Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili Dodoma keshokutwa, ikiwa ni
siku moja kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa
fedha 2014/15.
Habari zilizopatikana jana zinasema Rais ataongoza kikao cha Baraza la
Mawaziri kitakachopewa muhtasari kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka ujao
wa fedha na baadaye atafuatilia uwasilishaji wa bajeti hiyo bungeni
akiwa Dodoma.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema asingeweza
kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yuko likizo lakini akaweka bayana kwamba
kwa kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa bungeni, lazima Baraza la
Mawaziri lipewe muhtasari wa bajeti husika.
“Ni kawaida kabla ya bajeti kuwasilishwa, Rais huongoza kikao cha Baraza
la Mawaziri yaani pre budget cabinet meeting ambako Waziri wa Fedha
hutoa briefing (muhtasari) kuhusu maeneo muhimu ya bajeti, kwa hiyo siyo
jambo jipya ni suala la kawaida,” alisema Rweyemamu.
Itakumbukwa kuwa mwaka jana kabla ya kusomwa kwa bajeti ya 2013/14, Rais
Kikwete alikuwa Dodoma ambako pamoja na kukutana na mawaziri, pia
alifanya kikao na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Hata hivyo, uwepo wake mjini Dodoma safari hii umekuja wakati kukiwa na
dalili za mvutano mkubwa kati ya Bunge na Serikali kutokana na
kutotolewa kwa fedha za kutosha za maendeleo kwa mwaka wa fedha unaoisha
Juni 30 mwaka huu.
Taarifa zinasema bajeti inayomalizika mwishoni mwa mwaka huu,
inapungukiwa kiasi cha Sh1.8 trilioni, huku Serikali ikilaumiwa na
wabunge kwa kutoa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.52 trilioni, ambayo
ingepunguza nakisi iliyopo kwenye bajeti kwa asilimia 84.4.
Wakati wa mjadala wa bajeti za wizara tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti
Mei 6 mwaka huu, wabunge wamesikika mara kadhaa wakilalamika kwamba
fedha za maendeleo zilizotolewa kwa wizara katika bajeti ya 2013/14 ni
kati ya asilimia 25 na 30, jambo ambalo limesababisha kukwama kwa miradi
mingi.
Keshokutwa itakuwa siku ya mwisho ya mashauriano baina ya Serikali
kupitia Wizara ya Fedha na Bunge kupitia Kamati yake ya Bajeti
inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Mazungumzo hayo yaliyoanza Juni 5 mwaka huu, yalilenga kuangalia
uwezekano wa kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuwezesha kuzingatiwa
kwa ushauri wa wabunge, pamoja na kusaka fedha kuziba pengo la Sh1.8
trilioni katika bajeti ya 2013/14.
Alipoulizwa jana, Chenge hakuwa tayari kuzungumzia hatua iliyofikiwa
katika mashauriano hayo na badala yake alisema kwa ufupi: “Ndugu yangu
mambo ya Bunge, tutakutana kwenye taarifa yetu ya kamati
tutakayoiwasilisha bungeni.”
0 comments:
Post a Comment