouti, Equatorial Guinea, Eritrea, Ethiopia, Gambia, Guinea, Guinea-Bissau, Lesotho, Liberia, Madagascar, Malawi, Mali, Mauritania, Msumbiji, Niger, Rwanda, Sao Tome na Principe, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudan, Togo, Uganda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia;
Asia (9): Afghanistan, Bangladesh, Bhutan, Cambodia, Lao, Myanmar, Nepal, Timor-Leste na Yemen;
Caribbean (1): Haiti;
Pacific (5): Kiribati, Samoa, Solomon Islands, Tuvalu na Vanuatu.
Mchoro 1 – Nchi 48 za kundi la LDCs
Imetolewa na UNCTAD
--
Kutengeneza list ya LDCs
List ya LDCs inapitiwa upya kila baada ya miaka mitatu na Baraza la Uchumi na Jamii (ECOSOC) la Umoja wa Mataifa, kufuatana na mapendekezo ya kamati ya Sera ya Maendeleo (CDP).
Katika mapitio ya hivi karibuni, Machi 2012, CDP ilitumia vigezo vifuatavyo:
1. Kigezo cha pato la kila mtu, kwa kufuata Pato la Jumla la Nchi (GNI) kwa kila kichwa (wastani wa miaka mitatu)
2. Kigezo cha raslimali watu ambacho kinatumia viashiria kama lishe, afya, kuandikishwa shuleni na kujua kusoma na kuandika
3. Kigezo cha mazingira hatarishi ya kiuchumi. Ambacho kinatumia viashiria kama mishtuko ya kiasili, mishtuko ya kibiashara, udogo na umbali.
Nchi tatu tu zimefanikiwa kupanda daraja kutoka list ya nchi za kundi la LDCs: Botswana Desemba 1994, Cape Verde Desemba 2007 na Maldivs Januari 2011. Samoa inategemewa kupanda daraja tarehe 1 Januari 2014.
ECOSOC ilipitisha pendekezo la CDP kuipandisha daraja Equatiorial Guiones mwezi Julai mwaka 2009 na mwezi Julai 2012 ikakubali pendekezo la CDP kuipandisha Vanuatu. Hata hivyo ruhusa ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa bado itahitajika ili kuzipandisha daraja nchi hizi mbili.

HOJA ZOTE ZA AKINA HAMAD RASHIDIZATUPILIWA MBALI



 Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) Julius Mtatiro
Hamad Rashid 
--
Hukumu imemalizika muda so mrefu hapa mahakama kuu.

Hoja zote za akina Hamad Rashid zimetupiliwa mbali.

Mahakama imejiridhisha kwamba, amri ya mahakama kuu ya kusitisha kikao cha BARAZA KUU kilichowafukuza uanachama HR na wenzake wanne haikufikishwa kwa chama kwa hivyo kikao husika kilikuwa halali.

Hii ina maana kwamba OMBI la Hamad Rashid na mawakili wake kuwa WAJUMBE WOTE WA BARAZA KUU la CUF wafungwe jela kwa kukiuka amri ya mahakama limetupiliwa mbali.

Kesi ya msingi ambayo HR na wenzake waliifungua kupinga uhalali wa KAMATI YA MAADILI YA CHAMA itasikilizwa tarehe 28/01/2013 ambapo mawakili wa chama watapangiwa tarehe YA kuleta hoja za kutaka kesi ya msingi ifutwe kwa kuwa taratibu zote zilifuatwa na walifukuzwa kihalali na kwa kuzingatia katiba ya chama.

Chama chetu kimefurahishwa na uamuzi huu kwani unaonesha namna ambavyo hatukukurupuka.

Chama pia kinatoa pole kwa mhe. Hamad Rashid kwa kufiwa na mkewe mdogo jana, tutashiriki katika kutoa pole na mazishi pia. Tunaamini haya ya kimahakama yana nafasi yake na ya kibinadamu hayakwepeki.
Na
 Naibu Katibu Mkuu wa CUF(Bara) 
Julius Mtatiro

Kutoka Ofisi za Bunge:Rais Jakaya Kikwete Azindua Rasmi Ukumbi Mpya Wa Bunge la Afrika Jijini Arusha Leo

 
Spika wa Bunge la Africa Mashariki Mhe. Margret Natongo Zziwa (kulia) akimkaribisha Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda katika jengo hilo leo.
 Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda akimpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati alipokuwa akiwasili katika jengo jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha kwa lengo la kuzindua Ukumbi wa Bunge la Afrika Mashariki ulioko katika jengo hilo.
 Spika wa Bunge Afrika Mashariki,Mhe. Margret Natongo Zziwa akimkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (kushoto) ili kulihutubia Bunge la Afrika Mashariki.Kulia ni Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Anne Makinda.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete akilihutubia Bunge la Afrika Mashariki wakati alipofika kuzindua Ukumbi Mpya wa Bunge la Afrika Mashariki ulioko katika jengo jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki Jijini Arusha.
 Baadhi ya Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Jengo jipya la Jumuiya ya Afrika Mashariki.Picha na Prosper Minja- Bunge.

Tuesday, November 27, 2012

Mwili wa hayati Yasser Arafat wafukuliwa

 
Hayati Yasser Arafat
Mwili wa kiongozi wa zamani wa Palestina, Yasser Arafat, umefukuliwa kutoka kaburi lake liloko ukingo wa Magharibi mjini Rammala ili kuwawezesha kuufanyia uchunguzi kubaini iwapo aliuwawa kwa sumu.
Bwana Arafat alifariki dunia mwaka 2004 nchini Ufaransa baada ya kuugua kwa kipindi kifupi.
Maradhi yaliyopelekea kifo chake hayakubainika. Uamuzi wa kuufukua mwili wa Yasser Arafat katika kaburi lake lililoko ukingo wa Magharibi unafuatia makala ya televisheni iliyodai kupata mabaki ya madini ya kitonoradi aina ya Polonium kwenye nguo zake.
Wapalestina wengi wanashuku kwamba huenda Israel ilihusika katika kifo cha kiongozi huyo. Israel imekuwa ikikanusha shutuma hizo.
Uchunguzi wa mauaji dhidi ya Bwana Arafat umeanzishwa nchini ufaransa kufuatia ombi lililowasilishwa na mjane wake.
...............xxx........xxx.......xxx.....

Katu hatuondoki Goma'' wasema M23


Waasi wa M23 wamewalazimisha watu kutoroka mji wa Goma
Kiongozi wa waasi wa M23 ambao wiki jana waliuteka mji wa Goma Mashariki mwa DRC, wanasema katu hawataondoka Goma hadi serikali itakapotimiza matakwa yao.
Kiongozi wa kundi hilo, Jean-Marie Runiga alisema kuwa wapiganaji wake wataondoka mara moja ikiwa Rais Joseph Kabila, ataitikia matakwa yao ambayo ni pamoja na kuivunja tume ya uchaguzi.
Serikali ya Congo hata hivyo imepuuza matakwa hayo kama ya kipuuzi.
Uganda ambayo imekuwa ikipatanisha pande hizo mbili kwenye mkutano mjini Kampala, awali ilisema walikubali kuondoka Goma bila vikwazo.
Mnamo Jumamosi, serikali za nchi za Maziwa makuu ziliwapatia waasi hao makataa ya siku mbili kuondoka Goma.

JB aahidi kufanya shoo ya kufa mtu kesho Arusha

JB Mpiana akizungumza mna Waandishi Dar es Salaam leo
Na Prince Akbar
MWANAMUZIKI nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana aliyetua jijini Dar es Salaam juzi kwa maonyesho kadhaa, likiwamo la uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band inayokwenda kwa jina la Risasi Kidole, itayofanyika Ijumaa katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam.
Kabla ya shoo hiyo ya Ijumaa, JB Mpiana ambaye amekuja na kundi lake zima la Wenge Musica BCBG, likiwahusisha wanamuziki wake za zamani na wapya, atauwasha moto jijini Arusha kesho kabla ya kufanya kweli jijini Mwanza Jumapili.
Akizungumza katika Hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, Dar es Salaam, JB Mpiana ameahidi kutoa shoo ya aina yake ambayo anaamini itakonga nyoyo za Watanzania.
Alisema kuwa amefurahisa sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, ikiwa ni pamoja na mapokezi aliyoyapata, akiahidi kutoa burudani ya nguvu kwa Watanzania kuwalipa mapokezi waliyomwonesha.
 “Nina imani waandaaji wamefanya maandalizi ya kutosha, nimekuja na wanamuziki wangu wote 25, nimekuja na vifaa vyangu vyote vilivyopo katika kundi langu, ili kutoa burudani ya kutosha kwa Watanzania.
 “Nimewaletea albamu inayojulikana kwa jina la Biloko (chakula), watanzania wajiandae kula, yaani kupata burudani ya nguvu kutoka kwangu na kundi langu,” alisema JB Mpiana.
Kati ya wasanii aliokuja nao, alisema wapo wale wa zamani aliokuwa nao enzi hizo ndani ya kundi lake hilo lilipoanza kutamba katika anga ya muziki, na wengine wapya ambao wapo fiti.
Katika programu yake hapa nchini, amesema atapiga nyimbo zake za zamani na mpya ili kuwapa watanzania fursa ya kupata vionjo vya zamani na vipya, kuweza kupima ubora wa kazi hizo.
Akizungumzia muziki wa Tanzania, amewataka wasanii wa hapa nchini kujituma na kuzipenda kazi zao na kuiheshimu waweze kufanikiwa katika kazi zao hizo.
Juu ya kiongozi wa safu ya unenguaji, alisema safari hii inaongozwa na mwanadada Zambrota, ikiwa ni baada ya kufariki kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Monica.
 “Nimefurahi sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, wapenzi wa burudani wajiandae kupata shoo ya nguvu kutoka kwa JB Mpiana,” alisema mkali huyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya QS Muhonda, Joseph Muhonda, waratibu wa maonesho hayo, amesema kuwa ni matarajio yao wakazi wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza, watafurahia shoo hiyo kutoka kwa JB Mpiana na Mashujaa kutokana na maandalizi ya nguvu waliyofanya, akiwataka wakazi wa maeneo hayo, kujitokeza kwa wingi.
Alisema kuwa katoka onesho la JB Mpiana jijini Arusha, atatumbuiza katika ukumbi wa Triple A kuanzia saa tatu usiku, wakati Desemba Mosi atakuwa katika ukumbi wa Villa Park kuanzia saa tatu usiku.
 “Maandalizi yote yapo sawa, kila kitu kimekamilika, tuliahidi JB Mpiana anakuja na kweli amekuja kama mlivyomuona,” alisema na kuongeza kuwa JB Mpiana atasindikizwa na wasanii wa Bongo Fleva kama H Baba, MB Doggy, Ney wa Mitego na wengineo.