.

.
Saturday, December 15, 2012

12:35 AM
FUGAJI wa Jamii ya Wamasai wamevitaka vyombo vya habari nchini kujenga tabia ya kuandika habari chanya zinazowahusu na siyo hasi peke yake kama ilivyo kawaida ya baadhi ya vyombo vya habari vingi vinavyofanya.
Kauli hiyo waliitoa kwa pamoja katika maazimio yao baada ya kumalizika majadiliano kuhusu matatizo ya wafugaji wa jamii hiyo, mkutano ulioandaliwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC).
Katika mazimio hayo wafugaji hao walisema kuwa ni vyema vyombo vya habari viwe na tabia ya kuripoti hata mambo mazuri ya kwao na siyo yale mabaya jambo ambalo linawafanya kuona kama wananyanyapaliwa.
Pia wafugaji hao walimwomba Mkurugenzi wa UTPC, Abubakar Karasan kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wafugaji hao kila mara ili kujadili matatizo yao na kuweza kuyatafutia ufumbuzi. Aidha wafugaji hao waliomba UTPC kufikisha mapendekezo yao waliyotoa katika mjadala huo juu ya suala zima la katiba mpya katika Tume ya Katiba.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuwapo na uwakilishi wao katika uongozi katika serikali za kijiji hadi kata, ili waweze kuwa na uwakilishi wa kutosha na kuweza kuwa na nguvu katika maamuzi.
Walidai kuwa mara nyingi viongozi wengi wanakuwa ni wakulima hivyo wanapotoa uamuzi unapendelea upande wao. Rais wa UTPC Keneth Simbaya aliwataka wafugaji hao kuondokana na dhana ya kunung’unika na kwamba hali hiyo mara nyingi inajenga mazingira ya hasira na hivyo kufanya uamuzi usio sahihi na kwamba badala ya kufanya hivyo watafute njia ya ufumbuzi.
Alisema kuwa mara nyingi uamuzi unayofanywa katika hasira unakuwa hauna busara na hivyo husababisha kuwa na majuto baadaye. Alisema kuwa UTPC itaandaa utaratibu wa kuwa wanakutana na wafugaji hao katika maeneo tofauti hapa nchini ili kujua kero zao.

0 comments:

Post a Comment