ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema elimu inayotolewa nchini ni ya kibaguzi.
Kardinali
Pengo alisema hayo Dar es Salaam jana alipokuwa akiwasilisha ujumbe wa
maaskofu wa Kanisa Katoliki walioutoa katika mkutano wao uliofanyika
Oktoba 7 hadi 28, mwaka huu huko Roma, Italia.
Alisema watu wote wenye mapenzi mema na nchi hii wanapaswa kutoa kipaumbele katika upatikanaji wa elimu bora kwa kila Mtanzania.
Kardinali
Pengo alisema hapendezwi na namna elimu inavyotolewa nchini kwani
kimfumo, baadhi ya shule zimekuwa vitegauchumi, hivyo kuwa kikwazo kwa
watu wenye kipato cha chini.
“Wenye
vipato vya chini hawawezi kusoma katika shule hizi kwa sababu zinatoza
ada kubwa ambayo maskini hawezi kumudu gharama zake,” alisema.
Askofu
Pengo alionya kuwa endapo hali hiyo itaachiwa, inaweza kuwafanya wale
waliokosa elimu kuwa chanzo cha vurugu kwa kuwa watasimama kidete kudai
haki yao.
Maoni ya Katiba
Katika
hatua nyingine, Kardinali Pengo alizungumzia mchakato wa Maoni ya
Katiba unaoendelea nchini, huku akiwaonya baadhi ya wanasiasa na
taasisi mbalimbali za dini kuacha kuwashinikiza wananchi kutoa maoni
kwa ajili ya masilahi yao binafsi.
“Kila
mtu aruhusiwe kutoa maoni yake, lakini lazima tukubaliane kuwa kila mtu
ana maoni yake na maoni yote hayawezi kuingizwa katika Katiba Mpya,”
alisema Pengo.
Alisema
kwa kuwa Katiba inagusa masilahi ya nchi, ni vyema kila mwananchi
akatumia fursa yake ya kuwasilisha maoni yake mwenyewe.
Alitahadharisha
kuwa wananchi wasiposhirikishwa katika mchakato wa Katiba Mpya,
wanaweza kuja kuikataa kwa sababu maoni yao hayakuzingatiwa.
Suala la udini
Kiongozi
huyo wa Kanisa Katoliki wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitaka
Serikali kuchukua hatua za makusudi kwa wale wote watakaobainika
kusababisha uharibifu wa mali za dhehebu la dini yoyote hapa nchini,
kama wanavyofanya pindi kunapotokea uhalifu katika benki au wizi katika
maeneo ya viongozi na sehemu nyingine.
Alisema
nchi imegawanyika katika madhehebu mbalimbali, hivyo inapotokea dhehebu
moja kulitukana na kuharibu mali za jingine, Serikali haipaswi kukaa
kimya.
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment