KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), inakutana kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, leo
na kesho, katika kikao chake cha kawaida, ambapo mbali na mambo mengine
itamjadili Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa CHADEMA, Tumaini
Makene, ilisema kuwa Kamati Kuu itapokea taarifa ya utekelezaji
kutokana na maazimio ya kikao cha dharura kilichokutana Septemba 9,
mwaka huu.
Kikao hicho mbali ya kuagiza chama kimwandikie barua rasmi Rais
Kikwete ili asimamie utekelezaji wa baadhi ya masuala yaliyoko kwenye
mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Kamati Kuu pia iliazimia
masuala kadhaa.
Miongoni mwa masuala hayo ambayo yaliazimiwa ni kuwataka Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali wa Polisi Saidi Mwema, na Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la
Polisi, Kamishna Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,
Faustine Shilogile, wawajibike kwa kujiuzulu nafasi zao au wafukuzwe
kazi.
CHADEMA iliazimia hivyo kwa kuzingatia kwamba mauaji kadhaa
yametokea mikononi mwa Jeshi la Polisi ambalo liko chini ya usimamizi
wao; na vilevile waliazimia kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa,
Michael Kamuhanda, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Morogoro
na askari waliosababisha mauaji ya raia wasio na hatia Morogoro na
Iringa wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.
Licha ya Rais Jakaya Kikwete kukionya chama chake kuacha kutegemea
nguvu ya jeshi la polisi katika kukabiliana na wapinzani, mpaka sasa
bado hajajibu barua aliyoandikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe, kuhusu mauaji yanayofanywa na jeshi hilo kwenye shughuli za
chama hicho.
Hata hivyo, watuhumiwa wanaolalamikiwa na CHADEMA wakitakiwa
kujiuzulu, kufukuzwa au kuchukuliwa hatua za kisheria, bado Rais
Kikwete ameshindwa kuwachukulia hatua yoyote mpaka sasa.
Kwa mujibu wa Makeni, kikao hicho cha siku mbili, mbali na kupokea
taarifa hiyo kuhusu Rais Kikwete, pia kitakuwa na ajenda tatu ambazo ni
taarifa ya hali ya siasa nchini; mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya
nchi; na Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C).
Mara kadhaa viongozi wakuu wa chama hicho, wamekuwa wakimkumbusha
Rais Kikwete kujibu barua yao na kuwachukulia hatua wahusika ili
kuondoa hofu ambayo imetawala kwa umma kuhusu mauaji ya raia yanayozidi
kujitokeza.
CHADEMA katika barua hiyo kwa Rais Kikwete walitoa wito wakimtaka
aunde tume ya huru ya kiuchunguzi ya kimahakama (Judiciary Commission
of Inquiry) kuchunguza vifo vilivyotokea katika mazingira tata katika
mikoa ya Arusha, Tabora, Singida, Morogoro na Iringa.
Pia kutokana na utendaji wasiokuwa na imani nao wa Msajili wa Vyama
vya Siasa, John Tendwa, Kamati Kuu ilimtangaza kuwa ni adui wa
demokrasia asiyefaa kuwa katika nafasi aliyo nayo.
Kamati Kuu iliazimia kuwa pamoja na kuendelea kuheshimu sheria ya
vyama vya siasa, CHADEMA haitashiriki shughuli zozote zitakazosimamiwa
na Tendwa hadi hapo atakapoondolewa katika nafasi yake na kuteuliwa
msajili mwingine.
Likini pia azimio hili hadi leo halijatekelezwa pamoja na lile la
kutaka vyombo vya habari vya umma kuripoti taarifa zao bila upendeleo
wowote kwa weledi, maadili na utaalamu wa hali ya juu kutokana na
kuendeshwa kwa kodi za wananchi.
Chazo: tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment