CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimeendelea kudhihirisha umwamba wake katika Mkoa wa Arusha,
ambapo kwa mara nyingine tena kimeipiga kikumbo CCM na kutwaa
halmashauri mpya ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Usa River.
Ushindi huo unakuja zikiwa ni siku chache tangu chama hicho kiitwae
Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha ambayo ilikuwa ikiongozwa na diwani
wa Chama Cha Mapinduzi, aliyefariki dunia.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na Halmasuri ya Arumeru Mashariki
kugawanywa, na hivyo kuunda halmashauri mpya ya mamlaka ya mji mdogo wa
Usa River.
Kabla ya kugawanywa, mitaa yote ilikuwa ikiongozwa na CCM na hivyo,
ikalazimika viongozi hao wajiuzulu ili uchaguzi ufanyike upya wa
kuwapata wenyeviti wapya wa mitaa tisa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana jioni, tayari CHADEMA kilikuwa
kimejizolea ushindi mkubwa katika mitaa sita, huku CCM kiking’ara
kwenye mitaa mitatu.
Mitaa hiyo na kura zake kwenye mabano ilikuwa Manyata Kati (CHADEMA
118, CCM 78), Nganana (CHADEMA 127, CCM 117), Kisambare (CHADEMA 613,
CCM 190), Ngarasero (CHADEMA 785, CCM 355) na Magadini ambako CHADEMA
walipata kura 303 dhidi ya 106 za CCM.
Hata hivyo, CCM ilifanikiwa kurejesha mitaa mitatu ya Magadirisho, Mlima Sioni na Usa Madukani.
Kwa ushindi huo, CHADEMA sasa wamefanikiwa kuongoza halmashauri ya
pili katika Mkoa wa Arusha, kwani kwa zaidi ya miaka kumi wamekuwa
wakiongoza Halmashauri ya Wilaya ya Karatu.
Akizungumza kwa simu jana, Katibu wa CHADEMA Mkoa
wa Arusha, Amani Golugwa, alisema kuwa wanataka kuifanya halmashauri
mpya ya Usa River iwe ya mfano katika Jiji la Arusha.
“Tumejipanga kuiboresha Usa River kuanzia usafi, mapato na
miundombinu yake, kwani CCM wamekuwa wakisuasua, lakini sasa
wameachia,” alisema.
CHADEMA kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa CCM katika Mkoa wa
Arusha kwani hata kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la
Arumeru Mashariki, chama hicho kilitwaa kiti hicho kilichokuwa
kikikaliwa na wapinzani wao baada ya aliyekuwa mbunge kufariki
chanzocha habari: tanzania daima.
0 comments:
Post a Comment