.

.
Sunday, December 23, 2012

10:57 PM

Na Abubakar Mapwisa, Kinshasa
 
AZAM FC ya Dar es Salaam, jana imetwaa ubingwa wa Kombe la Hisani, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya kuwafunga wenyeji Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa.
Azam walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya 75.
Katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Hata hivyo, Azam jana hawakukabidhiwa Kombe uwanjani hapo baada ya waandaji kusema wanakwenda kulipamba kwanza, hivyo sherehe za makabidhiano ya Kombe zinaweza kufanyika leo.
Azam jana ilicheza bila kocha wake Mkuu, Muingereza Stewart Hall ambaye aliondoka juzi usiku mjini hapa kwenda kwao Uingereza kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kabla ya kuondoka mjini hapa, Stewart alisema kwamba anamuachia timu hiyo msaidizi wake, Kali Ongala na anaamini atafanya kazi.
Stewart alisema Kali ni mtu ambaye siku zote amekuwa akimuandaa kuwa kocha wa baadaye wa Azam na hii si mara ya kwanza kumuachia timu, kwani aliwahi kufanya hivyo mara kadhaa ikiwemo kwenye Kombe la Urafiki, ambalo aliiongoza timu kufika Fainali.
“Siku moja nitaondoka Azam na kumuacha Kali awe kocha Mkuu, siku zote namtayarisha, namjengea kujiamini, naamini atakuwa kocha bora sana wa Azam, sina wasiwasi naye, namuachia timu na anaweza kurudisha Kombe Dar es Salaam,”alisema Stewart ambaye atarejea mwakani.
Azam iliingia fainali, baada ya juzi kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs. Azam inatarajiwa kuondoka hapa kesho mchana kurejea Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana, kikosi cha Azam kinatarajiwa kuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samih Hajji Nuhu, Joackins Atudo, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou, Seif Abdallah/Uhuru Suleiman, Kipre Tchetche/Zahor Pazi, Humphrey Mieno na Gaudence Mwaikimba. 

0 comments:

Post a Comment