Umati mkubwa wa watu ulijitokeza kwenye mapokezi ya mbunge huyo jana
kuanzia njia panda ya kutokea Uwanja Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA) ambapo msururu mrefu wa magari, bodaboda na baiskeli ulipamba
mapokezi hayo.
Lema aliyekuwa akitokea jijini Dar es Salaam ambapo Mahakama ya Rufaa
ilimrejeshea ubunge wake juzi, alikuwa kwenye gari la wazi huku
akipungia wananchi.
Kwenye baadhi ya miji ya Wilaya ya Arumeru, alilazimishwa kusimama kutokana na wananchi kumzuia wakitaka awasalimu.
Hali hiyo ilisababisha safari kutoka KIA hadi jijini Arusha ambapo kwa
kawaida hutumia saa moja, kuchukua zaidi ya saa sita, kuanzia saa tatu
asubuhi mpaka saa tisa alasiri kufika jijini Arusha.
Baada ya kufika Arusha, msafara huo ulipita kwenye barabara mbalimbali
za jiji hilo, ikiwemo ile ya Afrika ya Mashariki, Goliondoi, Sokoine
kisha kuingia kwenye Uwanja wa Kilombero walikofanyia mkutano, ambapo
kote walipokuwa wakipita wananchi walikuwa wamejaa barabarani
wakimpungia huku wengine wakiwa wamebeba majani kuashiria amani.
Hata hivyo, wananchi wengine waliamua kufuata msafara huo kwa miguu na
magari hali iliyofanya baadhi ya shughuli kusimama kwa muda kwenye
maeneo ambayo ulipita, huku barabara zikiwa hazipitiki mpaka msafara
huo ulipopita.
Aidha, wananchi mbalimbali walitoa maoni yao wakionesha kuridhishwa na
uamuzi wa Mahakama ya Rufaa wa kumrejeshea Lema ubunge ambao alivuliwa
na Mahakama Kuu kwa madai kuwa, haki inaweza kucheleshwa, lakini
haipotei, hivyo wakautaka mhimili wa mahakama kujizatiti kuhakikisha
unatenda haki ili uendelee kuheshimiwa.
Katibu Mwenenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nduruma, Iddi
Ramadhani maarufu kama Iddi Nduruma akizungumza kwenye eneo la mkutano,
alisema kuwa anaamini Mahakama ya Rufaa haitendi kosa kwani ina majaji
makini, hivyo hana kinyongo na uamuzi huo, na kuongeza kuwa shauri hilo
limemkuza zaidi Lema kisiasa kwani hajawahi kushuhudia mapokezi makubwa
kama yake.
“Imefika wakati vyama vya siasa viache chuki binafsi ambazo zinaleta
hasara kwa taifa, huku wakiwanyima wananchi kuhudumiwa na wawakilishi
wao kama ilivyokuwa katika shauri hili ambalo limesababisha wananchi wa
Arusha wakose uwakilishi kwa zaidi ya miezi nane, huku miaka miwili
akiimalizia mahakamani kwenye kesi,” alisema mmoja wa watu waliofika
katika mapokezi hayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa CHADEMA
(BAVICHA), John Heche akizungumza kwenye mkutano huo alisema kuwa
Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe amekwenda Nairobi
nchini Kenya kwenye kampeni za chama cha ODM, kinachoongozwa na Raila
Odinga, ambacho ni chama rafiki, vinginevyo naye angejumuika kwenye
mkutano huo.
Aidha, aliwatahadharisha vijana aliodai kuwa hawana nidhamu ndani ya
baraza hilo ambao wanatumiwa na watu ndani ya CHADEMA na CCM wakipewa
fedha kwa lengo la kukivuruga.
Alisema hakutakuwa na msamaha kwa wote watakaobainika kwani
watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa taratibu na kanuni walizojiwekea.
“Bora tubaki wachache ndani ya BAVICHA kulikoni kuendelea kukaa na watu
wengi ambao ni mamluki, hatutakubali hawa wahuni wachache ambao kwa
tamaa zao za kutaka utajiri wa haraka haraka watuvuruge pamoja na chama
chetu, tutawashughulikia kwenye vikao vyetu,” alisema Heche.
Alisema CHADEMA inapigania kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini
ikiwemo nishati ya gesi, maji, ardhi, madini na nyingine nyingi
zinawanufaisha Watanzania wote, hivyo hawako tayari kuwavumilia mamluki
wachache wanaotumiwa kwa kupewa fedha ili kukwamisha jitihada hizo, ni
lazima wawachukulie hatua.
“Rais Jakaya Kikwete alikuja Arusha akasema kuwa kuna amani, amani ipi?
Amani siyo ujinga wala kuvumilia njaa, bali ni kuwa na maisha bora,
uhakika wa huduma za afya. Hapa nchini hakuna amani bali kuna utulivu
kwani watu wana shida nyingi zinazowakosesha amani, hata wakienda
polisi wanaishia kubambikiziwa kesi,” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo, Lema alitoboa siri kuwa
kilichosababisha arudishiwe ubunge ni baada ya kubaini kuwa hata
wakimvua na uchaguzi ukirudiwa, ataibuka mshindi tena na walifanya
majaribio kwa uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Daraja Mbili ambapo
CHADEMA iliibuka mshindi.
Alisema kuwa hatakuwa tayari kuona machinga wakiendelea kunyanyasika
ndani ya Jimbo la Arusha ambapo alidai kuwa wanahitaji kuheshimiwa kwa
kuhakikisha wanatafutiwa maeneo kabla ya kuondolewa kwenye maeneo
waliyopo kwa kile alichodai kuwa kuwaondoa bila kuwapa maeneo si sawa
kwani hawawezi kwenda porini.
Lema alisema sasa anarudi bungeni, hivyo hoja yake aliyoiwasilisha
akidai kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilidanganya Bunge kuhusiana na
mgogoro wa uchaguzi wa Meya wa Arusha, ataifufua upya.
Aidha, mkutano huo ulihudhuriwa na madiwani wa CHADEMA kutoka
halmashauri za Jiji la Arusha, Hai, Moshi, Karatu, pamoja Mbunge wa
Karatu, Israel Natse, Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Arusha, Cecilia
Paresso na Katibu wa CHADEMA Kanda maalum ya Kinondoni, Henry Kilewo.
0 comments:
Post a Comment