WATALII zaidi ya 100 kutoka nchi 25
ulimwenguni jana walianza safari yao ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa
lengo la kuchangisha dola za Marekani zaidi ya milioni 1 sawa na zaidi
ya sh bilioni 1.5 za Tanzania ambazo zitatumika kusaidia miradi ya
wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi mbalimbali za taifa hapa nchini.
Safari hiyo imeandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Nchini
(Tanapa) kwa kushirikiana na kampuni ya Wings of Kilimanjaro ya nchini
Australia ambapo watashuka toka kwenye kilele cha mlima huo mrefu
kuliko yote barani Afrika kwa kuruka kwa kutumia miamvuli maalumu,
tukio ambalo litakuwa ni la kwanza tangu kugunduliwa kwa mlima huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, meneja
uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete, na meneja mradi wa kampuni hiyo,
Adrian Mgrae, walisema kuwa fedha hizo zitaelekezwa kwenye miradi
mbalimbali ya kukabiliana na umaskini vijijini, uharibifu wa mazingira
na misaada ya kibinadamu.
Walisema kuwa misaada hiyo inajumuisha uchimbaji wa visima vya maji
safi ya kunywa, kuboresha miundo mbinu ya elimu na kusaidia waathirika
wa virusi vinavyosababisha ukimwi inayosimamiwa na mashirika yasiyo ya
kiserikali ya One Foundation, Plant with Purpose na Worldsave
International.
Walisema kuwa watalii hao wanaotarajiwa kupanda mlima huo kupitia
njia ya Machame mwishoni mwa Januari, mwaka huu, wanatarajiwa kushuka
kwa kuruka na miamvuli hiyo maalumu kati ya Februari 5 na 6 kulingana
na hali ya hewa itakavyokuwa kwenye kilele cha Kibo.
Shelutete alisema kuwa watalii hao wanaotazamiwa kupanda mlima huo
kwa muda wa siku saba wanatazamiwa kutua kwa miavuli hiyo kwenye
viwanja vya Shule ya Sekondari Umbwe na Chuo cha Ufundi Stadi cha
Kibosho, wilayani Moshi, hivyo aliwahimiza wananchi kujitokeza kujionea
tukio hilo la kihistoria.
Meneja uhusiano huyo wa Tanapa alisema kuwa tukio hilo pia
linatazamiwa kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 600 ambao
watawahudumia watalii hao kwa safari ya kupanda milima huo ikijumuisha
wabeba mizigo, wapishi na waongoza watalii.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya uwakala wa Utalii ya Top
of Africa ya mjini Moshi, Silvanus Mvungi, ambaye ndiye aliyeandaa
safari ya watalii hao alisema kuwa katika kuhakikisha usalama wa wageni
hao kutakuwa na helikopta maalumu kwa ajili ya uokoaji ambayo itakuwa
tayari muda wote mpaka kukamilika kwa shughuli hiyo.
No comments:
Post a Comment