.

.
Tuesday, December 18, 2012

11:09 PM
mkuu wa kitengo cha polisi jamii Merry Lugola alipokuwa akitoa somo kwa vijana wa chama cha mapinduzi mkoa wa Arusha
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la polisi mkoa wa Arusha kupitia kitengo cha Polisi Jamii limeanza kupenyeza elimu yake hadi kwa vyama vya siasa ikiwa ni utekelezaji wa usambaji wa elimu hiyo kupitia makundi mbalimbali.
Tukio hilo lilitokea juzi katika ukumbi wa mikutano wa Golden Rose uliopo jijini hapa ambapo viongozi na wajumbe wa Mkutano wa Baraza  la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi lilipotoa mwaliko kwa jeshi hilo kupitia kitengo hicho ili wajumbe wake wapate elimu hiyo.
Kutokana na mwaliko huo ndipo Mkuu wa kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Arusha, Mrakibu wa Polisi Mary Lugola alipowasili ukumbini hapo na kuanza kutoa somo hilo kwa wajumbe hao. Bi, Lugola alisema kwamba jeshi la Polisi linahimiza suala la ulinzi shirikishi kwa mitaa mbalimbali kuanzisha vikundi hivyo ili kuimarisha usalama katika maeneo yao.
Alisema programu hiyo ambayo lengo lake ni kushirikisha wananchi katika kupambana na uhalifu itasaidia kubaini, kuzuia, kutanzua, na kupeana taarifa kabla uhalifu haujatokea katika eneo husika.
“Sisi jeshi la Polisi tupo tayari kwenda kuelimisha kwenye kikundi au chama chochote ambacho kitakuwa tayari kupokea elimu tunayoitoa hali ambayo itasaidia kuimarika kwa usalama katika mkoa wetu”. Alifafanua Bi. Lugola.
Mrakibu huyo aliongeza kwa kusema kwamba, anaamini viongozi wa vyama, dini na wazee wa mila ndio makundi ambayo yanaushawishi mkubwa kwa wananchi hivyo kupitia makundi hayo jeshi la polisi linaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuisambaza elimu hiyo kwa watanzania wengi.
Mkuu huyo wa kitengo hicho alisema kwamba, kuwepo kwa ushirikiano kati ya jeshi la Polisi na wananchi kumeleta na kutaendelea kuleta tija katika suala zima la kupeana taarifa za kiuhalifu na waalifu. Aliongeza kwa kusema kwamba katika kipindi hiki wanajamii wanatakiwa wawe pamoja katika suala la ulinzi bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini hasa kwa kufuata sheria za serikali za mitaa ya mwaka 1982.
Aliwataka wajumbe hao kupitia maeneo yao wanayoishi waviwezeshe vikundi hivyo vya ulinzi shirikishi kwa kuvichangia vifaa mbalimbali kama vile tochi, sare na kadhalika ili viweze kuanya kazi kwa ufanisi zaidi huku akiongeza kwamba, falsafa ya Polisi Jamii haijanza leo bali imeanza toka mwaka 1820’s nchini Uingereza hivyo si kitu kigeni hapa duniani kwani karibu nchi zote zinatekeleza mpango huo kwa lengo la kujiimarisha kiulinzi.
Bi. Lugola pia aliwataka wanaUVCCM mkoa wa Arusha kutii sheria bila shuruti katika utendaji wao hali ambayo itasaidia kuimarisha amani iliyopo mkoani hapa.
Alimalizia kwa kuahidi kutoa elimu ya polisi jamii katika siku zijazo pindi atakapoalikwa tena kwani bado kuna Programu nyingi kama vile Usalama wetu kwanza, Ulinzi jirani na kadhalika ambazo hakuweza kuzifundisha kutokana na ufinyu wa muda ambapo wajumbe hao walikuwa na ratiba ya kwenda hospitali na kisha kurudi tena ukumbini hapo kuanza mkutano kulingana na ratiba yao jinsi ilivyokuwa inaonyesha.
Toka mwaka 2006 jeshi la polisi hapa nchini limekuwa likiwatembelea viongozi, vikundi vya ulinzi shirikishi na wananchi katika maeneo yao hasa ngazi ya mtaa, kata hadi tarafa kwa lengo la kuwapa elimu ya ulinzi shirikishi jambo ambalo linasaidia katika upatikanaji wa taarifa za uhalifu na wahalifu ambazo zinafanyiwa kazi na jeshi hilo na hatimaye kuendeleza uimarishaji wa ulinzi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
 

0 comments:

Post a Comment