Na Mahmud Ahmed- Arusha
MFANYABIASHARA wa madini aina ya Tanzanite mkoani
Arusha,Ngerii Olerumwa anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40 amekutwa
amekufa katika mazingira ya kutatanisha ndani ya hoteli ya Premier Palace
ambayo timu ya wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano imeweka kambi hotelini
hapo jijini Arusha.
Maiti ya mfanyabiashara huyo iligundulika majira ya saa
3 ;30 asubuhi jana mara baada ya mhudumu wa hoteli hiyo kugonga kwa muda
mrefu mlango wa chumba alichokuwa amefikia marehemu huyo bila mafanikio na
kisha kubaini alikuwa amefariki dunia.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo akiwemo meneja wa
hoteli hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake hadharani alisema kwamba marehemu
huyo aliwasili hotelini hapo mnamo desemba 3 mwaka huu majira ya saa 1 ;00
jioni na kukodi chumba kimojawapo hotelini hapo.
Meneja huyo akisimulia tukio hilo alisema kwamba marehemu
aliwasili akiwa peke yake hotelini hapo na kubainisha kwamba yeye ndiye alikuwa
mtu wa mwisho kukodi chumba hotelini hapo.
Hatahivyo,alidai kwamba ilipotimu jana majira ya saa
3 ;30 asubuhi wakati mhudumu wa hoteli hiyo akigonga mlango wa chumba
alichofia marehemu kwa lengo la kufanya usafi mlango huo haukuweza kufunguliwa
kwa wakati hali iliyowapelekea kufanya juhudi za kuufungua mlango huo kwa
lazima.
Alisema kwamba baada ya kufanikiwa kuufungua mlango huo
walijaribu kumwamsha marehemu lakini hakuweza kuamka hali iliyowapelekea
kuliarifu jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo.
Gazeti hili lilipofika maeneo ya hoteli hiyo liliwashuhudia
askari wa upepelezi kutoka jeshi la polisi mkoani hapa wakichukua maelezo kwa
baadhi ya watumishi wa hoteli hiyo wakiwemo walinzi wa hoteli hiyo huku baadhi
ya wabunge wanaounda timu ya wabunge wa bunge la jamhuri wakitaharuki kutokana
na tukio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti ndugu wa marehemu ambao
walikusanyanya nje ya hoteli hiyo walisema kwamba wameshtushwa na kifo cha
ndugu yao na wanahisi kwamba aliuwawa katika mazingira ya kutatanisha huku
wakilitaka jeshi la polisi kubaini chanzo cha kifo cha marehemu.
Akihojiwa na waandishi wa habari kamanda mkuu wa jeshi la
polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo huku
akisisitiza kwamba jeshi lake linachunguza kwa kina kifo hicho.
Sabas,alisema kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika
chumba cha kuhifadhia maiti ndani ya hospitali ya mkoa ya Mt,Meru na atatoa
taarifa kamili ya tukio hilo kuanzia leo mbele ya waandishi wa habari.
0 comments:
Post a Comment