Kiemba, shujaa wa Simba leo |
Na Nurat Mahmoud,
Muscat
SIMBA SC
imefanikiwa kupata ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman jioni hii, baada
ya kuifunga Ahly Sidab kwenye Uwanja wa Sidab mjini Muscat.
Katika mchezo
huo, shujaa wa Simba, alikuwa ni kiungo aliyerudi juu kisoka hivi sasa, Amri Ramadhan
Kiemba aliyeifungia timu hiyo bao la ushindi.
Katika mechi
hiyo nzuri na ya kusisimua, wenyeji ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kipindi
cha kwanza, lililofungwa na kiungo Mbrazil, aitwaye Lopez, kabla ya kiungo wa Simba,
Kiggi Makassy kusawazisha kipindi hicho hicho cha kwanza.
Hadi mapumziko,
timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na leo Simba walicheza soka nzuri mno, huku
wachezaji vijana, Miraj Adam, Abdallah Seseme, Haroun Chanongo na Shomari
Kapombe waking’ara zaidi.
Kipindi cha
pili, kocha Mfaransa, Patrick Liewig alifanya mabadiliko, akiwaingiza Rashid
Ismail, Marcel Kaheza wote waliopandishwa kutoka timu B na Kiemba ambao waliongeza
makali ya Mnyama na hatimaye kupata ushindi huo.
Alikuwa ni
kiungo wa zamani wa Kagera Sugar, Yanga SC, Miembeni na Moro United aliyeipatia
Simba ushindi wa kwanza katika ziara yake ya Oman kwa kufunga bao safi la
ushindi dakika za mwishoni.
Huo ulikuwa
mchezo wa tatu kwa Simba katika ziara hiyo, awali ikifungwa 1-0 na U23 ya Oman
na baadaye 3-1 na timu ya Jeshi la nchi hiyo, Qaboos, bao la Wekundu hao wa
Msimbazi, likifungwa na Haruna Moshi ‘Boban’.
Huo ulikuwa
mchezo wa sita kwa Mfaransa, Liewig kuiongoza Simba tangu aanze kazi mapema
mwezi huu, awali akishinda mechi moja, sare mbili na kufungwa mbili.
Aliiongoza Simba SC kuifunga 4-2 Jamhuri, sare ya 1-1 na Tusker
FC,
1-1 na Bandari zote katika Kombe
la Mapinduzi Zanzibar, kabla ya kufungwa 1-0 na U23 ya Oman na 3-1 dhidi ya Qaboos
katika ziara ya Oman.
Simba SC
inatarajiwa kurejea nchini Jumatano baada ya ziara hiyo, tayari kwa mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo
wa leo, kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja, Miraj Adam, Paul Ngalema, Mussa
Mudde, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Abdallah Seseme, Abdallah
Juma/Rashid Ismail, Mrisho Ngassa/Marcel Kaheza na Kiggi Makassy/Amri Kiemba.
REKODI YA
PATRICK LIEWIG SIMBA SC
Simba SC 4-2 Jamhuri (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Tusker FC (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 1-1 Bandari (Kombe la Mapinduzi)
Simba SC 0-1 U23 Oman (Kirafiki)
Simba SC 1-3 Qaboos (Kirafiki)
Simba 2-1 Ahly Sidab (Kirafiki)
0 comments:
Post a Comment