.

.
Thursday, December 27, 2012

10:04 PM
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema amesema baadhi ya maofisa wa usalama wa Taifa hawana uzalendo na nchi kwani rasilimali na maliasili  zinaporwa huku wenyewe wakishindwa kuchukua hatua yoyote.
Lema aliyasema hayo juzi mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara kwenye mkutano wa vuguvugu la mabadiliko (M4C) akiwa na Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari na James Ole Millya.
Alisema haoni umuhimu wa watumishi hao wa idara hiyo nyeti ya usalama wa Taifa ambayo inategemewa na nchi,lakini mali hizo zinaporwa huku watu hao hawachukui hatua ya kukomesha vitendo hivyo vya uporaji.
Alisema idara hiyo hivi sasa haina watu wa adilifu kwani wengi wao wamebaki kunywa pombe kali na kuwa wambeya na kusahau wajibu wao wa kujali maslahi ya Taifa ambapo jamii inategemea.

“Hivi sasa hawa watu wamebaki kunywa viroba na kuwa wambea hata hapa kwenye mkutano wapo wananirekodi lakini mimi sina hofu yoyote kwani nazungumza kwa uchungu wa uporwaji wa rasilimali zetu,” alisema Lema.

Alitoa mfano kwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kia ambapo mtu akipita na kitu kidogo hata shilingi 100 kuna kengele inalia kuashiria tatizo lakini imewezekana Twiga akapitishwa kwenye ndege na usalama wa Taifa wapo.

“Kuna faida gani kuwa na watu kama hawa kwani wameshindwa kuzuia wizi na uporaji wa rasilimali zetu hadi nchi nyingine zinakamata mali zetu zikiwa zimeshaondoka kwenye ardhi ya nchi yetu,” alisema Lema.
Alisema kuwa rasilimali na maliasili kama Twiga,nyati,mamba na viboko wanachukuliwa na kusafirishwa kwenda nchi za nje huku idara hiyo inaangalia bila kuchukua hatua yoyote ya kudhibiti hali hiyo.
Naye,Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la vijana la Chadema (Bavicha),John Heche aliwataka wakazi wa wilaya hiyo kuamka kutoka usingizi kwani wamelala,hadi wanakubali rasilimali yao ya madini ya Tanzanite yanaporwa.
Heche alisema kwa muda wote wakazi wa wilaya ya Simanjiro wamekuwa wakiichagua CCM ili hali kuna madini ya Tanzanite ambayo yana thamani kubwa lakini hayawasaidii chochote,kwani wakazi hao wapo kwenye lindi la umasikini.
“Wacheni kucheka katika hili sisi Chadema tunaendelea kuwaelimisha na ninyi kwa ninyi mnapaswa kuamshana ili muda wa uchaguzi ukifika muwaondoe madarakani na kuweka chama ambapo kitajali maslahi yenu,”alisema Heche.
Naye,Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari alisema anashangazwa na mji mdogo wa Mirerani kuwa na madini ya Tanzanite yanayopatikana sehemu hiyo peke yake duniani lakini hakuna maendeleo.
“Mvua imenyesha kwa muda wa nusu saa,lakini barabara zenu zimejaa maji na sisi tumepita kwa shida kuja hapa mkutanoni,tunashangazwa na mji wenye madini ya Tanzanite lakini hakuna miundombinu bora,” alisema Nasarri. 
chanzo:libeneke la kaskazini

0 comments:

Post a Comment