OFISA uchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Bhoke Ryoba, ameuwawa kwa kupigwa rasisi na watu
wasiojulikana.
Habari
zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea
usiku wa kuamkia jana eneo la Kigamboni Manispaa ya Temeke jijini Dar
es Salaam, ambako ofisa huyo alikuwa anahudhuria sharehe.
Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hoseah, akizungumzia tukio hilo alithibitisha na kueleza kuwa alifariki dunia juzi usiku.
“Tumekuwa
tukipokea simu nyingi kutoka kwa watu mbalimbali wakihitaji kufahamu
ukweli kuhusu tukio la kupigwa risasi kwa mtumishi wa Takukuru, Bhoke
Ryoba,” imesema sehemu ya taarifa hiyo ya Dk Hoseah iliyotolewa na
ofisi ya habari ya Takukuru.
Iliendelea,
“Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hoseah, anapenda kutoa ufafanuzi
kuhusu tukio hili kwamba ni kweli mtumishi Bhoke Ryoba amefariki dunia
jana usiku, Jumamosi Desemba 22, 2012 baada ya kupigwa risasi.
Uchunguzi wa Polisi kuhusu chanzo cha tukio hilo bado unaendelea”.
Baadaye
ofisa habari wa Takukuru Doreen Kapwani alifafanua kuwa ofisa huyo
mchunguzi alifikwa na umauti wakati anajumuika na marafiki zake katika
moja ya tafrija iliyokuwa ikifanyika katika eneo la Kigamboni.
Alisema akiwa katika hafla hiyo, ghalfa walitokea watu wasiojulikana na kumiminia risasi hadi kufa.
“Hawa
watu walimvamia Ryoba aliyekuwa kwenye sherehe moja na kumshambulia kwa
risasi na kisha wakatokomea kusikojulikana,” alisema na kuongeza:
“Watu hao hawakutambulika kwa kuwa baada ya kutekeleza azma hiyo walitoweka haraka na kutokomea.”
Alipotakiwa
kueleza pengine kumekuwepo matukio yoyote katika siku za hivi karibuni
yanayoweza kusababisha tukio hilo, Kapwani alijibu “ni mapema mno sasa
kudadisi suala hilo.”
Kapwani alisema Ofisi ya Takukuru kwa sasa haiwezi kueleza chochote kwani tukio hilo limeripotiwa polisi kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova alipotakiwa
kuelezea hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo baada ya tukio hilo,
alisema kuwa hangeweza kuzungumzia chochote kwa vile alikuwa nje ya
ofisi.
0 comments:
Post a Comment