Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa
wa Mara, John Tupa kwenye viwanja vya Nyerere mjini Dodoma Machi 28,
2014.
Wengine pichani ni
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowasa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,
Stephen Wasira a Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameongoza
viongozi mbalimbali na mamia ya wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuuaga mwili wa
aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mara ambaye alifariki dunia ghafla Machi 25,
2014 akiwa ziarani wilayani Tarime.
Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa
marehemu John Gabriel Tuppa kwa wakazi wa mji wa Dodoma ilifanyika leo
mchana (Ijumaa, Machi 28, 2014) kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere
ambako ibada ya kumwombea marehemu ilifanyika. Baadaye mchana, mwili
wake ulisafirishwa kwenda wilayani Kilosa, mkoani Morogoro kwa mazishi.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho,
Padri Chesco Msaga ambaye aliongoza ibada hiyo, alisema Mungu aliwaumba
wanadamu ili wampende na wamtumikie na kwamba marehemu Tuppa alilitimiza
jambo hilo vilivyo.
Alisema wakati wa uhai wake, Bw.
Tuppa alipenda haki na popote alipokwenda alitetea haki za wanyonge.
“Sote ni mashahidi wa jinsi alivyopenda watu na jinsi alivyowatumikia
watu. Alikuwa mnyenyekevu, aliwasikiliza wengine na alithamini michango
ya wengine. Na sisi tunapaswa kuiga hilo,” alisema.
Naye Dk. Right Mmbaga, akitoa
salamu za rambirambi kwa niaba ya Baraza la Wazee la Dodoma Mjini
alisema: “Wale watumishi ambao bado wako kazini na walipata nafasi ya
kufanya kazi na Bw. Tuppa, wajifunze kutoka kwake na wafuate nyayo zake
kama njia ya kumuenzi.”
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Bw.
Mwigulu Nchemba, akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, alisema
Chama cha Mapinduzi kimempoteza kamisaa makini sana aliyekuwa mstari wa
mbele katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), Bw.
William Lukuvi aliwaasa wakazi wa Dodoma kuenzi mambo ambayo Bw. Tuppa
aliwafanyia wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma hata kama walikuwa
hawayaoni.
“Alikuwa na upeo wa kufanya kazi
kwa spidi lakini kwa utulivu. Wakati tumeanza naye kazi hapa Dodoma
mwaka 2006, kulikuwa na shule sita tu za sekondari lakini katika kipindi
cha miaka miwili alifanikisha kusimamia ujenzi wa shule za sekondari
30,” alisema Bw. Lukuvi ambaye wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi
wa Makanisa ya mkoa wa Dodoma, Askofu Dk. Yohana Masinga alisema
viongozi hawajui kwamba wakishateuliwa, wao ni watumishi wa Mungu kwa
sababu wanawaongoza watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Akinukuu neno la Mungu kutoka
kitabu cha Waebrania sura ya 13 aya ya 7, linalosema wakumbukeni
waliokuwa wakiwaongoza, ichunguzeni miisho ya mwenendo wao na iigeni
imani yao, Askofu Masinga aliwataka wote waige mfano wa utendaji kazi wa
Bw. Tuppa.
“John Tuppa alikuwa ni mtendaji na
kanisa limempoteza mtu makini. Ninawaomba viongozi wa nchi hii waige
mfano wa John Tuppa. John Tuppa awe ni mfano kwao, na wafanye hivyo kwa
ukombozi wa nchi yetu,” alisema.
Bw. Tuppa anatarajiwa kuzikwa kesho (Jumamosi, Machi 29, 2014) wilayani Kilosa.
Alizaliwa Januari mosi, 1950. Amewahi
kuwa Mkuu wa Wilaya za Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya
kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mke na watoto
watano.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
Home
»
»Unlabelled
» PINDA KUONGOZA MAZISHI YA MKUU WA MKOA WA MARA
Friday, March 28, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment