Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane kutokana na tuhuma mbalimbali.
DAR ES SALAAM.
RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kuipanga upya safu ya Baraza lake la Mawaziri wakati wowote, huku baadhi ya naibu mawaziri wakipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mawaziri kamili.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kutengua
uteuzi wa mawaziri wanne alioufanya siku tisa zilizopita, mawaziri hao
walishutumiwa kushindwa kuwajibika katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza Ujangili.
Ripoti ya kamati ndogo ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira iliyoundwa kuchunguza operesheni hiyo, ilieleza
kuwa athari zilizotokana na operesheni hiyo zilisababishwa na wizara nne
zilizokuwa zikiongozwa na mawaziri hao.
Waliong’olewa katika sakata hilo ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Mambo ya Ndani
ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk
Mathayo David.
Rais Kikwete anafanya mabadiliko ya baraza lake la
mawaziri ikiwa imepita miezi 18 tangu alipowang’oa mawaziri wanane
kutokana na tuhuma mbalimbali.
Historia inaonyesha kuwa Rais Kikwete amekuwa na
utaratibu wa kuwapa uwaziri wabunge ambao amewateua, huku akiwapandisha
naibu mawaziri kuwa mawaziri.
Kwa mujibu wa Ibara ya 66 (1) (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa
marekebisho inampa mamlaka Rais kuwateua wabunge 10, mpaka sasa
ameshawateua wanane na kubakiza nafasi mbili pekee.
Kati ya wabunge wanane walioteuliwa na Rais Kikwete, watano walipewa wizara za kuziongoza.
Wabunge hao na wizara zao kwenye mabano ni Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Profesa Makame
Mbarawa (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia).
Wengine ni Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na
Madini), na Saada Mkuya na Janet Mbene (wote ni Naibu Mawaziri wa Wizara
ya Fedha).
Kutokana na utamaduni huo, Dk Asha-Rose Migiro
anapewa nafasi kubwa ya kuingia kwenye baraza jipya la mawaziri, kwani
naye hivi karibuni ameteuliwa kuwa mbunge.
Wabunge ambao wameteuliwa na Rais lakini
hakuwapa uwaziri mpaka sasa ni Zakia Meghji, James Mbatia na Dk
Asha-Rose Migiro.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment