.

.
Monday, June 9, 2014

11:36 PM
WABUNGE wa Tanzania katika Bunge la jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), wamesisitiza kutounga mkono hoja ya kumng’oa Spika wa bunge hilo, Margaret Zziwa, kwa kuwa haina maslahi na Tanzania na wana Afrika Mashariki kwa ujumla.

Hayo yameelezwa jana na wabunge watatu miongoni mwa wabunge hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA Tanzania, Adam Kimbisa ambapo alisema baada ya kuchunguza kwa umakini walibaini kuwa katika jaribio hilo la kumng’oa spika kuna ajenda ya siri.

Alisema kuwa hoja hiyo haina maslahi ya Tanzania na iko kinyume na malengo ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, pia wamebaini kuwa hoja yenyewe ni sehemu ya mchezo mchafu wa ajenda ya siri ya kujaribu kuweka mbele maslahi ya baadhi ya wanachama wachache ndani ya jumuiya hiyo badala ya kuzingatia maslahi mapana ya jumuiya hiyo.

“Tuhuma zilizotajwa dhidi ya Spika wa EALA kuhusu yeye kuonesha upendeleaji, ujeuri na mapungufu mengine ya uongozi zimegundulika kuwa hazina mashiko wala mantiki,” alisema Kimbisa.

Aidha, alisema kitendo kilichowashtua ni kumekuwa na majaribio ya baadhi ya wabunge wa EALA kutoka nje ya Tanzania na viongozi wa sekretarieti ya jumuiya hiyo kutaka kulazimisha sahihi za baadhi ya wabunge wa Tanzania kutumika kinyume na utaratibu kuunga mkono azimio hilo, jambo linalodhihirisha kuwepo kwa ajenda ya siri katika sakata hilo dhidi ya maslahi ya Tanzania na jumuiya kwa ujumla.

Alisema wabunge watatu wa EALA kutoka Tanzania ambao awali waliunga mkono hoja hiyo kwa sahihi zao, baadae waliamua kuipinga kwa kutoa sahihi zao kwa hiari yao wenyewe baada ya kuchunguza kwa umakini zaidi na kugundua mchezo huo, ambapo walimwandikia barua Katibu wa Bunge wa EALA kumweleza uamuzi wao.

“Hoja yenyewe kisheria ni batili kwa kuwa haikuwasilishwa bungeni ndani ya siku saba tangu ilipopelekwa kwa Katibu wa Bunge na pia imekosa sahihi za kuungwa mkono na wabunge wanne kutoka kila nchi mwanachama wa jumuiya kama kanuni zinavyotamka.

“Tunaomba uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ngazi zote, ikiwemo sekretarieti ya jumuiya kuheshimu maamuzi ya wabunge wa EALA kutoka Tanzania,” alisema.

Alisema awali wabunge watano wa bunge hilo wa Tanzania kati ya tisa walionesha kuunga mkono hoja hiyo lakini baada ya kubaini kuwepo kwa mchezo mchafui na ajenda ya siri wabunge watatu waliondoa sahihi zao na kufanya idadi ya wabunge kutoka Tanzania kupinga hoja hiyo kufikia saba kati ya tisa.

Alisema wabunge hao wameshapoteza muda mwingi, fedha na rasilimali nyingine katika kujadili hoja hiyo isiyo na tija.

Alisema sasa wanahitaji kuweka jitihada zao katika kazi myuhimu ya kutetea maslahi ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Naye Katibu wa Wabunge wa EALA wa Tanzania, Shy-Rose Bhanji alisema, awali alikuwa mstari wa mbele kuunga mkono hoja hiyo lakini alikuja kubaini kuwa kuna vikao vya siri vinaendelea juu ya sakata hilo, jambo lililofanya aamuue kupinga hoja hiyo.

“Ni kweli nilikuwa mstari wa mbele kutaka aondolewe lakini baada ya kutafakari na kuchunguza kwa makini chanzo halisi niligundua kuwa hoja hii haina maslahi kwa Watanzania na sisi ni wazalendo tuko kwa ajili ya kuiwakilisha Tanzania,” alusema.

Alisema kuwa Spika huyo ni binadamu hivyo hawezi akakosa mapungufu hivyo baadhi ya wabunge wanataka kutumia udhaifu huo kumngo’oa katika nafasi hiyo.

0 comments:

Post a Comment