Rais Jakaya Kikwete akifuatilia zoezi la uokoaji kwenye jengo la
ghorofa 16 lililoanguka katika Mtaa wa Indira Gandhi jana. Kulia ni
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na
Mkurugenzi wa Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Meja Jenerali,
Sylvester Rioba.
Zoezi la kutafuta miili iliyokwama katika vifusi inaendelea, zaidi ya maiti 22 zapatikana.
Dar es Salaam. Idadi
ya watu waliokufa kutokana na kufukiwa na kifusi cha jengo la ghorofa
16 lililoporomoka juzi asubuhi jijini Dar es Salaam, imefikia 22.
Habari
zilizopatikana kutoka eneo la uokoaji na kuthibitishwa na Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova zinaeleza kuwa
miili iliyopatikana imepelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jengo
hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko
Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya Lucky Construction Limited
liliporomoka saa 2.30 asubuhi wakati mafundi na vibarua wakiendelea na
ujenzi huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na
biashara zao kama kawaida.
Rais Kikwete
Rais
Jakaya Kikwete ambaye jana pia alifika katika eneo la tukio, kama
ilivyokuwa juzi, alipata taarifa fupi ya maendeleo ya uokoaji kutoka
kwa Mkuu wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda Kova.
Baada
ya kupewa taarifa hiyo, Rais Kikwete alimwagiza Kamanda Kova
kuhakikisha wahusika wanakamatwa akiwamo Mkadiriaji Majengo (Quantity
surveyor), mchora ramani za majengo (Architecturer), Mhandisi Mshauri
(Consultant) na Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam. Juzi baada ya
kutembelea eneo la tukio, Rais Kikwete aliagiza wahusika wote wa ujenzi
huo wachukuliwe hatua kali.
Habari
zilizopatikana jana zilidai kuwa Diwani wa Kata ya Goba, Wilaya
Kinondoni, Ibrahim Kisoka ambaye ndiye mmiliki wa kampuni ya ujenzi, na
Mhandisi Mshauri kwa pamoja wamejisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi na
hadi saa 8:00 jana mchana walikuwa wakihojiwa.
Awali
Kamanda Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemtaka mmiliki wa
Kampuni ya Lucky Construction Limited ambaye ni Diwani wa Kata ya Goba,
Kisoka na wahusika wengine kujisamilisha kituo cha polisi, kabla
hawajaamua kutumia nguvu kumtafuta.
Pinda atembelea eneo la tukio
Waziri
Mkuu Mizengo Pinda alifika eneo hilo saa 3:41 asubuhi, kujionea hali
ilivyo, lakini hakutoa tamko lolote. “Sina la kusema,” alisema Waziri
Mkuu alipoulizwa na waandishi wa habari kutoa kauli ya serikali
kuhusiana na tukio hilo.
Hata
hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,
William Lukuvi aliyefuatana na Pinda, alisikika akimwagiza Kamanda Kova
kuhakikisha mchora ramani wa jengo hilo naye anatiwa nguvuni kwa kuwa
jengo hilo lilikuwa la ghorofa 10, lakini likajengwa hadi 16. Mtu
mwingine ambaye anatafutwa na jeshi la polisi kukamatwa ni Mhandisi
Mshauri.
Lukuvi
alimwagiza Kova kuwa watu waliokuwa karibu na jengo jingine la ghorofa
15 lililojengwa na mkandarasi huyo, kuhama mara moja na ubomoaji
ufanyike bila kuleta madhara.
Mwenyekiti wa CUF
Mwenyekiti
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alitumia fursa
hiyo kuitaka Serikali kuwabana makandarasi wasio na sifa kwani
wanahatarisha maisha ya watu.
“Huu ni uzembe, wahandisi wa jiji
walikuwa wapi? Wasimamizi na washauri walikuwa wapi hadi jengo
linafikia ghorofa 16?” Alihoji Profesa Lipumba.
Profesa
Lipumba aliitaka Bodi ya Makandarasi (CRB) kufuta leseni ya kampuni
hiyo, kwani imeonyesha kuwa haiwezi kusimamia ujenzi na hivyo
kusababisha vifo.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment