FRIENDS of Simba wamesikia kelele na tambo za
Yanga hasa baada ya kutua kwa Wabrazili Marcio Maximo (kocha) na Andrey
Coutinho Kiungo), wamecheka sana kisha wakatamka jambo moja kwa
mashabiki kwa wao kwa kusema: “Tulieni fitna zote za mpira tunazijua.”
Kundi hilo ambalo limeahidi kumaliza usajili wa
Simba wiki hii na kuingiza timu kambini lipo karibu na uongozi uliopo
madarakani na limetenga fungu lisilopungua Sh300 milioni kuhakikisha
Simba inarudi kwenye hadhi yake. Imebainika kuwa kambi haitakuwa karibu
na macho ya Yanga wala Azam ambao ndio wapinzani wao wakubwa.
Mmoja wa vigogo wa Friends na ambaye pia ni Katibu
wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kassim Dewji, ameliambia Mwanaspoti kuwa
wanasikia kelele za watani wao juu ya mambo mengi, lakini wao wameamua
kunyamaza wanafanya mambo yao kwa vitendo na majibu yataonekana
uwanjani.
Dewji alisema kuwa majigambo ya Maximo na wadau
wengine wa Yanga hayawatishi kwani wanachokifanya wao kwa sasa wanakijua
na uongozi uliopo madarakani unajitambua tofauti na miaka ya nyuma na
wana ufahamu mkubwa wa kila fitina inayofanyika ndani na nje ya uwanja
kwenye Ligi Kuu Bara.
“Tunawasikia kelele zao na wala hazituumizi sisi
tunafanya yetu, msimu ujao ndiyo watajua tulikuwa tunafanya nini,
hatutaki kupiga kelele juu ya usajili hata kama watasema timu ni mbovu
lakini kikubwa ni ushindi na mashindano ya kimataifa Simba itashiriki.
“Wanasimba wasipate taabu na ujio wa kocha wa
Yanga, Maximo ni kocha mzuri lakini ni wa kawaida tu, kwa sasa
tunajipanga juu ya usajili,” alisema Dewji.
Alisema kuwa baada ya Rais wa Simba, Evans Aveva
kuunda Kamati zake, kila mjumbe atakuwa na jukumu la kutekeleza kazi
yake aliyopewa ambapo wao wanahakikisha kumaliza suala la usajili wiki
hii.
Tayari kamati hiyo imeanza michakato wa kuwasajili
straika wa Kenya Raphael Kiongera anayekipiga klabu ya KCB, kipa
Hussein Sharif ‘Cassilas’ wa Mtibwa Sugar Sugar, Mkenya Jerry Santo na
Deus Kaseke kutoka Mbeya.
Mabeki Joram Mgeveke na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ tayari ni mali halali ya Simba.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba, zimesema
kuwa mazoezi ya timu hiyo yataanza kesho Jumatano kati ya viwanja vitatu
vilivyopendekezwa ambavyo ni Kunduchi, Chuo Kikuu na Chuo cha Sheria.
Amissi Tambwe, Joseph Owino na Donald Mosoti wao imeelezwa watawasili siku yoyote kwani suala lao la usafiri linashughulikiwa.
0 comments:
Post a Comment