MWANAFUNZI wa kidato cha tatu katika shule ya Sekondari ya
Tongoni nje kidogo ya jiji la Tanga, (jina tunalihifadhi) amekutwa
amekufa ndani ya nyumba ya kulala wageni alikopelekwa kutolewa mimba
bila mafanikio.
Kwa
mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe mwanafunzi huyo alikutwa amekufa
juzi katika nyumba ya kulala wageni iliyopo barabara ya 21 jijini Tanga.
Mmoja
wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni ambaye aliomba jina lake
lihifadhiwe alisema kwamba mwanafunzi huyo aliingia saa 4.00 asubuhi
siku ya tukio akiwa ameambatana na kijana mmoja wakakodi chumba.
“Baadaye
alikuja mwanaume mmoja wa makamo ambaye alituuliza kama wameingia
mwanafunzi huyo na mwenzake, tulipomwonyesha chumba walichoingia naye
akakodi chumba cha jirani ndipo tukaona wote wakijifungia kwenye chumba
kimoja,” alisema mhudumu.
Mhudumu
huyo alisema baada ya muda wa saa moja, mvulana na mzee huyo wakaaga
kwamba wanatoka huku wakisema kwamba msichana amebaki chumbani akiwa
amepumzika. Akithibitisha habari hizi, Kamanda Massawe alisema taarifa
ya tukio hilo ilitolewa na mhudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni
katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni Jijini Tanga.
“Tatizo
ni kwamba nyumba hii ya wageni wahudumu wake hawakuwapa wageni hao
daftari ili waorodheshe majina yao hivyo inakuwa vigumu kuwafahamu,”
alisema Kamanda Massawe na kufafanua kuwa alifariki akitolewa mimba ya
mwezi mmoja.
Kamanda
Massawe alisema mpaka sasa hakuna mtu aliyekamatwa na kwamba polisi
wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini waliohusika na kifo hicho.
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment