CHAMA cha Demokarasia na Maendeleo
(CHADEMA) Wilaya ya Chato mkoani Geita, kimemshukia Mkuu wa Polisi
wilayani humo, Leonard Nyaoga kwa madai kuwa anatumiwa na CCM kutaka
kudhoofisha jitihada zao.
Tuhuma hizo zimekuja kufuatia OCD huyo kuualifu uongozi wa CHADEMA
kwa njia ya simu kuwa amesitisha mikutano yao ya hadhara kwa madai
tayari walikwisha kukaa kikao cha pamoja na viongozi wa vyama vya siasa
na dini na kukubaliana kuisitisha.
Hata hivyo sababu hizo zilipingwa vikali na CHADEMA kwa madai kuwa
katika kikao cha pamoja na jeshi hilo Nevemba 7 mwaka huu, ilizuiliwa
mihadhara ya kidini na wala si mikutano ya vyama vya siasa.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu wa
CHADEMA wilaya ya Chato, Mange Ludomya, alisema kitendo cha OCD kuzuia
kuendelea na mikutano yao kinaonyesha wazi jinsi anavyoweza kuwa
anatumiwa na chama tawala kuwadhoofisha.
"Tunamshangaa sana huyu OCD wetu...sisi tulipeleka barua ya
kumtaarifu kuwa tutakuwa na mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha
Nyarututu kata ya Bwanga Desemab 16 kama sheria inavyotuagiza lakini
amenipigia simu ananieleza kuwa mkutano huo usitishwe kwa kuwa
tulikubaliana,” alisema.
Kufuatia hali hiyo, Katibu huyo alisisitiza kuwa mikutano ya
CHADEMA itafanyika kama kawaida na kama ni nguvu za jeshi la polisi ni
bora zikatumika kusaka majambazi wenye silaha zinazoangamiza maisha ya
wananchi.
Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,
Leonard Paulo alikana kuwepo kwa zuio hilo na kudai kuwa zuio kama hilo
hufanyika kwa maandishi si kwa njia ya simu.
Aidha, aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kunapotokea
mkanganyiko kama huo ni vema wakawasiliana na wenzao ngazi ya mkoa kwa
lengo la kumfikia ofisini kwake na kufanya mazungumzo ili kuondoa
dosari zinazoweza kujitokeza.
chanzo: tanzania daima
0 comments:
Post a Comment