Halmashauri
ya jiji la Arusha limefanikiwa kuitimisha zoezi la uandikishaji wa daftari la
wapiga kura kwa kuandikisha jumla ya wananchi 321,575, huku mkurugunzi wa jiji hilo
akiwataka wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura.
Akizungumza
na gazeti hili wakala wa uandikishaji jiji la Arusha, Iddi Juma ambaye pia ni
Mkurugenzi wa jiji alisema kuwa awali walitarajia kuandikisha watu 265,087
lakini wamefanikiwa kuvuka lengo kwa zaidi ya asilimia 21 kwani wameandikisha
watu 321,575 ambayo ni sawa na asilimia 121.
“Tunajivunia
kuvuka lengo letu la idadi ya walioandikishwa lakini hatuwezi kujivunia kwa
uandikishaji tu bali tutajivuania zaidi pale idadi hii waliyojiandikishwa wakijitokeza
wote kupiga kura octoba kwenye uchaguzi mkuu wa kupata viongozi mbali mbali wa
nchi”
“Nimesema
hivyo kwa sababu vijana wengi walioonekana kupata vitambulisho hivyo
walifurahia tu kuwa itawasaidia katika mambo yao binafsi lakini siyo kupia
kura, lakini naomba niwaambie kuwa kupata kitambulisho ni jambo moja lakini
kupiga kura ni jambo la msingi zaidi hasa ikizingatiwa ni haki ya msingi kupata
kiongozi aliyepatikana kwa kura yako hivyo wajitokeze kwa wingi kupiga kura”
Mkuu huyo
amesema kuwa kumekuwa na mazoea ya wananchi kutokujitokeza katika zoezi la
upigaji kura kutokana na kuendekeza starehe pamoja na biashara na kusema kuwa
swala hil ni kosa kwa sheria ya nchi hasa kutokana na gharama kubwa serikali
inayotumia kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa hivyo kwa mwaka huu Arusha wasifanye
kosa hilo bali wajitokeze kuchagua kiongozi wanaemtaka kwa maendeleo ya jiji,
mkoa na nchi kwa ujumla.
Zoezi la
uandikishaji wa wapiga kura jiji la Arusha lilianza june 16 na kufikia tamati
julai 18 huku wanawake 160, 143 wakijiandikisha na wanaume 161, 432 katika
vituo 183 katika kata 25 za jiji la Arusha.
“Katika
zoezi hili naamini hakuna mtu asiyejiandikisha hasa baada ya kuruhusu watu
wenye kazi au biashara wajiandikishe kwenye vituo vya biashara zao kutokana na
ugumu wa kutoka, na pia hili linajidhihirisha siku tatu za mwisho hakukuwa na
foleni kabisa kwenye vituo vya uandikishaji huku vituo vingine wakala wakikosa
kabisa wateja la kushinda wakipiga soga hii inaonyesha kabisa watu wamemalizika
na kama kuna watu wasiojiandikisha basi hawakutaka tu”
No comments:
Post a Comment