Na Bertha Ismail - Arusha
Timu ya Ushirika ya mjini Moshi
imefanikwa kuwa washindi katika bonanza la maveterani baada ya kuichapa timu ya
Kivule ya jijini Dar- es-salaam kwa magoli 2-0 katika uwanja wa Sheik Amri
Abeid ya jijini Arusha.
Bonanza hilo lililoandaliwa na timu
ya maveterani ya jijini Arusha “All Stars” lilihudhuriwa na timu sita za
maveterani kutoka mikoa mbalimbali ya hapa nchini ambapo walishindana katika
kusakata soka huku wenyeji Arusha wakionekana kutamba dakika za awali na baadae
kuzidiwa nguvu na timu za wageni na kuzima ndoto za kutwaa ubingwa.
Katika bonanza hilo, timu za
maveterani zilizokuwa kundi ‘A’ ni pamoja na timu ya Mwanza Veterani “Mwanza
starehe”, Dar-es-salaam “Kivule” pamoja na Dodoma Veterani, huku zilizokuwa
kundi ‘B’ ni pamoja na Arusha All Stars, Ushirika na Namanga Veterani.
Michuano hiyo iliyokuwa ikichezwa
kwa dakika 30 ilifunguliwa dimba na wenyeji, Arusha all stars na Namanga ambapo
timu ya Arusha ilifanikiwa kuichapa Namanga kwa magoli 2-0, mechi iliyofuatiwa
na timu ya Kivule ya Jijini Dar na kuichapa Dodoma Veterani kwa goli 1-0.
Timu ya Namanga ilizidi kuonewa
baada ya kushuka dimbani na timu ya Ushirika ya Moshi na kugaragazwa 1-0,
ambapo Timu ya Dodoma walitoshana nguvu na timu ya Mwanza Veterani baada ya
kumaliza mchuano bila kufungana, na baada ya mchuano huo timu ya Arusha all
Stars ilishuka dimbani tena kuminyana na timu ya Ushirika ya Moshi lakini
wenyeji hao walionekana kuzidiwa nguvu na majirani zao baada ya kufungwa goli
1-0.
Baada ya michuano hiyo kila kundi
lilitoa mshindi, ambao ni Arusha All Stars pamoja na Mwanza Starehe na kushuka
dimbani ambapo Arusha ilifanikiwa kuichapa Mwanza 1-0, huku Kivule ya
Dar-es-salaam ikishuka Dimbani na timu ya Ushirika ya Mjini Moshi ambapo Kivule
ilizidiwa nguvu dakika za mwisho na kuchapwa magoli 2-0 mfululizo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa waandaji
wa bonanza hilo, Laurence Sabuni, alisema kuwa kufuatia ushindi huo wa Timu ya
Ushirika ya Moshi itazawadiwa kikombe kikubwa huku mshindi wa pili ambae ni Kivule
ya jijini Dar-es-salaam ikizawadiwa kikombe kidogo ambazo hata hivyo hadi
bonanza linafikia tamati majira ya saa 12:30 jioni vikombe hivyo havikuwasili
eneo la tukio.
Wakizungumzia Matokeo hayo, Tumaini
Andrew wa timu ya Ushirika Pamoja na Joseph Mbewa wa timu ya Kivule ya Dar
walisema kuwa matokea hayo ni ya haki wala hakuna wa kumlaumu kwani katika
mashindano yeyote ile kuzidiana kupo hivyo kutumia udhaifu wa mwenzio kupata
ushindi ni sawa zaidi kuliko kutumia ubabe kununua ushindi.
Aidha bonanza hilo la maveterani
hufanyika kila mwaka mwezi wa nane kwa kuzunguka mikoa mbalimbali kwa lengo la
kuwaenzi maveterani watatu (Francis Lungu, Judicate Estomili, Amani Mwalim) wa
timu ya All stars waliofariki mwaka 1999 kwa ajali mbaya ya gari eneo la Mwanga
mkoani Kilimanjaro walipokuwa wakitokea jijini Dar-es-salaam kwenye mashindano
ya maveterani wa mikoa mbalimbali hapa nchini na wengi kujeruhiwa.
Mwisho……..
No comments:
Post a Comment