Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania
(JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha akiwa na wabunge wa Chadema,Godbless
Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) baada ya
kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge hao katika
Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara jana.
MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema) Godbless Lema, huenda akazo
kitita cha Sh85 milioni ambazo ni malimbikizo ya mishahara na posho
mbalimbali ambazo hakulipwa wakati alipokuwa nje ya Bunge.
Lema
amekuwa nje ya Bunge kwa miezi minane, kuanzia Aprili 5 mwaka huu
wakati alipovuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, hadi
aliporejeshewa ubunge wake Ijumaa wiki iliyopita na Mahakama ya Rufani
ambayo ilikubali rufaa yake iliyopinga uamuzi huo.
Katibu
wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah jana alisema baada ya kurejea bungeni,
Lema atalipwa stahili zake zote anazostahili kwa muda wote wa siku 260
ambao alikwa nje ya Bunge.
Ingawa
ofisi hiyo ya bunge haikusema atalipwa shilingi ngapi, uchambuzi wa
malipo na stahili za wabunge umebaini kuwa mbunge huyo kupitia Chadema,
atalipwa kitita cha Sh85 milioni ikiwa ni mshahara wake na posho kwa
kipindi cha miezi nane alichokuwa nje ya Bunge.
Hata hivyo, Lema mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kuwa, malipo yake yanaweza kufikia Sh60 milioni.
Lema
aliyeibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alivuliwa
wadhifa huo na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, April 5, 2012, kufuatia
kesi iliyofunguliwa na makanda watatu wa CCM; Mussa Mkanga, Happy
Kivuyo na Agness Mollel, wakipinga ushindi wake. Hata hivyo, Desemba
21,2012, Mahakama ya Rufani ilimrejesha bungeni, baada ya kushinda
rufaa yake aliyokata mahakamani hapo kupinga hukumu na tuzo ya Mahakama
Kuu Arusha iliyomvua wadhifa huo.
Tangu
alipovuliwa ubunge hadi Mahakama ya Rufani ilipomrejesha tena bungeni,
Lema alikuwa amekosa mikutano mitatu ya Bunge yenye jumla ya vikao 84.
Mikutano hiyo ni ule wa mwezi Aprili, mkutano wa Bunge la Bajeti Juni hadi Agosti na mkutano wa Novemba.
Vyanzo
vya kuaminika kutoka ndani ya Bunge na wakiwamo wabunge wa upinzani na
wale wa CCM vilisema kwamba malipo ya mbunge kwa mwezi ni Sh10.7
milioni, yakijumuisha Sh2.3 milioni za mshahara, Sh2.5 milioni za
mafuta, posho ya jimbo inayokaribia Sh5 milioni na malipo mengineyo.
Kwa
muda wa miezi zaidi ya minane ambao amekuwa nje ya Bunge, malimbikizo
ya mshahara wake yanafikia Sh18.4 milioni, posho ya jimbo Sh40 milioni,
mafuta Sh20 milioni na posho nyingine Sh6.6 milioni.
Kauli ya Lema
Hata
hivyo akizungumza na Mwananchi jana, Lema alisema kuwa ingawa hajui kwa
hakika kuwa malipo yake ni kiasi gani, lakini kwa hesabu za haraka,
yanafikia Sh60 milioni.
Alisema wakati wa kesi hiyo ikiendelea hakuwahi kuwaza kwamba angerejeshwa bungeni, hivyo hakuwahi atalipwa kiasi gani na Bunge.
“Sijui
kwanza nitalipwa nini kwani sikuwahi kukaa na kupiga hesabu za malipo
haya, maana najua ubunge siyo faraja bali ni kuongoza harakati za
kuwasaidia wananchi kutetea haki zao mbalimbali,” alisema Lema.
Alisema
alichokuwa akijua ni kwamba kama akishinda basi, atarejeshewa gharama
za kesi yake na makada wa CCM ambao walimfungulia kesi kwani ni malipo
yanayotambulika kisheria.
“Najua lazima hawa makada wa CCM, walipe
gharama zangu za kesi.Baada ya wao kushinda kesi Mahakama Kuu, Arusha,
waliniletea madai ya kuwalipa Sh139 milioni na sasa mimi nawadai zaidi
ya milioni 250,” alisema Lema na kuongeza.
chanzo :mwananchi
0 comments:
Post a Comment