MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema amesema
baadhi ya maofisa wa usalama wa Taifa hawana uzalendo na nchi kwani rasilimali
na maliasili zinaporwa huku wenyewe
wakishindwa kuchukua hatua yoyote.
Lema aliyasema hayo juzi mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kwenye mkutano wa vuguvugu la mabadiliko
(M4C) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari na James Ole
Millya.
Alisema haoni umuhimu wa watumishi hao wa
idara hiyo nyeti ya usalama wa Taifa ambayo inategemewa na nchi,lakini mali
hizo zinaporwa huku watu hao hawachukui hatua ya kukomesha vitendo hivyo vya
uporaji.
Alisema idara hiyo hivi sasa haina watu wa
adilifu kwani wengi wao wamebaki kunywa pombe kali na kuwa wambeya na kusahau
wajibu wao wa kujali maslahi ya Taifa ambapo jamii inategemea.
“Hivi sasa hawa watu wamebaki kunywa viroba na
kuwa wambea hata hapa kwenye mkutano wapo wananirekodi lakini mimi sina hofu
yoyote kwani nazungumza kwa uchungu wa uporwaji wa rasilimali zetu,” alisema
Lema.
Alitoa mfano kwa uwanja wa ndege wa kimataifa
wa Kia ambapo mtu akipita na kitu kidogo hata shilingi 100 kuna kengele inalia
kuashiria tatizo lakini imewezekana Twiga akapitishwa kwenye ndege na usalama
wa Taifa wapo.
“Kuna faida gani kuwa na watu kama hawa kwani
wameshindwa kuzuia wizi na uporaji wa rasilimali zetu hadi nchi nyingine
zinakamata mali zetu zikiwa zimeshaondoka kwenye ardhi ya nchi yetu,” alisema
Lema.
Alisema kuwa rasilimali na maliasili kama
Twiga,nyati,mamba na viboko wanachukuliwa na kusafirishwa kwenda nchi za nje
huku idara hiyo inaangalia bila kuchukua hatua yoyote ya kudhibiti hali hiyo.
Naye,Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la
vijana la Chadema (Bavicha),John Heche aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuamka
kutoka usingizi kwani wamelala,hadi wanakubali rasilimali yao ya madini ya
Tanzanite yanaporwa.
Heche alisema kwa muda wote wakazi wa
wilaya ya Simanjiro wamekuwa wakiichagua CCM ili hali kuna madini ya Tanzanite
ambayo yana thamani kubwa lakini hayawasaidii chochote,kwani wakazi hao wapo
kwenye lindi la umasikini.
“Wacheni kucheka katika hili sisi Chadema
tunaendelea kuwaelimisha na ninyi kwa ninyi mnapaswa kuamshana ili muda wa
uchaguzi ukifika muwaondoe madarakani na kuweka chama ambapo kitajali maslahi
yenu,”alisema Heche.
Naye,Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki
Joshua Nassari alisema anashangazwa na mji mdogo wa Mirerani kuwa na madini ya
Tanzanite yanayopatikana sehemu hiyo peke yake duniani lakini hakuna maendeleo.
“Mvua imenyesha kwa muda wa nusu saa,lakini
barabara zenu zimejaa maji na sisi tumepita kwa shida kuja hapa mkutanoni,tunashangazwa
na mji wenye madini ya Tanzanite lakini hakuna miundombinu bora,” alisema
Nasarri.
chanzo:libeneke la kaskazini
No comments:
Post a Comment