MKUU WA MKOA WA ARUSHA MAGESSA S. MULONGO |
Watoto wanaotoka katika
mazingira magumu na kulelewa katika vituo maalumu, wameiomba serikali kuangalia
uwezekano wa kuwaondoa watoto wenzao wanaoishi magerezani na mama zao bila
hatia ,kwani licha ya kuteseka na hali mbaya ya mazingira iliyopo gerezani, wanakosa
mahitaji ya msingi yanayomstahili mtoto kuyapata.
Aidha wamedai kuwa kitendo cha
watoto hao kuendelea kuishi gerezani ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu na haki zingine
wakati hawana hatia yoyote hivyo wameililia
serikali iwatoe na kuwakabidhi hata kwenye vituo vya kulelea watoto .
Watoto hao walitoa kilio hicho
mbele ya mkuu wa mkoa wa Arusha ,Magesa Mulongo aliyekuwa mgeni rasmi katika
harambee ya kuchangia ujenzi wa madarasa mawili katika kituo cha St.Gemma
kilichopo kisongo jijini hapa, ambacho ni kituo pekee Tanzania kinacholea watoto waliopo
gerezani ambao mama zao walifungwa.
Wakisoma risala yao kwa pamoja iliowasisimua
wageni mbalimbali waliohudhulia hafla hiyo huku baadhi yao kujikuta
wakibubujikwa na machozi akiwemo mkuu huyo wa mkoa,watoto hao wenye umri mdogo
walisema kuwa kitendo cha wenzao kukaa gerezani kama wafungwa ni kuwanyima
uhuru wa kuishi kwani hawana hatia wenye hatia ni wazazi ama walezi wao.
Waliendelea kusema ni vizuri
serikali ikatafakari upya na kuona umuhimu wa kuwaondoa watoto hao waliopo
magerezani ili waungane na wenzao waliopo uraiani na kuondokana na
mateso wanayoyapata bila hatia ikiwemo kuathirika kisaikolojia kutokana na
mazingira ya mageraza pamoja na kukosa
elimu.
‘’kwanini serikali inatufunga
gerezani kwani tumekosa nini kama ni kosa
wametenda wazazi wetu sisi tunafanya nini gerezani ,watoto wanashindwa kusoma
,kula vizuri na kucheza na wenzao, viongozi wa serikali tuoneeni huruma jamani,
tunaomba wenzetu watolewe gerezani’’walisema.
Naye meneja wa kituo hicho,Flora
Ndwata alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa mwaka 2007 kikiwa na watoto
watatu , hadi sasa kina jumla ya watoto 14 wenye umri wa miaka mitatu hadi 10
na kwamba kimeshindwa kuchukuwa watoto wengi kwa sababu ya kukosa fedha za kujiendeshea.
Alisema kituo hicho kilibuniwa
na masister wa kanisa katoliki,shirika la St Gemme baada ya masister hao
kuguswa na hali mbaya za watoto hao waliopo magerezani na kuamua
kuanzisha mkakati wa kuwasaidia kwa kuwaondoa kwa wazazi wao waliopo gerezani.
Alisema hatua hiyo iliwafanya
wachangishane na kuamua kujenga vyumba viwili ambapo walifanikiwa kuwa na
watoto wawili ambao walimudu kuwalea na baadae watu mbalimbali waliwaunga mkono
kwa kuwasaidai michango iliyosaidia kuongezeka kwa watoto hao.
''tumekuwa
tukiwauliza wamewapataje watoto hao wanasema wengine waliingia gerezani wakiwa
na ujauzito na wengine walisema walipata ujauzito wakiwa huko na
kujifungua''alisema Sister Flora
Aliongeza kuwa hadi sasa wana
watoto kutoka gereza kuu la Isanga Dodoma,gereza la Babati na gereza kuu la
Kisongo jijini hapa na kwamba wanatarajia kuomba watoto wengine kadri wanapo
kuwa na uwezo wa kuwahudumia.
Kwa upande wa mkuu wa mkoa wa
Arusha,Magesa Mulongo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwanye harambee hiyo ya
kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa,alifanikiwa kuchangisha shilingi
milioni 63.3 na kuvuka malengo ya shilingi milioni 46 zilizokuwa
zikihitajika,huku ofisi yake ikichangia shilingi milioni 10.
0 comments:
Post a Comment