Mbunge jimbo la Ubungo-Chadema,Mh John Mnyika.
----
Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha
Sheria ya ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa
masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86)
kutoka China.
Nitataka pia nakala za mikataba wa
mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya
kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu
la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi
Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.
Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza
pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na
unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na
baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba
wa mradi husika.
Pendekezo hilo lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia
serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa
yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za
uwekezaji huo mkubwa.
Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo na badala
yake Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe 8 Novemba 2012
Mkoani Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko yameanza kujitokeza
katika maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa bungeni
na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka
Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine
inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi husika.
Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya
kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo;
Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo
imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha
utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga
Fungu (Kilwa).
Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila
kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa
kuishauri na kuisimamia Serikali hivyo
ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na barua niliyomwandikia
mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa haijajibiwa.
Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake
kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati
na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata
kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa
sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Pamoja na mambo mengine nilipendekeza
Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa
Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya
hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya
fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera,
mpango mkakati na sheria ya gesi asili.
Hatua hii ni muhimu kwa sasa kwa
kuwa hata baada ya uamuzi wake kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati
husika, Spika hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa hali
ambayo imeacha ombwe la uongozi na usimamizi wa kibunge (Parliamentary
Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
26/12/2012
0 comments:
Post a Comment