.

.
Sunday, December 22, 2013

2:00 AM

 NINA furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu ! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji.



Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.



Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia.



Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995.




Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko.



Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. 



Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana.



Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma. Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma.



Nimekuwa nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu. Viatu hivyo viliitwa ‘asante Salim’ vilivyokuwa vinatengenezwa na Kampuni ya Bora Shoes.



Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha! Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la tatu.



Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania. Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu, lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza watoto wote.



Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na mafanikio ya hali ya juu sana.



Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia.



Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo.



Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga. Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya.



Haya ni matunda ya nyinyi watu wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo.



Juhudi hizi lazima ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji.




Katika kipindi cha utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna watu hapa nyumbani walisema ‘sasa huyu kawa mbunge wa Taifa’ lakini watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na sio Kigoma tu.




Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani. 



Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. 


Hii ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri Mkuu.



Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za Umma. 



Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika kuimarisha demokrasia yetu.



Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.



Kutoaminiana.
Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. 



Wananchi wameacha kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni uongo.
Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli. 



Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa unatengenezwa badala ya kutafutwa.


Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko Uswisi.



Huu ulikuwa ni uongo. 


Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi kinyumecha sheria.


Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina, bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata kupelekea mchakato mzima kuvurugika.



Sitaingia mtego huu! Lakini hatua hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA.



Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na uhuru wa mawazo.



Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na waliojaa woga. 



Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia. Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta.
Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa litaongozwa.



Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli.



Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu. Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni vicheko na mazungumzo.




Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule. Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. 



Na siasa ina misingi yake ambayo sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi.
Msingi wa siasa ni kuwa inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa. Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.




Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo!
Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. 



Ninasukumwa kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu;kila ninapoona akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi; ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai asubuhi.


Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu. Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni 2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania.



Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3) zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).



Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa – robo yake tuingeweza kujenga barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka Dar-es-salaam! Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza ajira bora kwa vijana wetu.




Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu angalau pea 10 ya viatu.



Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti !.



Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea bila sababu.



Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra zake zinakuwa huru.




Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko huleta matumaini.
Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi hiki kipya.



Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha; ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo.


Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania; siasa za mabadiliko; siasa zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo wananchi wa Tanzania. 

Mungu ibariki Tanzania

0 comments:

Post a Comment