Nassary awagawia wananchi wake ardhi ya ACU wilayni Arumeru mkoano Arusha
Joshua Nassari
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari juzi aliongoza wapiga kura wake kugawa shamba linalomilikiwa na Chama cha Ushirika mkoani Arusha (ACU), akisema amechoka kuona wananchi wake wakisotea ardhi ilhali kuna maeneo hayaendelezwi.
Nassari aliongozana na wapiga kura wake hadi eneo la shamba la Valeska na kuanza kuwagawia ardhi bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mmiliki wa ardhi husika.
Akiwa katika eneo hilo, alipima ardhi kwa kuhesabu hatua na kuigawa kwa wapigakura wake wenye uhitaji wa ardhi.
Kutokana na uamuzi wake huo wa kujichukulia madaraka na kuigawa ardhi kuonekana kuwashangaza wengi, mwandishi wa habari hizi alilazimika kuomba ufafanuzi wa tukio hilo kupitia simu yake ya kiganjani, ambapo alisema amelazimika kuchukua uamuzi huo anaouona unafaa ili wananchi wake wapate ardhi.
Alisema amelazimika kuingilia kati suala hilo, kutokana na migogoro isiyoisha ya ardhi wilayani Arumeru kwani awali wahusika wa ushirika huo walitoa ekari 1,500 za ardhi na kuzigawa kwa wananchi ili kuepusha maandamano na uvamizi wa mara kwa mara, lakini kinyume chake ardhi hiyo hawakupewa wananchi, bali madiwani wa Halmashauri ya Arumeru wamekuwa nao wakiitaka ardhi hiyo.
Aidha, alisema wakati wananchi ambao ni wapigakura wake wakidai ekari hizo, kuna watumishi wamejitwalia ekari 400 kati ya hizo 1,500 zilizotolewa na ACU na kujimilikisha wao huku watumishi hao bila kuwataja majina wakiwakodishia wananchi wake.
Alisema madiwani wa Halmashauri hiyo walitoa ekari 500 na kuwapa wananchi na ekari nyingine wakipanga mambo yao na kutokana na hali hiyo, anaamini kuna maslahi ya watumishi wa halmashauri hiyo.
“Kutokana na hali hiyo nimeamua kama mbunge nigawe ardhi mwenyewe kwa kupima kwa miguu ili kila mwananchi aweze kupata ardhi sababu watendaji wameshindwa kusimamia haki.
“Hapa ndio nimeanza na nitaendelea kugawa ardhi kwenye mashamba yasiyoendelezwa na hayo ndio maamuzi yangu kama Mbunge. “Nasema siwezi kukubali wananchi wangu kila siku walalamikie masuala ya ardhi wakati kuna madiwani, Mkuu wa Wilaya (DC) na viongozi mbalimbali. Nimegawa Valeska, bado nitakweenda Mbughuni hadi Kikuletwa nitagawa ardhi, kama Mbunge nimechoka na migogoro isiyoisha”.
Suala la Nassari kugawa ardhi bila kufuata utaratibu liliibuka mara baada ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene kufanya kikao na maofisa ardhi na wapimaji wa Mkoa wa Arusha kutoka Halmashauri tatu za Jiji la Arusha, Arusha Vijijini na Arumeru ili kubaini ukubwa wa tatizo hilo na kutafuta suluhu ya migogoro hiyo.
Katika mazungumzo hayo na watumishi hao, pia walifika viongozi kutoka ACU ambao walisema chama hicho kilishatoa ekari 1,500 kwa wananchi wa wilaya hiyo, lakini madiwani walikataa eneo la Mashariki walilopewa na kutaka wachague eneo wanalolitaka wao.
Alisema ACU imeshatoa eneo hilo ili kuwapa wananchi, lakini kuna milolongo mingi ikiwemo masuala ya siasa kati ya madiwani ambao hawakubaliani na maamuzi ya ACU.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mjumbe wa Bodi ya ACU, Furahini Mungure alisema shamba hilo la ACU ni kubwa na linahitaji kuendelezwa ikiwemo kujenga vitega uchumi sambamba na mradi wa ghorofa 17, hivyo kutokana na mgogoro huo ukiwamo wa suala la Nassari kugawa ardhi kunarudisha nyuma masuala ya uwekezaji.
“Tunamshangaa Mbunge kwa kitendo cha kugawa ardhi tunayoimiliki bila kufuata taratibu, yeye amechukua kinamama, watoto, wazee, vijana na kwenda kuwagawia ardhi kwa kuwapimia na miguu… sasa hii ni siasa ili aonekane ni mwema kwao kumbe hakufuata taratibu hivyo tunakuomba Naibu Waziri uingilie kati mgogoro huu,” alisema. A
lisema wakati Nassari alipokuwa akigawa ardhi hiyo, Polisi walifika eneo hilo la shamba la Valeska ili kumwamuru mbunge huyo na wananchi wasitishe kugawana ardhi, lakini bila ya kutumia nguvu.
“Polisi walimhoji Nassari kwa nini anafanya hivyo, lakini yeye aliendelea kugawa ardhi na hapo tunawapongeza polisi licha ya ardhi ya shamba letu kugawiwa na mbunge kwa wananchi sababu kulikuwa na wananchi wa rika mbalimbali wakiwemo watoto kama wangeweza kuchukua maamuzi magumu watu wangeumia. “Lakini kwa busara, polisi waliondoka na kumwacha Nassari akigawa ardhi ambayo si halali kwa wananchi, hivyo hatujui hii ni mbinu ya mtaji wa kisiasa au ni nini maana masuala ya ugawaji ardhi yana taratibu zake kisheria,” alisema.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arumeru, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Benedict Mapujila alisema polisi walitumia busara maana kulikuwa na wananchi wengi pamoja na watoto.
Naye Simbachawene alisema inashangaza kuona Mbunge anayejua sheria, taratibu na kanuni kuchukua maamuzi yasiyofaa na kuahidi kuonana naye ili kuzungumza zaidi juu ya suala hilo.
Pia alisema atapanga ziara ya kukutana na madiwani wa Halmashauri hiyo pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Nyirembe Munasa ili kutatua mgogoro huo, kwani ameshindwa kukutana nao kwa sasa kutokana na misiba iliyotokea ambayo ilisababisha wafanyakazi wa halmashauri hiyo kufa kutokana na ajali eneo la Nduruma.
Wilaya ya Arumeru imekuwa na migogoro mingi ya ardhi hali inayosababisha wananchi kuvamia mara kwa mara mashamba ya wawekezaji kwa madai ya kuwa mashamba hayo hayajaendelezwa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment