MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu
Tanzania (THRD), umedai kupokea kwa mshangao taarifa zilizoandikwa na
gazeti la serikali zikisema kuwa Rais Jakaya Kikwete amelizika rasmi
gazeti la MwanaHalisi kwa uchochezi.
Kwamba habari hiyo imeupotosha umma kwa kiwango kikubwa, na hivyo
wanaitaka Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu kutoa ufafanuzi,
kutokana na kupotoshwa kwa kosa lililosababisha gazeti hilo kufungiwa.
Mtandao huo ambao ni mkusanyiko wa mashirika zaidi ya 60 ya
watetezi wa haki za binadamu wakiwamo wanasheria, waandishi na watetezi
wengine, ulisema kuwa habari hizo ni za upotoshaji kwa sababu
zinamkariri Rais Kikwete akiwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Kwamba habari iliyochapishwa na gazeti hilo la HabariLeo ilidai
kuwa MwanaHalisi lilifungiwa kwa sababu liliandika habari ya uchochezi
ikiwataka askari kuasi na kutotii amri.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mratibu wa Mtandao huo,
Onesmo Olengurumwa alisema kuwa habari hiyo haikuandikwa na gazeti la
MwanaHalisi bali gazeti jingine ambapo tayari watuhumiwa wamefikishwa
mahakamani.
“Tunaamini kilichoandikwa na mwandishi wa gazeti hilo ndiyo kauli
iliyotolewa na Rais Kikwete kwa sababu habari hiyo imeletwa na mhariri
mzoefu na makini, na tunaamini hivyo kwa sababu rais ameitoa kauli hiyo
mahali pake, wakati akiwasilisha ripoti ya Tathmini ya Utawala Bora
(APRM),” alisema.
Aliongeza kuwa, wanashawishika kuamini kwamba iwapo siku zote Rais
Kikwete alikuwa akiamini kuwa MwanaHalisi ndiyo waliochapisha habari
inayohusu askari kugoma, basi alipotoshwa tangu mwanzo na hivyo
anahitaji kuelimishwa vizuri juu ya suala hilo.
Alisisitiza kuwa, wanaendelea kuamini kuwa MwanaHalisi lilionewa
kama sababu zilizosababishwa kufungiwa ni pamoja na zile ambazo gazeti
hilo lilimnukuu Rais Kikwete huko Ethiopia.
Katika habari hiyo, Rais Kikwete alikaririwa akisema “...Ndio kuna
gazeti moja tumelifungia na kuna watu wanaosema tuliondolee
adhabu…tumesema hapana…kutaka Jeshi liasi huu sio uandishi wa habari.”
MwanaHalisi lilifungiwa na serikali Julai 30 mwaka jana, kutokana
na habari yake iliyomhusisha ofisa wa Ikulu katika sakata la kutekwa na
kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka,
kudaiwa kuwa ni ya uchochezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers (HHPL)
inayochapisha MwanaHalisi, Saed Kubenea, alipoulizwa juu ya kauli ya
rais, alisema ameipokea kwa faraja.
“Tuna taarifa za serikali kukamata na kushitaki mwandishi
aliyeandika habari ambazo serikali ilisema zinachochea uasi katika
majeshi; mhariri wa gazeti lililozichapisha na mwenye mtambo uliochapa
gazeti. Lakini hayo yote hayahusu MwanaHalisi,” alisema.
Alisema kuwa kwake si gazeti wala waandishi wa habari wanaotuhumiwa
uchochezi wa jeshi. Lakini kama walifungiwa kwa madai hayo, basi sasa
rais ameibuka na ukweli ambao utawaweka huru.
chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment