.

.
Sunday, December 23, 2012

11:01 PM
Kikosi cha Azam kilichokuwa tishio DRC

Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
MABINGWA wa Kombe la Hisani, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Azam FC ya Dar es Salaam wanaondoka leo saa 5:00 za hapa, sawa na saa 7:00 mchana za Afrika Mashariki, kurejea nyumbani Tanzania kwa furaha baada ya kutwaa taji hilo.
Azam wanaondoka kwa ndege ya Kenya Airwarys na watapitia Nairobi, ambako wataunganisha ndege ya kurejea Dar es Salaam.
Katibu wa Azam, Nassor Idrisa amesema kwamba timu ikirejea Dar es Salaam, wachezaji watapewa mapumziko ya siku mbili kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi na baada ya hapo watakutana kujiandaa kwa safari ya Zanzibar kwenda kutetea Kombe lao la Mapinduzi.
Azam juzi ilitwaa ubingwa wa Kombe la Hisani baada ya kuwafunga wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs mjini hapa.
Azam walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 12 kabla ya Dragons kusawazisha dakika ya 75 na katika mikwaju ya penalti, kipa Mwadini Ally alicheza mikwaju miwili ya Dragons, wakati Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Joackins Atudo na Samih Hajji Nuhu walifunga penalti za Azam.
Azam juzi ilicheza bila kocha wake Mkuu, Muingereza Stewart Hall ambaye aliondoka juzi usiku mjini hapa kwenda kwao Uingereza kwa ajili ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya na iliongozwa na Kocha Msaidizi, Kali Ongala.
Azam iliingia fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya hapa Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
Kikosi cha Azam kilichoshiriki mashindano haya ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki, Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey Mieno na Joackins Atudo.
Katika mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti.

0 comments:

Post a Comment