Ni bahati mbaya kwamba Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania linalotarajiwa kuanza kikao chake Mei 6, mwaka huu
mjini Dodoma litalazimika kuendeshwa ‘fastafasta’ kutokana na kutengewa
siku chache kukamilisha shughuli zake. Kama inavyofahamika kwa wengi,
utaratibu wa sasa unalitaka Bunge hilo kuwa limejadili na kupitisha
Bajeti ya Serikali pamoja na Sheria za Fedha ifikapo mwishoni mwa Juni
kila mwaka, ili kuruhusu bajeti husika kuanza kutumika Julai Mosi,
ambayo ndiyo siku ya kwanza ya mwaka mpya wa fedha.
Tunazo sababu mbili za msingi tunaposema ni bahati
mbaya Bunge la Bajeti kulazimika kuendeshwa ‘fastafasta’. Kwanza ni
ukweli kwamba mijadala kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali na bajeti za wizara
mbalimbali haitakuwa ya kina kutokana na ufinyu wa muda. Pili, kutokana
na ufinyu huo wa muda, kuna uwezekano mkubwa Bajeti Kuu ya Serikali na
za wizara nyingi kubwa na nyeti kama Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo
inatumia zaidi ya theluthi moja ya bajeti nzima ya Serikali,
zikapitishwa zikiwa na takwimu za kupikwa na za kufikirika zilizobuniwa
na watumishi wasio waaminifu wanaoendesha mitandao ya wizi wa fedha za
Serikali.
Hatari itakayotokana na hali hiyo ni kupatikana
kwa bajeti zisizokuwa na uhalisia, kwani hata Kamati za Bunge zimepewa
wiki moja tu kujadili bajeti husika, badala ya wiki tatu. Matokeo ya
kazi za kurashiarashia namna hiyo ni kulifanya Bunge kuwa mhuri wa
kupitisha madudu na kuhalalisha vitendo vya wizi, ufisadi na ubadhirifu
wa fedha za Serikali. Ratiba ya Bunge hilo inaonyesha kuwa, Bunge la
Bajeti litakutana kwa siku 52, zikiwa pungufu kwa siku 28,
ikilinganishwa na mkutano kama huo mwaka jana.
Swali la kujiuliza hapa ni hili: Kwanini Bunge
limefikia hali hiyo? Pamoja na Uongozi wa Bunge kusema siku nyingi
zimetumika kwenye shughuli za Bunge Maalumu la Katiba, halisemi kwanini
mamlaka husika haikushauriwa kuahirisha Bunge hilo la Katiba ambalo
limetumia siku 67 katika malumbano na mijadala isiyokuwa na tija kwa
taifa. Bunge la Bajeti lingepewa kipaumbele kwa sababu ndilo uti wa
mgongo wa shughuli za Serikali na taasisi zake.
Sisi tunadhani kwamba yalikuwa makosa makubwa
kuwaacha mawaziri na wabunge wa Bunge la Muungano wakijikita katika
siasa na itikadi za vyama ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, huku wakijua
fika kwamba Bunge la Bajeti lazima liwe limepitisha Bajeti na kumaliza
mkutano wake ifikapo mwishoni mwa Juni. Pamoja na kutambua kwamba
kutofanya hivyo kunaweza kusababisha majanga kwa taifa, bado waliona
kipaumbele ni siasa na malumbano yasiyoisha kuhusu ‘kura iwe ya siri au
ya wazi’ na ‘muundo wa serikali mbili au tatu’. Hayo ndiyo matokeo ya
kuweka siasa mbele na kudidimiza uchumi.
Sasa nini kifanyike? Spika anaweza kujaribu kuokoa
jahazi kwa kutoruhusu porojo bungeni. Mawaziri wawasilishe bajeti fupi
lakini zilizosheheni takwimu sahihi na tafakuri jadidi. Michango ya
wabunge ilenge kwenye hoja na wasipewe muda wa kupongezana na
kuwatambulisha marafiki, mashemeji na kadhalika. Iwapo kanuni na ratiba
vitapanguliwa ili vikao vifanyike mchana na usiku, siku za kazi na za
mapumziko, itawezekana kupatikana kwa bajeti zilizochambuliwa barabara,
zenye mwelekeo na endelevu.
mwananchi
mwananchi
No comments:
Post a Comment