Dodoma. Uzalishaji wa chakula
Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki, unatarajiwa kuongezeka msimu wa
kilimo wa 2014/2015, hivyo kupunguza soko la mazao ya chakula
yanayozalishwa nchini.
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher
Chizza alisema kama hali itakuwa hivyo, Serikali inawashauri wakulima
na wafanyabiashara nchini kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake
kwa mwaka 2014/2015 bungeni jana yanayofikia Sh318.7 bilioni, Chizza
alisema wakulima na wafanyabiashara wataruhusiwa kuuza mazao nje ya
nchi.
Chizza alisema taarifa za awali zinaonyesha kuwa,
mvua zimenyesha vizuri katika nchi nyingine za Afrika Mashariki, hali
inayoashiria kuwapo kwa mavuno mazuri katika nchi hizo.
Kwa muda mrefu, Serikali imekuwa ikizuia mazao ya
chakula, hususan mahindi ambayo yana soko kubwa nchi za Kenya na Somalia
kuuzwa nje.
“Hali ikiwa hivyo kwa maana ya kuongezeka mavuno
nchi nyingine za Afrika Mashariki, Serikali inawashauri wakulima na
wafanyabiashara kutafuta masoko nje ya nchi,” alisema Waziri Chizza na
kuongeza:
“Napenda kusisitiza kwamba, Serikali haizuii
uuzaji halali wa chakula cha ziada nje ya nchi kwa sababu tunatarajia
kupata mavuno mengi msimu huu wa kilimo,” alisema waziri huyo katika
bajeti yake.
Hata hivyo, Waziri Chizza alisema hali halisi ya
chakula kitakachovunwa nchini msimu huu wa kilimo itajulikana baada ya
kufanya tathmini Juni, 2014.
Alisema ingawa dalili ziko hivyo, lakini watakuwa na uhakika zaidi wa hali ya chakula kufikia katikati ya mwaka huu.
Wakati huohuo, Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA),
imepanga kununua kutoka kwa wakulima tani 200,000 za nafaka, zikiwamo
tani 190,000 za mahindi na tani 10,000 za mpunga kwa msimu wa kilimo wa
2014/2015.
No comments:
Post a Comment